Wanatetemeka

Muktasari:
Msafara wa wachezaji 23 wa mabingwa hao wa kihistoria walitua jijini wakiongozwa na kocha huyo Mdachi aliye kiri kuifanyia ushushushu Yanga ili kujua mbinu zao, lakini alikiri kwa Hans Pluijm ana kazi. Yanga haijapoteza mechi zake za nyumbani msimu huu iwe katika ligi au michuano ya Kimataifa.
WAMISRI, Al Ahly wametua nchini alfajiri ya jana Jumatano na kujichimbia Hoteli ya Kempski, wakihodhi vyumba vyote, lakini kocha wao Martin Jol amejibu maswali matatu akidai anahofia rekodi ya Yanga ikiwa nyumbani.
Msafara wa wachezaji 23 wa mabingwa hao wa kihistoria walitua jijini wakiongozwa na kocha huyo Mdachi aliye kiri kuifanyia ushushushu Yanga ili kujua mbinu zao, lakini alikiri kwa Hans Pluijm ana kazi. Yanga haijapoteza mechi zake za nyumbani msimu huu iwe katika ligi au michuano ya Kimataifa.
Rekozi zinaonyesha Yanga na Al Ahly zimeshakutana kama mara nne katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1982, 1988, 2009 na 2014 na Jumamosi hii zitakutana tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Kocha Jol aliyewahi kutamba na klabu maarufu za Ulaya akisema kuwa Yanga ni wagumu.
Akizungumza baada ya kuwasili Jol kwanza ametamba kwamba mikanda ya video ya mechi za Yanga waliyoipata ikiwa ni pamoja na taarifa muhimu zimeongeza hali ya kuajiamini katika kikosi chao na wako tayari kwa kuwaondoa Yanga ambao tayari mbinu zao zipo katika makabrasha yake ya maandalizi.
Jol aliyezifundisha Tottenham Hotspur, Fulham za England, Hamburger SV ya Ujerumani na Ajax ya kwao Uholanzi, alisema licha ya kupata mikanda hiyo hawatarajii mchezo huo uwe rahisi kutokana na kikosi kinachofundishwa na rafiki yake Hans Pluijm kuwa na mazingira ya kutotabirika hasa kufuatia matokeo yao ya mwisho wakiwa hapa nchini ambapo walipokea kipigo cha bao 1-0 mwaka 2014.
Alisema anamjua vyema Pluijm, ni kocha mzuri ambaye uwepo wake ndani ya Yanga utaongeza ugumu kwao, japo wako tayari kukabiliana na ugumu huo ndiyo maana wakawahi kuja nchini kuzoea mazingira.
“Unaona tumewahi kuja Tanzania ni ishara kwamba tunataka kufanya mambo kwa umakini, itakuwa mechi ngumu lakini nafurahi tulifanya jitihada kupata mikanda yao na taarifa muhimu ambazo naamini zitatusaidia,” alisema Jol.
Waduwazwa
Al Ahly imeshtushwa na taarifa ya mabadiliko makubwa ya kikosi cha Yanga katika kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, lakini imebainika kuwa hata kikosi chao kimekuwa na mabadiliko makubwa na ni nyota wanane tu waliokuwapo mwaka juzi.
Al Ahly iliwasili jana Jumatano alfajiri na kikosi cha wachezaji 23 lakini kati yao ni wanane tu waliocheza mechi dhidi ya Yanga mwaka 2014 na kuweka ulinzi mkali kwenye kambi yao hoteli ya Kempski, wakizuia vyumba vyote ili wasihujumiwe.
Nyota wa Al Ahly waliocheza mchezo huo ambao ulishuhudia Ahly ikishinda kwa bao 1-0 na kisha kupata ushindi wa penalti 4-3 na sasa wapo kikosini ni kipa Sherif Ekramy, mabeki Ahmed Fathi, Saad Samir na Rami Rabia. Wengine ni viungo Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Walid Soliman, Abdalla El-Said na mshambuliaji Emad Meteb. Mfungaji wa bao pekee katika mechi hiyo ya marudiano, Abdul-Wahed Al-Sayed tayari ameondoka kikosini hapo.
Kwa upande wa Yanga nyota waliocheza mechi hiyo ya marudiano Misri ambao bado wapo na Yanga ni kipa Deo Munishi ‘Dida’, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Saimon Msuva.
Nyota wa Yanga waliokuwepo Yanga na wapo hadi sasa lakini hawakucheza mchezo huo ni Haruna Niyonzima, Juma Abdul na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Babi afichua siri
Nahodha wa zamani wa Yanga, Abdi Kassim ‘Babi’ alifichua siri kuwa vijana wa Pluijm wanaweza kuifunga Al Ahly, iwapo watashuka uwanjani wakijiamini na kuondoa dhana kwamba hawawezi mbele ya Waarabu.
Alisema ameiangalia Yanga na kubaini ina kikosi kizuri hivyo ni wajibu kwa wachezaji kushuka uwanjani wakiamini wanaweza kuisimamisha Ahly, ila wakiingia kwa woga wanaweza kuchezea nyingi.
Kiungo huyo alisema Yanga itambue inacheza na timu iliyoandaliwa vema, hivyo iwe makini muda wote wa dakika 90.
“Tahadhari hii si kwa Yanga tu, hata Azam watakaocheza na Esperance. Timu zetu ziepuke rafu za kijinga na kutowapa nafasi wapinzani wao kuwatawala.”
Imeandikwa na Khatimu Naheka, Doris Maliyaga, Gift Macha na Olipa Assa.