Wanatisha! Upepo upo kwao huu

WIKIENDI iliyopita, Jumapili, Simba na Yanga kila timu ilijua hatima yake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba ilifuzu hatua ya makundi wakiitoa Agosto ya Angola.
Yanga wao waliangukia kucheza mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Shirikisho hatua ya makundi baada ya kufungwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.
Achana na matokeo hayo, kwani baada ya kumaliza shughuli hiyo mipango yao iligeukia kwenye mechi ya dabi ya Kariakoo ikiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza.
Keshokutwa, Jumapili, Simba atakuwa mgeni wa Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa, ikiwa mara ya pili kwao msimu huu kukutana katika michuano yote baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika Ngao ya Jamii.
Kutokana na uimara wa vikosi hivyo kuna wachezaji wanaotarajiwa kufanya vizuri na wakang’aa kutokana na uwezo wao mkubwa walioonyesha hadi sasa katika mashindano yote.
MOSES PHIRI - SIMBA
Yanga wanapaswa kumchunga Phiri kwani ni mshambuliaji ambaye yupo kwenye kiwango bora tangu ajiunge Simba msimu huu akitokea Zanaco inayocheza Ligi Kuu Zambia.
Phiri ni mchezaji wa kikosi cha kwanza ingawa mechi ya Ngao ya Jamii hakucheza sababu wakati huo wa kocha Zoran Maki hakuwa chaguo lake lakini chini ya Juma Mgunda ni panga pangua na amefunga mabao tisa katika mechi tiza zilizopita za michuano yote.
Mechi yake ya kwanza kimashindano kucheza ilikuwa dhidi ya Geita Gold alifunga bao na tangu hapo amekuwa kwenye kiwango bora kwa kufunga mabao manne kwenye ligi akiwa amecheza mechi tano.
Ubora wa Phiri si kwenye mashindano ya ndani bali hata Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao matano katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika.
FISTON MAYELE - YANGA
Amekuwa katika kiwango bora tangu msimu uliopita alimaliza ligi akiwa nafasi ya pili kwenye ufungaji kwa mabao 16, moja nyuma kwa George Mpole aliyemaliza kinara wa ufungaji akiwa na mabao 17.
Msimu huu Mayele tayari amefunga mabao 13 katika mechi 10 za michuano yote, yakiwamo mawili aliyoifunga Simba katika mechi ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii, Yanga iliposhinda 2-1.
Mayele msimu uliopita alikutana na Simba kwenye michezo minne miwili ya ligi ambayo hakufunga hata mmoja, nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) hakufunga ila aliitungua Simba bao moja kwenye mchezo wa ufunguzi wa msimu Ngao ya Jamii pia.
CLATOUS CHAMA - SIMBA
Unaweza kuzungumza kuhusu Phiri kufunga mabao mengi ya Simba msimu huu, lakini Chama amekuwa akihusika na bao katika mechi zote tisa kati ya 10 ambazo Wekundu wa Msimbazi wamecheza msimu huu hadi sasa. Katika mechi hizo tisa kama hajafunga, basi ametoa asisti, na kama hajatoa asisti basi amempasia mtu aliyetoa asisti ya bao. Huyo ndiye Chama wa msimu huu, anatisha kama njaa. Amerudi kuwa yule ambaye kila mmoja anamfahamu ambaye alikuwa akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu.
Chama amekuwa katika kiwango bora msimu huu hadi sasa amefunga mabao mawili kwenye ligi na moja kwenye Ligi ya Mabingwa na ametoa jmla ya asisti 7 katika michuano yote, ikiwamo ile tamu ya kurusha juu ya ukuta aliyompa Pape Ousmane Sakho dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii.
FEISAL SALUM - YANGA
Tangu kuanza kwa ligi msimu huu amekuwa katika kiwango bora kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga, kuanzisha mashambulizi, kupiga pasi za mwisho na muda mwingine kufunga mwenyewe.
