Wanasubiri Januari ifike

Muktasari:

  • Manchester City wanafikiria kumchukua Sanchez, wakati Ozil mara kadhaa ametajwa kuwapo kwenye rada za Jose Mourinho

LONDON, ENGLAND

ASIKWAMBIE mtu dirisha la usajili wa Januari si tu kwamba, linafurahisha mashabiki kwa kuona sura mpya zinaongezeka kwenye timu zao wanazozishangilia, bali limekuwa likiwapa presha makocha wa timu hizo kwa sababu kuna mastaa wao watalazimika kuondoka na hivyo kuwatibulia kwenye mipango yao.

Makala haya yanahusu wachezaji wanaoweza kuzihama timu zao kwenye dirisha la Januari kwa klabu zote za Ligi Kuu England.

ARSENAL- ALEXIS SANCHEZ

Kocha Arsene Wenger ana mtihani mzito huko Arsenal kutokana na kukabiliwa na hatari ya kuwapoteza mastaa wake muhimu, Alexis Sanchez na Mesut Ozil. Mastaa hao kwa sasa wamegomea kusaini mikataba mipya na Kocha Wenger aliwahi kusema anaweza kufikiria kuwauza kwenye dirisha la Januari kama hawatakuwa wamesaini dili jipya kabla ya muda kufika.

Arsenal italazimika kuwauza kwenye dirisha lijalo la Januari ili kupata pesa kuliko kuendelea kukaa nao hadi mwisho wa msimu ambapo, watakuwa huru kwenda kujiunga na timu yoyote kwa uhamisho wa bure kabisa.

Manchester City wanafikiria kumchukua Sanchez, wakati Ozil mara kadhaa ametajwa kuwapo kwenye rada za Jose Mourinho huko Manchester United baada ya wawili hao kuwahi kuwa pamoja walipokuwa Real Madrid.

CHELSEA-MICHY BATSHUAYI

Chelsea wataingia Januari bila ya huduma ya mtu wao aliyekuwa makini kwenye kufanya usajili, Michael Emenalo, huku wakihusishwa kuwa na mpango wa kufanya usajili katika dirisha hilo.

Hata hivyo, Kocha Antonio Conte amepanga kupunguza idadi ya watu kwenye kikosi chake kabla ya kuongeza wengine huku wachezaji walio kwenye hatari ya kuondoka Stamford Bridge ni straika Michy Batshuayi.

Conte alitaka kumtoa kwa mkopo Batshuayi kwenye dirisha lililopita, lakini aliamua kumbakiza baada ya kukosa straika mwingine na hivyo alitaka abaki kumsaidia Alvaro Morata. Kama straika mwingine atapatikana dirisha lijalo la usajili, basi hapo hakutakuwa na kikwazo kwa Batshuayi kufunguliwa mlango wa kutokea.

LIVERPOOL-DANNY INGS

Majeruhi mawili makubwa yametibua mwenendo mzuri wa soka la staa wa Liverpool, Danny Ings na sasa anafikiria kuachana na timu hiyo.

Kwa misimu miwili sasa, kila Ings anaporejea kwenye ubora wake amekuwa akikumbana na changamoto ya kuumia tena na hivyo, kumfanya azidi kuwekwa benchi tu katika kikosi hicho cha Kocha Jurgen Klopp na sasa haonekani kama ataweza kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wake huko Anfield.

Inaripotiwa staa huyo ataondoka Liverpool dirisha lijalo la Januari, akitajwa kutimka kwa mkopo huku West Ham United na Newcastle United zikitajwa kumfukuzia.

MAN CITY-YAYA TOURE

Licha ya msimu uliopita alipandisha kiwango chake na kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Pep Guardiola, mambo yamegeuka na Yaya Toure sasa anaonekana hana kitu anachoweza kukifanya pale Etihad.

Guardiola anaonekana tayari ameshatengeneza timu anayotaka kutokana na kucheza kwa ubora mkubwa kabisa na msimu huu hawakamatiki kwa kushinda mechi zake na kuongoza Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya mahasimu wao, Manchester United.

Kutokana na hilo, Yaya sasa amekuwa mchezaji wa ziada tu huko Man City na huenda akafunguliwa mpango wa kutoka akipelekwa ya New York City FC ya Marekani.

MAN UNITED-LUKE SHAW

Waingereza wengi walikuwa wakipiga sala kuona beki wao Luke Shaw anafikia mafanikio huko Old Trafford, lakini sala zao zinaonekana kugomba mwamba kwani mambo yamekwenda tofauti na matarajio yao.

Tangu beki huyo alipovunjika mguu Septemba 2015 ameshindwa kurejea katika ubora wake wa kumfanya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Akiwa na umri wa miaka 22, Shaw bado ana miaka mingi sana ya kucheza soka na ripoti zinadaiwa kwamba, Manchester United wapo tayari kumpiga bei kwenye dirisha la Januari kwa Pauni 20 milioni tu. Danny Rose anatajwa kuja kuziba pengo lake.

TIMU NYINGINE

Wakati dirisha hilo la usajili wa Januari likiwa mbioni kufunguliwa mastaa kibao wanahusishwa na mpango wa kuachana na timu zao na West Ham United, anatajwa Diafra Sakho anaweza kuondoka, wakati Nacer Chadli amedaiwa na mpango wa kuachana na West Brom na Watford wakiripotiwa kuwa kwenye hatari ya kumpoteza Stefano Okaka.

Tottenham Hotspur inaripotiwa kuwa inaweza kumpoteza kinda wao Kyle Walker-Peters na Swansea City ni Ki Sung-yeung huku Stoke City wakiwa kwenye hatari ya kuondokewa na Giannelli Imbula.

Beki Mdachi, Virgil van Dijk anaripotiwa kwamba anaweza kuachana na Southampton na Aleksandar Mitrovic yupo kwenye hatihati ya kuondoka huko Newcastle United.

Ahmed Musa, anatajwa kupiga hesabu za kuondoka huko Leicester City, wakati Huddersfield inatajwa kuwa kwenye mashaka makubwa ya kumpoteza Scott Malone na Everton ni Ross Barkley.

Crystal Palace anayetajwa ni Christian Benteke na Burnley ni Steven Defour wakati huko Brighton anayetajwa kuondoka ni Lewis Dunk na Bournemouth ni Harry Arter.