Watanzania walivyochuana Olimpiki Argentina

Muktasari:

Timu ya Riadha na kuogelea ndizo ziliiwakilisha nchi kwenye michezo hiyo na wanamichezo wa Tanzania wote hawakufanya vizuri.

Dar es Salaam. Pamoja na kutoka kapa kwenye michezo ya vijana ya Olimpiki nchini Argentina, wamichezo wa Tanzania imeacha kumbukumbu mbili nzuri katika michezo hiyo itakayofungwa Jumanne Ijayo.

Tayari wanamichezo wote wa Tanzania wameaga mashindano hayo licha ya kubaki Argentina kama watazamaji hadi watakaporejea nchini Oktoba 21.

Muogeleaji, Sonia Tumiotto na mwanariadha, Francis Damiano wameacha kumbukumbu ya pekee kwenye michezo hiyo licha ya kutopata medali.

Damiano ameacha kumbukumbu ya kuchomoka kwa kasi kwenye mbio za mita 3000, mbinu ambayo Mara ya mwisho ilitumiwa na Mtanzania, Filbert Bayi mwaka 1974 kwenye michezo ya madola na kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500.

Damiano aliirudia mbinu hiyo Leo Oktoba 12, kwenye mbio za mita 3000 kwa kuchomoka kwa spidi na kuwaacha mbali wapinzani wake hadi mita 2000, lakini akaishiwa nguvu akiwa amebakiza umbali wa mita 1000 kumaliza mbio.

"Kama angekuwa na pumzi ya kulinda mbinu yake angefanya vizuri," alisema Kocha wa timu hiyo, Mwinga Mwanjala.

Damiano alimaliza wa 12, Sonia yeye aliweka rekodi ya kuwa Muafrika pekee aliyemaliza wa kwanza Katika makundi kwenye mtindo wa freestyle mita 100.