Wawa: Nafasi yangu ipo Simba

Muktasari:
Beki wa Simba, Pascal Wawa amesema, hamu yake ni kuona timu yake inachukua ubingwa kwa mara nyingi na hana wasiwasi na nafasi yake ndani ya kikosi cha kwanza.
BEKI wa Simba, Pascal Wawa amesema, wataipigania klabu yao kuona inakuwa mwiba Ligi Kuu lakini anaendelea kuwa chaguo la kwanza la Kocha Patrick Aussems.
Wawa ambaye alikuwa na maumivu ya misuli tangu msimu wa Ligi Kuu Bara uanze alikosa mechi mbili dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar amerdui mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Alicheza mchezo huo pamoja na Mbrazil Tairone Santos da Silva, Erasto Nyoni alikuwa na matatizo ya kifamilia huku Kennedy Juma na Yusuf Mlipili hawakuwa kwenye programu ya Aussems.
Amesema, "Namshukuru Mungu kwa sasa hali yangu imekamilika kabisa na nipo fiti, binafsi naamini mechi zipo nyingi, nina muda na nafasi ya kuisaidia timu yangu ifanye vizuri.
"Hamu yangu ni kuiona Simba inakuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine kwa sababu inawezekana, kikubwa ni kupambana na kuweka nguvu katika kila mechi tunayocheza,"
"Lakini, katika harakati hizo napambana kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza. Sina wasiwasi sana katika hilo kwa sababu mechi za ligi ni nyingi tukipeana nafasi kila kitu kitakwenda vizuri," amesema Wawa.