Wamefunga kote, wameshindwa Anfield pekee

Muktasari:

Hii hapa orodha ya masupastaa watano wa nguvu kwenye soka, ambao wameshindwa kabisa kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield licha ya kwenda kucheza kwenye uwanja huo zaidi ya mara moja.

LIVERPOOL, ENGLAND . WANASEMA hata uwe mbabe vipi, kuna sehemu utakwama tu.

Usibishe. We nenda kamuulize straika moto kabisa wa Manchester City, Sergio Aguero.

Straika Aguero hajawahi kuziangusha timu zake kwenye kufunga mabao, ametamba kwenye viwanja kibao kwa kufunga mabao makali tena dhidi ya timu ngumu, lakini mahali anapokwama ni Anfield.

Jumapili iliyopita Aguero aliambatana na kikosi cha Man City kwenda kukipiga na Liverpool uwanjani hapo Anfield kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, lakini rekodi yake mbovu ya kutofunga bao kwenye uwanja huo iliendelea.

Man City ilichapwa 3-1 na Aguero ameondoka akiwa na machungu mengi; moja timu yake kuchapwa, lakini pili kushindwa kufunga bao akiendeleza rekodi ya kushindwa kutamba anapocheza uwanjani hapo. Ubabe wake wote Aguero, lakini akifika Anfield anakwama, hana maajabu.

Asikuambie mtu, Anfield si mahali pa mchezomchezo, wakati Liverpool wakicheza mechi kibao bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England, kuna wachezaji mastaa wa maana wameshindwa kufunga kwenye uwanja huo mara kadhaa walipokutana na wakali wa hapo, Liverpool.

Hii hapa orodha ya masupastaa watano wa nguvu kwenye soka, ambao wameshindwa kabisa kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield licha ya kwenda kucheza kwenye uwanja huo zaidi ya mara moja.

Lionel Messi (Mechi 2)

Lionel Messi ameendelea kuvunja rekodi baada ya rekodi kila msimu anaokuwa uwanjani kukipiga kwenye kikosi chake cha Barcelona. Kuhusu kufunga mabao, hilo jambo halijawahi kuwa gumu kwa supastaa huyo wa kimataifa wa Argentina, ambapo kwenye mechi 37 alizokutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni sita tu ambazo Messi hakutikisa nyavu zao na Liverpool ni mojawapo.

Messi amemenyana na Liverpool mara mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Anfield, kwanza ile hatua ya 16 bora mwaka 2006/07 na ya pili msimu uliopita tu kwenye nusu fainali, lakini ameshindwa kufunga bao Anfield. Ubora wake wote wa kufunga Anfield licha ya kucheza uwanjani hapo kwa dakika 180.

Ole Gunnar Solskjaer (Mechi 5)

Kocha wa sasa wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amecheza mechi 235 za Ligi Kuu England akiwa na kikosi hicho cha Old Trafford, lakini ‘muuaji huyo mwenye sura ya kitoto’, iwe kwenye Ligi Kuu England au michuano mingine yoyote alishindwa kuifunga Liverpool kwenye mechi zilizopigwa Anfield.

Kwenye uwanja huo wa Anfield, Solskjaer amecheza mechi tano, lakini hakuna hata moja aliyochungulia nyavu za Liverpool licha ya uhodari wake wote katika kutikisa nyavu.

Ole kwa sasa ni kocha wa Man United na ndio timu pekee iliyotoka sare na Liverpool msimu huu, licha ya kikosi chake kuwa na changamoto nyingi kikishika nafasi ya saba kwenye msimamo wakikusanya pointi 16 katika mechi 12.

Eric Cantona (Mechi 6)

Mfalme, Eric Cantona ameshindwa kufunga bao kwenye uwanja wa Anfield kwa kipindi chake chote alichokuwa Leeds United na baadaye Manchester United. Mwaka mmoja kabla ya Man United kumnasa Canton, Liverpool walikuwa na nafasi ya kunasa saini yake, lakini wakali hao wa Anfield hawakutaka kumnasa wakisema kwamba ni mchezaji mwenye matatizo mengi.

Licha ya kwamba Cantona hakufunga bao Anfield, lakini aliwapa maumivu mashabiki wa timu hiyo ya Merseyside kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 86 katika fainali ya Kombe la FA 1996. Cantona amekwenda Anfield kucheza mechi mara sita, zote hizo hakuna hata moja aliyofunga bao.

Dennis Bergkamp (Mechi 6)

Fundi wa mpira, Mdachi Dennis Bergkamp alikuwa moto kipindi hicho alipokuwa akikipiga kwenye kikosi cha Arsenal. Lakini, kwa ubora wake wote wa uwanjani na kupiga mabao makali, lakini alishindwa kufanya hivyo uwanjani Anfield.

Mara sita alizokwenda kucheza kwenye uwanja huo, Bergkamp ameshindwa kufunga kwenye michuano yote iliyompeleka kucheza na Liverpool.

Baada ya ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA, Bergkamp alisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia Arsenal.

Sergio Aguero (Mechi 11)

Anfield si mahali pepesi, lakini kwa miaka ya karibuni kutokana na kuongezeka kwa ushindani, Manchester City kwenye mechi zake ilizokwenda uwanjani hapo, zimekuwa za ushindani mkali na kuwafanya wachezaji kushindwa kabisa kutuliza akili zao za uwanjani kuwaza mchezo zaidi ya kurushiana tu maneno.

Jumapili iliyopita, Man City walikwenda kucheza uwanjani hapo nan kukutana na kipigo cha mabao 3-1, lakini kubwa ni kwa straika wao namba moja, Aguero kushindwa kufunga bao kwa mechi 11 za michuano tofauti alizokwenda kucheza kwenye uwanja huo wa kibabe.