Wanatamba: Ni zamu ya watoto wa Ivory Coast Ulaya

Muktasari:
- Lakini, sasa kuna kila dalili kwamba mzao wa watoto wenye asili ya Ivory Coast ndio umeanza kuiteka zaidi Ulaya.
LONDON, ENGLAND
WATOTO wa wazazi wa Kinigeria ndio ambao wametamba katika soka la Ulaya kwa muda mrefu baada ya kuzaliwa na kukulia barani Ulaya, au kuhamia barani humo wangali watoto.
Lakini, sasa kuna kila dalili kwamba mzao wa watoto wenye asili ya Ivory Coast ndio umeanza kuiteka zaidi Ulaya.
Serge Gnabry
Kinda ambaye ameanza kuwateka mashabiki wa soka wa Uingereza akiwa katika klabu yake ya Arsenal. Gnabry ni Mjerumani na anapigiwa chapuo na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low kukipiga katika fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Hata hivyo, baba yake Gnabry, Jean Hermann anatoka Ivory Coast. Jean aliondoka nchini kwao Ivory Coast kwenda Ujerumani kwa ajili ya kujifunza Lugha ya Kijerumani ili arudi nyumbani na kufundisha lugha hiyo.
Lakini, alipofika Ujerumani aliangukia katika penzi la mwanamke wa Kijerumani na hatimaye kumuoa. Baadaye aliamua kubaki Ujerumani na kumzaa Serge.
Wilfried Zaha
Tayari ameichezea timu ya taifa ya England katika ngazi zote. Na kama si benchi la kocha David Moyes kwenye klabu ya Manchester United, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotarajiwa kuiwakilisha England katika fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, Zaha ni mzaliwa wa Ivory Coast. Alizaliwa Abidjan na kuhamia England na wazazi wake angali akiwa na umri wa miaka minne tu.
Familia yake ilihamia eneo la Thornton Heath, Croydon, London na baadaye alikwenda Shule ya Whitehorse Manor Junior School, Thornton Heath na kisha kujiunga Selsdon High School, Selsdon.
Yohann Djourou
Staa wa zamani wa Arsenal ambaye sasa hivi ametulia katika soka la Hamburger SV ya Ujerumani. Djourou alizaliwa jijini Abidjan nchini Ivory Coast na wazazi wake wakiwa ni Joachim na Angeline.
Lakini baadaye akaasiliwa na mke wa kwanza wa baba yake, Daniele ambaye alikuwa ni mama wa Kiswisi. Walienda Geneva wakati Djourou akiwa na umri wa miezi 17 tu.
Soka la utotoni alilianzia katika kituo cha Payerne akiwa na miaka 13 kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Daraja la Pili ya Etoile Carouge akiwa na umri wa miaka 15.
Miezi michache baadaye alipata nafasi ya kujiunga na timu ya vijana ya Arsenal na alisaini mkataba wa kulipwa Agosti Mosi, 2003. Kwa sasa ni miongoni mwa walinzi wa timu ya taifa ya Uswisi.
Yaya Sanogo
Kinda nyota mwenye urefu wa futi 6 na inchi 3 ambaye mashabiki wa Arsenal bado hawajamfaidi uwanjani kutokana na kukabiliwa na majeruhi tangu alipotua klabuni hapo akitokea Auxerre ya Ufaransa.
Sanogo alizaliwa katika vitongoji vya watu wengi jijini Paris nchini Ufaransa mwaka 1993, lakini baba yake anatoka Ivory Coast wakati mama yake anatoka nchini Mali.
Timu yake ya kwanza kuchezea ni Pantin ya Paris, lakini pia akachezea timu nyingine ya uswahilini, Motrouge CF 92 timu ambayo pia nyota wa Ufaransa na Newcastle United, Hatem Ben Arfa alianzia maisha. Baadaye akachezea klabu ya Les Ullis ambayo inasifika kwa kumkuza Thierry Henry.
Akiwa na umri wa miaka 13 alijiunga katika Shule ya Soka ya Auxerre ambayo kwa sasa inasifiwa zaidi kwa kukuza vipaji vya mastaa wa sasa nchini Ufaransa.
Sanogo angeweza kuzichezea timu za taifa za Ivory Coast, Mali au Ufaransa, lakini mpaka sasa ni staa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa chini ya umri wa miaka 21.
Yannick Sagbo
Nyota wa klabu ya Hull City ya England ambaye jina lake kamili ni Yannick Anister Sagbo-Latte. Wazazi wake wanatoka Ivory Coast, lakini alizaliwa Aprili 12, 1988 katika jiji la Marseillle ambako wazazi wake walikwenda kutafuta maisha. Alianza kucheza soka katika klabu ya mtaani kwao ya SC Air Bel kabla ya kujiunga na Monaco katika kipindi cha majira ya joto mwaka 2004.
Tofauti na mastaa wengine walioamua kuchagua nchi za Ulaya kama vile Serge Gnabry, Wilfried Zaha, Yaya Sanogo na wengineo, Sagbo ameamua kuichezea timu ya wazazi wake Ivory Coast.
Rekodi zinaonyesha amecheza mechi mbili tu huku mechi ya kwanza ikiwa ya kirafiki dhidi ya Italia katika Uwanja wa Upton Park unaomilikiwa na West Ham United mnamo Agosti 10, 2010. Aliingia uwanjani dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Seydou Doumbia huku Ivory Coast ikishinda 1–0.
Abou Diaby
Kiungo ambaye majeraha ya muda mrefu yameathiri kiwango chake kwa kiasi kikubwa na hata sasa yuko nje kwa majeraha. Wazazi wa Diaby wanatoka Ivory Coast ingawa yeye mwenyewe alizaliwa na kukulia Paris katika maeneo ya mipango maalumu ya nyumba za kisasa Aubervilliers, kaskazini mashariki mwa Paris.
Baba yake alikuwa dereva wa mbio ndefu na Diaby aliamua kujikita katika soka zaidi baada ya kushuhudia Ufaransa ikitwaa Kombe la Dunia nyumbani kwao mwaka 1998. Shujaa wake ni kiungo wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira.
Katika kipindi cha majira ya joto mwaka 2012, Diaby na kiungo mahiri wa Ivory Coast, Yaya Toure walipanda ndege moja kwenda Ivory Coast kusalimia familia zao baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu England.
Hata hivyo, Diaby alichagua kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa katika anga za soka la kimataifa na alikuwepo katika kikosi cha Ufaransa kilichoshiriki na kuchemsha katika fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.