Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Winga Mganda anukia Azam

Muktasari:

  • Taarifa kutoka Uganda, zinaeleza nyota huyo yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho baada ya kufikia makubaliano kati yake na klabu inayommiliki, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja unaoisha Juni 30, 2027.

UONGOZI wa Azam FC, uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga raia wa Uganda, Hassan Mubiru kutokea SC Villa ya Uganda, baada ya nyota huyo kuridhia kujiunga na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam msimu wa 2026-2027.

Taarifa kutoka Uganda, zinaeleza nyota huyo yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho baada ya kufikia makubaliano kati yake na klabu inayommiliki, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja unaoisha Juni 30, 2027.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif, alisema suala lolote linalohusu usajili au kuboresha mkataba wa mchezaji wowote wa klabu hiyo watatoa taarifa rasmi, hivyo kwa sasa ni mapema pia kuzungumzia hilo.

Licha ya kauli hiyo, Mwanaspoti linatambua mchezaji huyo ana asilimia kubwa za kujiunga na kikosi hicho, baada ya kuonyesha kiwango bora msimu wa 2025-2026, akiwa na SC Villa aliyochangia mabao 13 kati ya 47 yaliyofungwa na timu hiyo.

Katika Ligi Kuu ya Uganda, Mubiru ameifungia SC Villa mabao sita na asisti saba, akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara tano, huku akikiwezesha kikosi hicho kumaliza msimu wa 2025-2026, kikiwa nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi 61.

Mubiru aliyezaliwa Julai 25, 2004, licha ya ubora wake, anatarajiwa kukutana na ushindani na nyota wengine wa timu hiyo, Idd Seleman 'Nado', Mzee Hassan Mzee, Abdul Suleiman 'Sopu' na Mnigeria Abel Abah wanaocheza nafasi yake.

Winga huyo alijiunga na SC Villa Julai 31, 2024, akitokea KCCA FC ya kwao pia Uganda, akiwa ni miongoni mwa nyota wenye kipaji kikubwa, huku akitabiriwa kufanya mambo makubwa licha ya ushindani wa nafasi katika kikosi hicho cha Azam.