Polisi Tanzania, Mbeya kwanza mwisho wa ubishi
Muktasari:
- Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Juni 28, 2026, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Polisi Tanzania ilishinda mabao 4-0, hivyo, inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga hatua inayofuata.
VITA ya kuisaka tiketi ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, inaendelea tena leo kwa mechi ya pili ya Play-Off, kati ya maafande wa kikosi cha Polisi Tanzania dhidi ya Mbeya Kwanza, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini, Moshi.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Juni 28, 2026, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Polisi Tanzania ilishinda mabao 4-0, hivyo, inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga hatua inayofuata.
Timu hizo zinakutana hatua hiyo baada ya Polisi kumaliza nafasi ya tatu na pointi 66, katika Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, huku kwa upande wa Mbeya Kwanza yenye maskani yake Tabora ikimaliza nafasi ya nne na pointi zake 61.
Katika mechi mbili za msimu huu wa 2025-2026, kila timu imeshinda nyumbani kwake, ikianza Mbeya Kwanza iliyoshinda mabao 4-2, Januari 11, 2026 kisha raundi ya pili kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, Polisi ikashinda pia bao 1-0, Juni 14, 2026.
Mbeya Kwanza iliyouzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu uliopita wa 2024-2025, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, baada ya kumaliza mkiani mwa nafasi ya 16, ikiwa imekusanya jumla ya pointi zake 25.
Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Polisi msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Salvatory Edward alisema licha ya kupoteza mechi ya kwanza kwa idadi kubwa ya mabao nyumbani ila bado hawajakata tamaa pia, licha ya kukiri ugumu wanaoenda kukutana nao ugenini kutokana na ubora wa wapinzani wao. “Kama wapinzani wetu walishinda ugenini na sisi pia tunaweza kushinda, mechi ya kwanza tulikosa utulivu wa kutumia vyema nafasi za kufunga tofauti na wenzetu, kikubwa tumefanyia kazi upungufu huo na tuko tayari kwa vita,” alisema Salvatory.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata alisema ushindi wa mechi ya kwanza umewapa matumaini makubwa na kuwaongezea hatua moja mbele, japo wataendelea kupambana pia ili kuhakikisha wanatumia vyema uwanja wao wa nyumbani. Mshindi wa jumla wa Polisi Tanzania na Mbeya Kwanza, itacheza Play-Off nyingine na timu itakayopoteza ya Ligi Kuu kati ya Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 32, dhidi ya Mbeya City iliyoshika nafasi ya 14 na pointi 30.