Wapinzani wa Simba, Yanga kujulikana Desemba 12

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetangaza rasmi droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile Kombe la Shirikisho ambayo itafanyika Jumatatu ya Desemba 12 katika makao makuu yake huko nchini Misri.

Awali droo hiyo ilipangwa kufanyika Novemba 16 ila ilishindwa kufanyika kutokana na kile ambapo CAF ilichoelezwa itapangiwa tarehe nyingine kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Simba na Yanga ndio timu pekee zinazoiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho huku zikiwa na muda mrefu wa kujiandaa kutokana na michezo yake kupigwa Februari mwakani.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika timu (16) zilizofuzu ni Al Ahly (Egypt), Al Hilal (Sudan), Al Merrikh SC (Sudan), Atletico Petroleos (Angola), Coton Sport (Cameroon), CR Belouizdad (Algeria), Esperance Tunis (Tunisia), Horoya (Guinea), JS Kabylie (Algeria) na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini),

Nyingine ni Raja Casablanca (Morocco), Simba SC (Tanzania), Vipers SC (Uganda), Wydad AC (Morocco), Zamalek (Egypt) na AS Vita Club (DR Congo).

Simba iko chungu namba tatu na timu za CR Belouizdad na JS Kabliye kutoka Algeria na Al Hilal ya Sudan ambayo inakumbukwa kwani iliinyima Yanga nafasi ya kutinga hatua makundi.

Kwenye Shirikisho ni Yanga (Tanzania), ASKO de Kara (Togo), DC Motema Pembe (DR Congo), Pyramids FC (Egypt), Rivers United (Nigeria), Al Akhdar SC (Libya), Diables Noirs (Congo) na TP Mazembe (DR Congo).

Zingine ni, ASFAR Club (Morocco), FC Saint Éloi Lupopo (DR Congo), US Monastir (Tunisia), AS Real Bamako (Mali), Future FC (Egypt), USM Alger (Algeria), Asec Mimosas (Ivory Coast) na Marumo Gallants ya Afrika Kusini.

Yanga iko kwenye ‘Poti’ ya pili pamoja na Motema Pembe ya DR Congo lakini timu hizo mbili haziwezi kukutana kwenye kundi moja lakini zitapangwa dhidi ya timu nyingine, moja kutoka poti namba moja ile ya kina TP Mazembe na timu nyingine mbili kutoka kwenye moja kati ya poti ya tatu na poti ya nne.