Prime
Wasauzi wawafuata Diarra, Mutale

Muktasari:
- Lengo kuu la Nabi kuwa uwanjani hapo ni kumsoma kwa ukaribu mmoja wa nyota machachari wa Simba sambamba na kufuatilia nyota wengine wawili ambao amewaainisha katika ripoti aliyoiwasilisha kwa mabosi wa Kaizer, jambo ambalo klabu za soka nchini zisipojipanga zitapoteza baadhi ya nyota wake.
KOCHA Mkuu wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, Jumatano wiki hii alikuwa jukwaani KMC Complex, jijini Dar es Salaam ili kushuhudia kiporo cha Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Singida BS, ikiwa ni saa chache tangu atoke kuwasilisha ripoti ya usajili ya timu hiyo akitaka kuboresha kikosi kwa msimu ujao.
Lengo kuu la Nabi kuwa uwanjani hapo ni kumsoma kwa ukaribu mmoja wa nyota machachari wa Simba sambamba na kufuatilia nyota wengine wawili ambao amewaainisha katika ripoti aliyoiwasilisha kwa mabosi wa Kaizer, jambo ambalo klabu za soka nchini zisipojipanga zitapoteza baadhi ya nyota wake.
Taarifa kutoka Afrika Kusini ni kwamba katika ripoti ya Nabi kuna mahitaji ya wachezaji watatu wanaocheza Ligi Kuu Bara, akiwamo Joshua Mutale wa Simba na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayetajwa kuwa ndiye mtu wa kwanza kocha huyo anamuhitaji.
Kaizer Chiefs kwa muda mrefu imekuwa ikiifukuzia saini ya Fei Toto, ambaye Nabi ni shabiki mkubwa wa kiungo huyo tangu alipokuwa naye Yanga.
Klabu hiyo iliwahi kutuma ofa ya Dola 350,000 (zaidi ya Sh 944 milioni) kwa Azam FC, kumnunua kiungo huyo, lakini matajiri wa Chamazi waligoma wakitaka Dola 500,000 (zaidi ya Sh 1.3 bilioni) ili kumuachia katika dirisha dogo la usajili lililopita.
Hata hivyo, Kaizer Chiefs kama itarudi tena kwa Azam kumwania kiungo huyo, itakumbana na upinzani mkali kwani Simba na Yanga nazo zinapambana kupata saini yake.
Mbali na Fei Toto, pia ripoti hiyo imemjumuisha kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra. Diarra bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, lakini analazimisha kutaka kuondoka huku klabu hiyo ikiendelea kupiga hesabu ndefu za nani ataziba nafasi yake.
Ndani ya Yanga, Mwanaspoti linafahamu kumeibuka kambi mbili moja ikitaka kipa huyo kubaki wengine wakitaka aruhusiwe kuondoka ambapo bado muafaka haujapatikana.
Staa wa tatu ambaye anatakiwa na miamba hiyo ni winga wa Simba Joshua Mutale, ambaye inaelezwa jina lake limeingiza hivi karibuni kufuatia kuonyesha makali katika mechi za Fainali ya Kombe La Shirikisho Afrika.
Inaelezwa mabosi wa juu wa Kaizer ndio wanamtaka zaidi Mutale, wakidai aliwahi kuwa kwenye rada zao wakati akiwa bado anacheza soka kwao Zambia, ambapo sasa Wasauzi hao watajaribu kumpata akitokea Simba.
Mutale ndiye aliyeifungia Simba bao pekee kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa fainali ya Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambapo Wekundu walipoteza kwa jumla ya mabao 3-1, ikianza kupoteza ugenini 2-0 na kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani.