Wasanii waanza kunufaika na viwanja vya Kigamboni

Muktasari:

Viwanja hivyo vinauzwa kwa wanamuziki na waingizaji wa filamu na wasanii wengine kwa bei nafuu

Dar es Salaam. Kufuatia ofa maalum ya wasanii kuuziwa viwanja kwa bei nafuu iliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Hashimu Mgandilwa tayari baadhi ya wasanii wameanza kuchangamkia fursa hiyo.

Mwanamuziki nyota nchini, Ally Choki jana alinunua rasmi kiwanja kutoka kampuni ya Datum ya jijini Dar es Salaam kwa bei elekezi iliyotolewa na mkuu huyo wa wilaya.

Ally Choki alifanya manunuzi hayo katika ofisi za kampuni ya Datum zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam nyuma ya hospital ya Regency akishuhudiwa na balozi wa kampuni hiyo Jacob Steven 'Jb'.

Kabla ya kuanza kufanya manunuzi hayo Jb alimuonesha Ally Choki ramani ya viwanja mbalimbali vinavyouzwa na kampuni hiyo na kumtaka achague akipendacho.

Ally Choki alimshukuru mkuu wa wilaya ya Kigamboni kwa kuwathamini wasanii na kuwataka wasikubali kupitwa na ofa hiyo.

"Ardhi ni kitu cha thamani sana. Nawaomba wasanii wenzangu wasipuuzie ofa hii, wafike kwenye ofisi za Datum wajipatie viwanja vilivyopimwa na vilivyopo kwenye maeneo rafiki na makazi ya watu," alisema.

Jb alimpongeza Choki kwa kununua kiwanja na kuwataka wasanii wengine waige mfano.

"Choki ameonesha njia na wengine wafuate. Hii ni ofa imetolewa wasiipuuze, hata kama msanii ana nyumba tayari au kiwanja haimzuii kuongeza kingine kama alivyofanya Ally Choki. Viwanja hivi vina hati kabisa na vipo maeneo mazuri yaliyotulia," alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Datum, Amos Masanja licha ya kumpongeza Ally Choki aliwataka wasanii wengine kwenda kununua viwanja hivyo na akasizitiza hata kama hawana pesa yote, wanaweza kukabidhiwa kwa utaratibu maalumu.