WPL ukizubaa imekula kwako

Muktasari:

  • Bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Simba Queens ameendelea kuonesha nia ya kutaka kombe hilo tena baada ya kuongoza kwenye msimamo kwa pointi 26 sawa na Fountain Gate Princess.

MBEYA. WAKATI mzunguko wa 11 wa ligi kuu ya Wanawake ukimalizika juzi vita ya ubingwa imeendelea kuwa ngumu kufuatia timu nne za juu kukabana koo kwenye mbio za kuwania taji msimu huu.

Bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Simba Queens ameendelea kuonesha nia ya kutaka kombe hilo tena baada ya kuongoza kwenye msimamo kwa pointi 26 sawa na Fountain Gate Princess.

JKT Queens wapo nafasi ya tatu kwa pointi 25 huku Yanga Princess wakiwa nafasi ya nne kwa alama 21 na kufanya vita msimu huu kuwa nzito kwenye kuwania ubingwa.

Hata wakati wababe hao wakitoana jasho huko juu, pia timu za The Tigers Queens, Aman Queens na Mkwawa Queens zinajipapatua kukwepa kushuka daraja huko mkiani.
The Tigers wamekusanya pointi saba katika nafasi ya nane,

Aman Queens nafasi ya tisa kwa pointi nne na Mkwawa wakifunga hesabu kwa alama mbili.
Kocha mkuu wa Fountain Gate Princess, Masoud Juma alisema bado ni mapema kutambia ubingwa, lakini malengo yao msimu huu ni kutwaa taji hilo akisema mechi zilizobaki ni vita ya pointi hadi kieleweke.

Alisema kinachowapa nguvu na matumaini ni usajili bora na kujituma kwa mchezaji mmoja mmoja na kwamba lazima wafanya kazi ya ziada ili kufikia malengo yao msimu huu

“Hadi sasa bingwa atatoka kwenye zile nafasi nne za juu ambapo na sisi tuko hapo hapo, kimsingi ni kucheza kwa malengo kwa kuwaheshimu wapinzani bila kujali mazingira aliyopo,” alisema Juma.