Fei amehusika katika mabao sita katika mechi 10 za michuano yote msimu huu akifunga mabao manne na kutoa asiti mbili.
Alifunga bao kwa kufumua roketi la mbali wakati yanga ilipoitoa Simba katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam msimu uliopita.
PAPE SAKHO - SIMBA
Alianza msimu huu vizuri kwa kufunga bao la kuongoza la mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ingawa dakika 90, zilimalizika kwa Simba kulala mabao 2-1.
Sakho kuna baadhi ya mechi mwanzoni mwa msimu huu amekuwa kwenye ubora kutokana na uwezo wake haswa anapokuwa na mpira mguuni na kama mabeki wa Yanga hawatakuwa makini kumzuia anaweza kuwapa shida.
AZIZ KI - YANGA
Alikuwa kwenye kiwango bora katika mechi yake ya kwanza ya Dabi ya Kariakoo, aliwasumbua mabeki na viungo wa Simba kutokana na umahiri wake, akimpiga matobo Mohammed Hussein na alihusika kwenye bao la pili alilofunga Mayele katika mechi hiyo dhidi ya Simba na tangu hapo amekuwa na muendelezo mzuri.
Katika Ligi, Ki amefunga bao moja sawa na Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo amehusika katika mabao matatu, akifunga mawili, asisti moja.
AUGUSTINE OKRAH - SIMBA
Mabeki wa Yanga haswa wale ambao watapata nafasi ya kuanza pembeni kama si Djuma Shabani basi Kibwana Shomary watakuwa na kazi ngumu ya kumzuia Okrah kuhakikisha haonyeshi makali yake.
Winga huyu wa Ghana, ambaye huitwa katika timu ya taifa hilo iliyojaa nyota wanaocheza Ulaya, ana kasi na uwezo wa kupiga chenga amefunga bao moja na kutoa asisti mbili katika michuano yote msimu huu ambao ndio wa kwanza tangu atue Simba.
Ni mkali wa kufunga kwa ‘frii-kiki’ ya moja kwa moja kama alivyowaliza Geita Gold waliyoichapa 3-0 katika Ligi Kuu na alivyofunga katika mechi ya kirafiki Zanzibar.
TUISILA KISINDA - YANGA
Yanga imemrudisha Tuisila kikosini katika dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa akitokea RS Berkane ya Morocco na benchi la ufundi limemuhitaji kwa hamu kutokana na michezo mikubwa.
Benchi la ufundi Yanga linahitaji kumuona Tuisila anaonyesha kiwango kikubwa kwenye michezo mikubwa kama huo dhidi ya Simba na hilo linawezekana kwake kwani alishawahi kufanya hivyo kabla ya kuondoka nchini.
HENOCK INONGA - SIMBA
Kumekuwa na maelewano mazuri kwenye mechi dhidi ya Yanga haswa anapocheza na beki mwenzake, Joash Onyango na muda mwingi wanawapa wakati mgumu washambuliaji wa timu pinzani kufunga mabao.
Mechi mbili za ligi msimu uliopita mabeki hao walicheza kwa pamoja walihakikisha Mayele anashindwa kufunga bao ila mechi ya Ngao ya Jamii msimu uliopita ambayo Mayele alifunga, Inonga hakuwepo.
Mayele alifunga mabao mawili msimu huu kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Onyango hakuwepo nafasi yake alicheza Mohammed Ouattara ambaye hakucheza kwa kiwango bora.
YANNICK BANGALA - YANGA
Mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Bangala ni maarufu kama ‘Mzee wa Kazi Chafu’. Wapinzani wamekuwa wakikutana na wakati mgumu akisimama katika eneo la kiungo ama beki wa kati.
Bangala katika michezo yote ya Simba aliyocheza ameifanya timu yake eneo la kiungo kuwa imara huku akiwapa kazi wale wa Simba, Jonas Mkude, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin na wengine kuwa na wakati mgumu.