Yaliyojiri tangu Mgosi afunge bao la mwisho

Muktasari:
Mgosi alirejeshwa Msimbazi msimu huu akitokea Mtibwa Sugar aliyoichezea kwa misimu mitatu. Straika huyo alianza kwa kasi Simba na kufanikiwa kuteuliwa kuwa nahodha, lakini ameshindwa kabisa kuifungia timu hiyo bao lolote kwenye Ligi na hata katika mashindano mengine.
INATIA huruma. Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/10, Mussa Hassan Mgosi, hajafunga bao lolote tangu Aprili mwaka jana, hivyo kutimiza zaidi ya siku 330 bila kuona nyavu. Huu ni muda mrefu mno kwa straika huyo aliyewahi kutikisa nchi kwa umahiri wake wa kufumania nyavu.
Mgosi alirejeshwa Msimbazi msimu huu akitokea Mtibwa Sugar aliyoichezea kwa misimu mitatu. Straika huyo alianza kwa kasi Simba na kufanikiwa kuteuliwa kuwa nahodha, lakini ameshindwa kabisa kuifungia timu hiyo bao lolote kwenye Ligi na hata katika mashindano mengine.
Hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa Mgosi na kusababisha kuachwa na Simba mwishoni mwa msimu kama atashindwa kufunga bao lolote katika mechi sita za Ligi Kuu zilizosalia na kumaliza msimu. Hiyo inaweza kuwa rekodi kwake na itakuwa ni mara ya kwanza kutokea kwenye maisha yake ya soka.
Kasi ya wapachika mabao, Hamis Kiiza anayeongoza akiwa na mabao 19, Ibrahim Ajib mwenye mabao tisa na Danny Lyanga mwenye mabao manne imesababisha Mgosi awe anapewa dakika chache za kucheza kwenye kikosi cha Kocha Jackson Mayanja.
Mwanaspoti leo linaangazia mambo yaliyotokea tangu Mgosi alipofunga kwa mara ya mwisho Aprili mwaka jana dhidi ya Azam.
KIMICHEZO
Katika sekta ya michezo mambo kadhaa yametokea tangu straika huyo ambaye amewahi kuifunga Yanga mara nne alipofunga bao lake la mwisho Ligi Kuu.
1. TRA yasepa na mkwanja wa TFF
Wakati Mgosi akisaka bao Ligi Kuu, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilizipitia akaunti za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuchota fedha zote ikiwa ni jitihada za kulilazimisha shirikisho hilo lilipe madeni linayodaiwa na TRA. TFF ilikuwa na deni kubwa TRA kutokana na kuweka malimbikizo katika malipo ya kodi za makocha wa kigeni waliowahi kuifundisha Taifa Stars na timu za taifa za vijana.
2. Mkwasa apewa Stars
Wakati Mgosi akipambana kusaka bao Ligi Kuu, aliyekuwa kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliteuliwa kuwa kocha wa muda wa Taifa Stars akirithi mikoba ya Mholanzi Mart Nooij aliyetimuliwa Juni mwaka jana. Mkwasa baadaye alipewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuifundisha Stars, hivyo kuachana na Yanga iliyompa ajira Juma Mwambusi akitokea Mbeya City. Mkwasa aliiongoza Stars kuondoshwa kwa aibu na Algeria katika kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa kipigo cha mabao 7-0 kwenye mchezo wa marudiano nchini Algeria baada ya sare ya mabao 2-2 Dar es Salaam, lakini Mgosi bado hajafunga.
3. Samatta atua Ulaya
Wakati Mbwana Samatta anatwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Mgosi alikuwa kapa. Samatta baadaye alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika, lakini hadi wakati huo Mgosi bado alikuwa hajafunga. Wiki chache Samatta alijiunga na KRC Genk ya Ubelgiji na ameshaifungia timu hiyo mabao mawili lakini bado Mgosi hajafunga. Ni noma kweli.
4. Kiiza atua Simba, atupia 23
Wakati Mgosi akiwa anasaka bao la kwanza Ligi Kuu straika Hamis Kiiza anasajiliwa na Simba na mpaka sasa ameifungia timu hiyo mabao 23 kwenye Ligi na Kombe la FA. Kiiza aliingia Simba sambamba na Mgosi ambaye kwa wakati huo alikuwa tayari ameandamwa na ukame wa mabao. Wakati huo huo Yanga imemsajili straika Mzimbabwe Donald Ngoma aliyeifungia timu hiyo mabao 18 katika michuano ya Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Mapinduzi.
KISIASA
Katika medani ya siasa mambo kadhaa yametokea wakati Mgosi akisaka bao lake la kwanza Ligi Kuu ndani ya kipindi hicho.
1. Lowassa atua Ukawa
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini baadaye jina lake lilikatwa na kuamua kutua Ukawa. Wakati wote huo wa mchakato Mgosi alikuwa bado hajafunga. Lowassa aligombea urais kwa tiketi ya Ukawa na kupata kura zaidi ya milioni sita, ila mambo yalikuwa magumu kwa Mgosi ambaye mpaka sasa bado hajafunga.
2. Magufuli Rais, atumbua majipu.
Akiwa hapewi nafasi kabisa hata ya kuwania urais, John Magufuli anapitishwa na CCM kugombea na kisha kushinda nafasi hiyo ya juu zaidi nchini. Wakati huo wote wa mchakato, Mgosi alipita bila kufunga bao na hadi sasa Magufuli akiwa anatumbua majipu bado Mgosi anataabika.
3. Mwapachu aondoka, arejea CCM
Balozi Juma Mwapachu alitimka CCM katikati ya mwaka jana wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea na wiki iliyopita alirejea katika chama hicho, lakini Mgosi bado hajafunga bao. Mwapachu alidai kutoridhishwa na mwenendo wa CCM na kujiweka kando lakini sasa karejea baada ya kuridhishwa na kasi ya Magufuli lakini bado Mgosi anatafuta bao la kwanza.
KIUCHUMI
Katika medani ya uchumi mambo kadhaa yamejiri wakati Mgosi akisaka bao lake la kwanza.
1. Kuporomoka kwa shilingi
Shilingi ya Tanzania imeporomoka vilivyo mbele ya Dola ya Marekani wakati ambao Mgosi anatafuta bao. Wakati Mgosi alipofunga bao lake la mwisho Ligi Kuu, Dola moja ilikuwa sawa na Sh1600, lakini sasa wakati akiwa anapambana kufunga tena Dola 1 imekaribia kufikia 2200. Ni ajabu na kweli.