Yanga akiumia beki mmoja basi

Muktasari:
Kocha huyo amekuwa akimuweka jukwaani mchezaji huyo mara kadhaa na pale inapotokea tatizo ndani ya uwanja humtumia Twite ambaye ni kiraka.
YANGA ina ukuta mzuri sana ambao ni nadra kuruhusu mabao, lakini kumbe akikosekana mchezaji mmoja tu katika safu yake mambo yanaharibika na mipango yote ya timu inakufa na haina mbadala wa beki wa kushoto.
Ikiwa chini ya Kocha Marcio Maximo, Yanga ilicheza mechi tano za kirafiki na kutoruhusu hata bao moja lakini wikiendi iliyopita iliruhusu mabao mawili dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.
Safu ya ulinzi ya Yanga inaundwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’, beki wa kulia Juma Abdul, kushoto yupo Oscar Joshua na katikati wapo Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Hadi sasa Yanga haina mbadala wa Joshua na hilo lilijitokeza dhidi ya Mtibwa ambapo Maximo ilibidi amrudishe Mbuyu Twite kushoto na kutoka namba sita kisha kumuingiza Omega Seme kwenye nafasi hiyo. Joshua alikuwa ameumia nyama za paja.
Omega alionekana kutomudu katikati hivyo kuruhusu mashambulizi mengi ya Mtibwa. Hata hivyo inaonekana Joshua hana mbadala kwani beki mwingine wa kushoto Edward Charles anaonekana kutokubalika na Maximo kwavile haendani na staili yake ya uchezaji.
Kocha huyo amekuwa akimuweka jukwaani mchezaji huyo mara kadhaa na pale inapotokea tatizo ndani ya uwanja humtumia Twite ambaye ni kiraka. Lakini habari za ndani zinadai kwamba Maximo amejadiliana kwa kina na viongozi wa Yanga kuhusiana na mustakabali wa Edward na kwamba ataanza kumpa nafasi kidogo kidogo.
Mchezaji huyo alikuwa akiwaniwa na Simba awali kabla ya Yanga kuingilia na kumsainisha Maximo akiwa hamjui wala hakuwahi kumuona. Yanga Jumapili wiki hii itacheza na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.