Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Azam zazidisha uzungu vikosini mwao

Kocha wa Azam, Stewart Hall

Muktasari:

Wachezaji wa benchi katika timu hizo bora zaidi nchini kwa sasa, wanawazidi kwa mbali wachezaji wa vikosi vya kwanza vya timu nyingine za Ligi Kuu Bara.

KINACHOFANYIKA Yanga na Azam ni uzungu na weledi wa aina yake. Matokeo ya furushi lililomwagwa kwenye usajili wao yameanza kuonyesha jinsi ufundi wa kizungu unavyoweza kufanya kazi. Sasa maisha katika klabu hizo yameanza kuwa kama ya klabu za Ulaya kuanzia kwenye kupanga vikosi.

Hali hiyo inaweza kuanza kuonekana keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa zitakapocheza mechi ya Ngao ya Hisani. Uchunguzi mdogo uliofanywa na Mwanaspoti umebaini kuwa Azam na Yanga zinaweza kuchezesha vikosi vya pili na mashabiki wa soka wasigundue. Kitendo hicho ni sawa na kupumzisha majembe, yaani wachezaji mahiri zaidi wa timu hizo. 

Wachezaji wa benchi katika timu hizo bora zaidi nchini kwa sasa, wanawazidi kwa mbali wachezaji wa vikosi vya kwanza vya timu nyingine za Ligi Kuu Bara.

Kikosi cha kwanza Yanga

Kwa namna upepo unavyokwenda sasa, kikosi cha kwanza cha Yanga kitaundwa na Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Thaban Kamusoko, Geofrey Mwashiuya, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke.

Kikosi cha kwanza Azam

Azam tayari pia imepata kikosi cha kwanza na kitaundwa na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Sergie Wawa, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Frank Domayo, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, John Bocco, Kipre Tchetche na Farid Mussa.

Achana na vikosi hivyo viwili ambavyo bila ubishi wowote ndiyo bora zaidi nchini kwa sasa. Kikosi cha kwanza cha Simba pia kinaonekana kuwa na makali kama hayo na kufuatiwa na Mwadui FC itakayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu.

 Kama wataamua Yanga na Azam zinaweza kutumia vikosi vyao vya pili katika mechi yao ya Jumamosi na kutoa burudani ile ile kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ndiyo mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Vikosi vya benchi

Langoni

Kipa namba mbili wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ bado ni bora nchini. Anawapiku makipa wengi namba moja wa timu nyingine za Ligi Kuu. Ubora wake na wa Barthez ni kama unalingana kwa kiasi fulani na akianza Yanga inakuwa haina shaka langoni.

Upande wa Azam kipa namba mbili, Mwadini Ali hafikii makali ya Manula kwa sasa, lakini ni bora zaidi ya makipa wengi namba moja nchini. Kwanza Mwadini ni mzoefu na hodari wa michomo ya juu.

Mabeki

Mabeki wa benchi wa Yanga ambao wanaweza kuanza na kutoa burudani murua ni Mbuyu Twite kwa upande wa kulia, Oscar Joshua kwa upande wa kushoto na Pato Ngonyani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mabeki wa kati. Ikumbukwe kuwa Cannavaro ambaye ni nahodha wa timu hiyo anampisha Bossou katika kikosi cha kwanza lakini bado ana vitu vingi adimu ambavyo mabeki wetu wengi hawana. Ngonyani hana uzoefu mkubwa lakini katika mechi alizopata nafasi ya kucheza amekuwa akionyesha uwezo wa kuvutia.

Azam nayo ina mabeki wa kikosi cha pili ambao wanaweza kuanza na kuonyesha makali vilivyo. Mabeki hao ni Himid Mao upande wa kulia, Gadiel Michael upande wa kushoto na Said Morad na David Mwantika kama mabeki wa kati. Mabeki hawa wote licha ya kuwa kikosi cha pili pale Azam ni wa viwango vya juu na wanaweza kupata nafasi katika vikosi vya kwanza vya timu zaidi ya 10 nyingine za Ligi Kuu.

Viungo

Baada ya usajili uliofanyika hivi karibuni Yanga sasa ina viungo ambao wanaweza kuonyesha vitu vya tofauti. Timu hiyo inaweza kuwatumia Said Juma ‘Makapu’ katika nafasi ya kiungo mkabaji na Salum Telela akiwa kiungo mchezeshaji na mechi bado ikawa na utamu uleule.

Azam ina utajiri wa viungo wa benchi ambao timu nyingine zinawamezea mate. Timu hiyo ina viungo watatu mahiri ambao hawana nafasi katika kikosi cha kwanza. Ina Kipre Bolou, Mudathir Yahya na Bryson Raphael. Hall anaweza kuamua kuwatumia viungo hao watatu kwa wakati mmoja ama kuwatumia wawili pekee.

Mawinga

Yanga ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara inaweza kuwapanga washambuliaji wake wa pembeni Andrey Coutinho na Simon Msuva ambao hawana nafasi katika kikosi cha kwanza na timu hiyo ikatoa burudani ya aina yake. Coutinho na Msuva licha ya kuwa kikosi cha pili Yanga wakienda timu nyingine 14 zinazoshiriki Ligi Kuu wanapata nafasi moja kwa moja katika vikosi vyao vya kwanza.

Azam nayo ina jeuri ya Ramadhan Singano, Mcha Hamis na Kelvin Friday ambao hawana nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Watatu hao wanamudu vizuri winga zote mbili na wakicheza burudani inakuwa palepale.

Mastraika

Hapa sasa ndipo ubora wa Yanga unapoonekana. Timu hiyo inaMalimi Busungu, Mateo Saimon na Hussein Javu benchi, ambao wanaweza kuanza katika kikosi cha kwanza na kuleta ushindani ule ule. Busungu na Mateo wana uwezo wa kuanza katika timu nyingi tu za Ligi Kuu.

Azam nayo ndiyo ina utitiri wa washambuliaji kwani benchi yupo Didier Kavumbagu, Allan Wanga na Ame Ali. Mastraika hawa wote ni wa viwango vya juu na wanazijua nyavu kweli kweli lakini pale Azam watakuwa katika kikosi cha pili.

Gharama

Gharama za kikosi cha pili cha Yanga kinakadiriwa kufikia zaidi ya Sh200 milioni ambayo ni wastani wa Sh18 milioni kwa usajili wa mchezaji mmoja mmoja.

Azam  ni zaidi kwani safu yake ya ushambuliaji pekee yenye Wanga, Kavumbagu, Singano na Ame inakadiriwa kuzidi Sh180 milioni fedha ambazo zinaweza kusajili kikosi cha kwanza Mtibwa Sugar na African Sports na chenji ikabaki. Kwa jumla kikosi cha benchi cha Azam kinakadiriwa kufikia Sh300 milioni, zinazidi gharama ya kikosi cha kwanza cha Simba.