Yanga akili kubwa, Yacouba OUT

BAADA ya mapumziko ya siku 10 tangu walipocheza mchezo wa mwisho, Yanga jana ilirudi mazoezini kuanza kujiandaa na muendelezo wa ligi na ratiba yao iko hivi.
Kikosi hicho kimerudi kazini kikiwa chini ya kocha msaidizi Cedric Kaze na ratiba ya kwanza wataanzia gym katika kurudisha utimamu wa mwili, huku mabosi wao wakitumia akili kubwa kwenye usajili.
Hata hivyo, ratiba hiyo itakuwa na mtego ndani yake kwani wachezaji wote walipewa programu maalum ya kufanya katika mapumziko yao ambapo makocha hao wataanza kuiangalia hapo jinsi utekelezaji huo ulivyofanyika sawasawa chini Kaze.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo zinasema kwamba kama kutabainika kwamba kuna wachezaji hawakufuata maelekezo sahihi wanaweza kukumbana na kitu kizito katika mazoezi yao ndani ya Kambi yao iliyopo Avic Town Kigamboni.
Wakati Yanga ikirejea kambini mshambuliaji Yacouba Sogne, dili lake la kupewa mkataba mpya limeota mbawa rasmi kufuatia timu hiyo kukosa nafasi yake.
Yanga ilikuwa inafikiria kumrudisha Yacouba kikosini hata hivyo, hilo halitaweza kutimia kutokana na nafasi finyu ya wachezaji wa kigeni waliyonayo na hivyo wanarudi tena mezani.
Yanga inataka kuingiza mastaa wawili wa kigeni wakiwemo mshambuliaji Kennedy Musonda, ambaye Mwanaspoti linajua ameshasaini dili la miaka miwili akitokea Power Dynamos ya Zambia.
Hata hivyo, baada ya Yacouba, msala mwingine upo kwa kiungo Gael Bigirimana amabye inaelezwa kuvunja mkataba wake ni gharama kubwa au winga Tuisila Kisinda ambapo mmoja wapo anaweza kupoteza nafasi kupisha usajili wa beki wa kati mpya wa kigeni ambaye ataingia kabla usajili haujafungwa.
Hesabu za Yanga ni kwamba kama watamtoa Bigirimana ambaye hajafunga bao wala kutoa pasi ya bao msimu huu, uongozi unatumia akili kubwa sana, wanataka kutumia kifungu cha sheria cha kushindwa kucheza kwa asilimia 30 katika kikosi hicho baada ya Mrundi huyo kusotea sana benchi akikosa nafasi ya moja kwa moja ili kuepuka msala.
Kwa upande wa Kisinda, mabosi wanakuna vichwa kumuacha kwani jamaa ameanza kuchanganya katika kiwango chake ingawa kumuacha kwake ni jambo rahisi zaidi kutokana na kuwa Yanga kwa mkopo akitokea RS Berkane ya Morocco na hivyo ni kiasi cha kuwasiliana na timu yake tu.