Waziri Masauni ataka vipaji vitunzwe

Muktasari:
- Waziri Masauni aliyasema hayo juzi wakati akikagua ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa TAYI uliopo Jimbo la Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Zanzibar alipokuwa katika ziara ya kikazi na kuongeza, vijana wanapaswa kupewa nafasi kuonyesha vipaji vyao.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yussuf Masauni amesema michezo ni fursa inayowawezesha vijana wengi ambao wameamua kuendeleza vipaji vyao kujiajiri, endapo kutakuwa na mazingira rafiki kwao ya kuviendeleza.
Waziri Masauni aliyasema hayo juzi wakati akikagua ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa TAYI uliopo Jimbo la Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Zanzibar alipokuwa katika ziara ya kikazi na kuongeza, vijana wanapaswa kupewa nafasi kuonyesha vipaji vyao.
Alisema uwepo wa mazingira mazuri ya kujifunzia kutawasaidia kuongeza morali na mwishowe kupata ajira ambayo itawasaidia kuendesha maisha yao, wazazi pamoja na kuongeza pato la taifa kutokana na michezo.
“Mtoto anapokuzwa katika akademia hizi anakuwa kwenye maadili mazuri ya kimichezo na hii itasaidia hata kupata ushirikiano katika mataifa mbalimbali kujiunga na timu zao kwa kuangalia makuzi yake ya michezo.
Waziri Masauni ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni eneo ambalo linajengwa uwanja huo alisema kuwepo kwa uwanja huo utasaidia hata watu wazima kufanya mazoezi ikiwa ni moja ya njia ya kulinda afya zao.
Mkandarasi wa uwanja huo, Rajabu Pazi alisema uwanja huo unajumuisha majukwaa kwa ajili ya watazamaji, vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji, chumba cha waamuzi, chumba kwa ajili ya watu mashuhuri, madarasa kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ya akademia za michezo.
“Uwanja huu utajumuisha viwanja viwili vya mpira wa miguu na kimoja kina ukubwa wa mita 50 kwa 30 na kingine kina ukubwa wa mita 25 kwa 15. Pia kuna kiwanja cha mpira wa kikapu na eneo la michezo ya watoto.
Alisema hadi kufikia Julai mwaka huu mradi utafikia hatua ya mwisho ikiwemo ujezi wa viwanja vyote pamoja na uzio kwa kila uwanja na kubakisha hatua ya mwisho ya kutandika nyasi bandia.