Yacouba aipeleka Yanga robo fainali ASFC

Muktasari:

Bao la dakika ya 53 likifungwa na mshambuliaji Yacouba Sogne limetosha kuivusha Yanga kwenda hatua ya Robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuwachapa wenyeji Prisons kwa bao 1-0.

Bao la dakika ya 53 likifungwa na mshambuliaji Yacouba Sogne limetosha kuivusha Yanga kwenda hatua ya Robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuwachapa wenyeji Prisons kwa bao 1-0.

Bao hilo ambalo lilipeleka furaha kwa Wanajangwani limetokana na pasi mujarabu ya Said Ntibazonkiza 'Saido' aliyewatoka mabeki na kupiga 'killerpass' iliyomkuta Yacouba ambaye naye alitulia na kuchagua wapi auweke mpira huo.

Ushindi huo unaifanya Yanga kivunja mwiko wa miaka mingi kushindwa kushinda katika uwanja huo wakiwatupa nje Prisons ambao wamekuwa wagumu kupoteza mbele ya vigogo katika uwanja huo.

Yanga ndio waliouanza kwa kasi mchezo huo ambao umechezwa katika uwanja wa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela na dakika ya kwanza tu wanafanya shambulizi kali kufuatia shambulizi la mpira wa kona ya Carlos Sterios 'Carlinhos' Yacouba anashindwa kufunga kwa tik tak.

Katika mchezo huo, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu zote zikienda mapumziko zikiwa bado hazijafungana.

Kwa ushindi huo Yanga wanakuwa timu ya tano kutinga hatua ya robo fainali ikitanguliwa na Mwadui ambayo imekuwa timu ya nne kufuzu hatua hiyo baada ya kuiondoa Coastal Union kwa kuifunga mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa mcha wa leo Ijumaa.

Timu nyingine ambazo tayari zimeshajikatia tiketi ya kucheza robo fainali ni pamoja na Rhino Rangers, Biashara United na Azam FC ambazo zilifuzu mapema jana.