Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba v Singida BS ni mechi ya kisasi, utamu uko hapa

KISASI Pict

Muktasari:

  • Hii ni mchi ya kisasi na iliyobeba matumaini ya Singida kuandika ukurasa mpya katika soka la Tanzania, huku kwa Simba ikiwa ni hatua ya kufosi kufika fainali ili kupigania ubingwa huo baada ya kulikosa kwa misimu mitatu mfululizo na kupoteza Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi iliyopita.

NGOJA TUONE. Baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya Simba katika Ligi Kuu Bara, Singida Black Stars leo ina nafasi ya kulipa kisasi katika pambano la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), linalopigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Babati, mkoani Manyara.

Hii ni mchi ya kisasi na iliyobeba matumaini ya Singida kuandika ukurasa mpya katika soka la Tanzania, huku kwa Simba ikiwa ni hatua ya kufosi kufika fainali ili kupigania ubingwa huo baada ya kulikosa kwa misimu mitatu mfululizo na kupoteza Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi iliyopita.

Japo mechi hiyo inachezwa kwenye uwanja ambao hauna mwenyeji (neutral venue), kijiografia Babati ipo karibu zaidi na makazi ya Singida BS.

Safari kutoka Singida hadi Babati ni kati ya kilomita 150 hadi 180 tu, tofauti na Simba ambayo mashabiki wake italazimika kuvuka mikoa kadhaa kutoka Dar es Salaam.

Mechi hii inakuja wakati Simba ikiwa na ratiba ngumu ndani ya siku saba ikitakiwa kucheza mechi ya tatu, kwani ilianza kuumana na RS Berkane ya Morocco katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutoka sare ya bao 1-1 kisha Singida BS kwenye ligi.

Kwa upande wa Singida BS, hii itakuwa mechi ya pili ndani ya siku nne, baada ya kipigo cha bao 1-0 ilichokipata dhidi ya Simba katika Ligi Kuu Jumatano iliyopita.

Hivyo kwa pande zote mbili, uchovu na hali ya miili ya wachezaji vitakuwa na nafasi kubwa katika namna wanavyoweza kutimiza mikakati yao uwanjani.

Kwa Singida BS, huu ni wakati wa kutafuta heshima na kusafisha uso mbele ya mashabiki wao. Kufungwa mara mbili na Simba msimu huu ni jambo linalowauma ndani kwa ndani, lakini linaweza kuwa chachu ya kuleta mapinduzi.

Ni mara ya pili kwa timu hiyo kufika nusu fainali ya FA tangu ilipopanda daraja msimu wa 2020-2021. Msimu uliopita wakati huo ikiitwa Ihefu ilifika hatua kama hii baada ya kuitoa Mashujaa kwa penalti 4-3, kabla ya kutolewa na Yanga kwenye uwanja huu huu wa Babati. Safari hii, inataka kwenda mbali zaidi inaiona Simba kama daraja la kuikutanisha na historia.

Kocha wa Singida BS, Davids Ouma, anaonekana kuijenga timu kwa kusema matokeo mabaya dhidi ya Simba si sababu ya kukata tamaa.

Alisisitiza walinyimwa penalti mbili za wazi katika mechi iliyopita, na hiyo iliwakatisha tamaa, lakini sasa hawataki kulalamika bali kujibu mapigo uwanjani.

“Wachezaji wangu wameelewa ukubwa wa mechi hii. Tutapambana kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho. Tulinyimwa penalti mbili za wazi. Na kwa timu inayopambana dhidi ya klabu kubwa kama Simba, huwezi kupuuza matukio kama hayo. Lakini hatutaki kulalamika tena. Tutajibu kwa vitendo,” alisema Ouma, raia wa Kenya aliyewahi kuinoa Coastal Union na kuipa tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

3

Kwa upande wa Simba, Kocha Fadlu Davids anaifahamu presha ya mechi kama hii. Alisema huu si mchezo wa nusu fainali tu, bali ni fainali kamili kwao. Kwao hakuna nafasi ya kufikiria mechi inayofuata kila dakika ni ya vita.

Fadlu aliweka bayana kuwa Simba lazima icheze kwa nidhamu ya hali ya juu, umakini mkubwa, na nguvu zaidi ya ile waliyoonyesha dhidi ya RS Berkane.

“Hatua hii ya mashindano haikupi nafasi ya kurekebisha makosa. Tunapaswa kucheza kwa umakini mkubwa, nidhamu na nguvu kubwa zaidi ya tulivyofanya dhidi ya RS Berkane,” alisema Fadlu, aliyewasifu wachezaji wa timu hiyo hususani Steve Mukwala kwa kuonyesha kiwango bora n aliyefunga bao pekee mechi iliyopita.

“Takwimu zinaonyesha kuwa timu yetu ilikimbia zaidi ya kilomita 11.5 kwa kila mchezaji dhidi ya Berkane. Hii inaonyesha jinsi wachezaji wanavyojituma, na ndiyo tunahitaji Jumapili.”

Kwa upande wa mbinu, Simba inaonekana kuendelea na mfumo wao wa 4-2-3-1 mfumo unaowapa nafasi ya kulinda na kushambulia kwa kasi.

4
4

Katika mfumo huu, Fabrice Ngoma na Yusuf Kagoma kama ngome ya viungo, huku Charles Jean Ahoua akiwa kiungo mshambuliaji huru nyuma ya mshambuliaji wa kati ambaye anaweza kuwa Mukwala au Leonel Ateba. Pembeni, Simba ina chaguo la Kibu Denis, Ellie Mpanzu au  Joshua Mutale kuongeza kasi ya pembeni.

Kwa Singida BS, Kocha Ouma anaweza kutumia mfumo wa mabadiliko kati ya 4-3-3 na 4-2-3-1, kutegemea na aina ya presha kutoka kwa Simba. Atategemea mshambuliaji Jonathan Sowah, huku viungo kama Kelvin Nashon, Josephat Bada na Marouf Tchakei wakitakiwa kuwa na ubunifu na utulivu mkubwa katikati.

Pambano hili pia litakuwa la wachezaji wenye fomu kali. Sowah wa Singida BS mwenye mabao 11 ameendelea kuwa tishio langoni mwa wapinzani. Ni mfungaji mzuri, mwenye uwezo wa kutumia nafasi hata ndogo.

Kwa Simba, Mukwala ni mshambuliaji anayezidi kuimarika  ni mjanja, mwenye kasi, nguvu. Lakini vita halisi itakuwa katikati ya uwanja, eneo lililokuwa na ushindani mkali Jumatano,

 Mshindi wa mechi hiyo atakata tiketi ya kukutana na Yanga katika fainali itakayopigwa Juni 26-28.