William Edgar aingia anga za Azam
Muktasari:
- Edgar aliyemaliza msimu wa 2025-2026, akifunga mabao saba ya ligi huku ule wa 2024-2025 wakati anaichezea Fountain Gate akimaliza na mabao sita, hata hivyo, bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Dodoma, hivyo uongozi wa Azam unaangalia namna ya kumalizana na timu hiyo.
STRAIKA wa Dodoma Jiji, William Edgar, anafanya mazungumzo na Azam FC ili kufanya naye kazi msimu ujao wa 2026-2027 wakiamini anaweza akawa na mchango katika kikosi chao.
Edgar aliyemaliza msimu wa 2025-2026, akifunga mabao saba ya ligi huku ule wa 2024-2025 wakati anaichezea Fountain Gate akimaliza na mabao sita, hata hivyo, bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Dodoma, hivyo uongozi wa Azam unaangalia namna ya kumalizana na timu hiyo.
Chanzo kutoka Azam kilisema: “Edgar ni kati ya washambuliaji wazawa wenye uwezo mkubwa, hivyo tunaamini endapo tukifanikisha kumsajili atakuwa na mchango katika timu.” Endapo Azam ikifanikiwa kumsajili Edgar, katika nafasi ya ushambuliaji anakwenda kupambania namba na Jephte Kitambala aliyemaliza na mabao saba na kulikuwa na tetesi za huenda wakaachana naye. Pia kuna Jean-Jacques Ngita (mabao sita), Zidane Ally Sereri (mabao mawili) na Nassor Saadun (bao moja).
Ukiachana na Azam, nyota huyo aliwahi kuhusishwa kutakiwa na Simba.
Alipotafutwa Edgar kuhusiana na taarifa hizo, alisema bado ni mchezaji wa Dodoma Jiji, hivyo hawezi kuzungumzia masuala ya kutakiwa na timu nyingine.
“Hizo ni tetesi tu, kwa sasa mimi naendelea na mapumziko baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu, hivyo sitakuwa na nafasi ya kuzungumza wakati mimi ni mwajiriwa wa Dodoma,” alisema Edgar.