Yanga, Azam FC zategwa fainali Kombe la Shirikisho

Muktasari:

Akizungumzia droo hiyo ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema moja ya mambo waliyokuwa wanayahitaji ni kukutana na Azam FC.

DROO ya robo fainali na nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) imefanyika huku ikionyesha huenda mabingwa watetezi Yanga wakakutana na Azam FC kwenye fainali itakayofanyika Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite, Babati.

Katika droo hiyo, Ihefu iliyoitoa KMC kwa mabao 3-0 itakutana na Mashujaa iliyoiondosha Simba kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya timu hizo kufungana bao 1-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.

Coastal Union iliyoitoa JKT Tanzania kwa penalti 5-4 itacheza na Geita Gold iliyoifunga Rhino Rangers mabao 2-1, huku Azam FC iliyoitoa Mtibwa Sugar kwa 3-0 itacheza na Namungo iliyoifunga Kagera Sugar kwa penalti 5-3 baada suluhu dakika 90.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo msimu uliopita, Yanga ambao walifuzu kwa kuifunga Dodoma Jiji mabao 2-0, watakutana na Tabora United ambayo iliitoa Singida Fountain Gate kwa mabao 3-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kwenye hatua ya nusu fainali, mshindi kati ya Azam FC na Namungo atakutana na atakayepenya kati ya Coastal Union na Geita Gold huku mshindi wa Ihefu na Mashujaa atacheza na atakayefuzu kati ya Yanga na Tabora United.

Michezo ya robo fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa kati ya Mei 2-4 huku ile ya nusu fainali ikipigwa kati ya Mei 18 hadi 19.

Fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu inatarajiwa kupigwa Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite, uliopo Babati Manyara.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1967 ikifahamika kwa jina la FAT kabla ya 2015 kubadilishwa na kuitwa ASFC, Yanga ndio timu iliyotwaa mara nyingitaji hilo ikifanya hivyo mara saba kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.

Mbali na Yanga, timu nyingine iliyofika hatua hii iliyochukua ubingwa wa michuano hiyo ni Azam FC iliyofanya hivyo msimu wa 2018-2019 baada ya kuifunga Lipuli ya Iringa kwa bao 1-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu uliopo mjini Lindi.

Akizungumzia droo hiyo ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema moja ya mambo waliyokuwa wanayahitaji ni kukutana na Azam FC.

"Sisi kama mabingwa watetezi tumejipanga kutetea ubingwa wetu, niwashukuru TFF na wote waliohusika kwenye upangaji ila ikitokea Tabora wakaandika barua ya kubadilishiwa mpinzani basi sisi tupo tayari kwa lolote litakalotokea," alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema wao kufika hatua hiyo ni jambo nzuri na kubwa kwao ingawa kazi iliyopo mbele ni kujipanga vizuri kwani hakuna timu dhaifu iliyofika kwenye robo fainali ya mashindano hayo kwa bahati mbaya.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema licha ya ugumu uliopo ila watahakikisha wanafanya vizuri na kuchukua ubingwa kutokana na kukaa kwa muda mrefu tangu mara ya kwanza na ya mwisho walipolichukua msimu wa 2018-2019.