Mechi tisa za Mgunda kutembeza boli hizi hapa

Muktasari:

  • Matokeo ya mechi hizo ndiyo yaliyobeba hatma ya Simba msimu ujao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwani ili washiriki lazima wabaki katika nafasi mbili za juu ambazo Azam na Coastal Union wanaziwinda kwa kasi kubwa.

JUMA Mgunda na Seleman Matola wanaanza kibarua chao ndani ya Simba Jioni hii. Lakini ana mechi tisa mkononi ambazo atalazimika kutembeza boli kwa namna yoyote ile kutetea hadhi ya Simba kwenye Ligi Kuu Bara.

Matokeo ya mechi hizo ndiyo yaliyobeba hatma ya Simba msimu ujao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwani ili washiriki lazima wabaki katika nafasi mbili za juu ambazo Azam na Coastal Union wanaziwinda kwa kasi kubwa.

“Nimeshakutana na benchi la ufundi tumeshazungumza nimeelewa changamoto ambazo zipo natakiwa kupambana nazo, naamini tutafanya vizuri kwenye michezo yote iliyobaki, tuombe Mungu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars.

Safari yake ya mechi tisa inaanzia ugenini leo Jumanne jioni dhidi ya Namungo ambayo mzunguko wa kwanza matokeo yalikuwa 1-1. Mei 3, 2024, Simba itaikaribisha Mtibwa Sugar, mzunguko wa kwanza ugenini Simba ilishinda 4-2, huku rekodi yao ya nyumbani dhidi ya Mtibwa, ikiwa ni nzuri kutokana na kushinda zote, matokeo yakiwa hivi;5-0, 2-0 na 5-0.

Mtibwa Sugar hivi karibuni katika mechi zake za ugenini imeshinda moja, sare mbili, imepoteza kwa JKT Tanzania.
Wenyeji hao wa Turiani mkoani Morogoro, kumbuka pia wana kibarua dhidi ya Yanga na Azam, hivyo
katika kujinasua na janga la kushuka daraja, wanakutana na vigogo wote.

Mei 6, 2024, Simba itakuwa nyumbani mbele ya kibonde wake wa mzunguko wa kwanza, Tabora United
ambayo iliichapa mabao 4-0.

Tabora United rekodi yao ya mechi tatu za ugenini ilizocheza hivi karibuni, haijashinda hata moja,
imepoteza zote. Kumbuka Tabora iliyopo katika hatari ya kushuka daraja, inacheza dhidi ya Yanga na Simba katika mechi zao sita zilizobaki.

Mei 9, 2024 inaweza kuwa mechi ya kuamua kati ya Azam na Simba, hiyo ni kutokana na namna timu
hizo zilivyo kwenye msimamo. Mechi ya kwanza Simba ikiwa mwenyeji, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-
1.

Mechi zao sita za mwisho walizokutana, sare ni nne, huku kila mmoja akishinda mechi moja.
Mei 12, 2024, Simba itaenda Kaitaba kucheza dhidi ya Kagera Sugar baada ya mzunguko wa kwanza
nyumbani Simba kushinda 3-0.

Simba katika mechi tatu za mwisho ilipoenda ugenini kucheza na Kagera Sugar, imeshinda moja, sare
moja na kupoteza moja. Wakati rekodi ya Kagera Sugar ikiwa nyumbani hivi karibuni katika mechi tatu
haijashinda wala kupoteza, imetoka sare zote.
Dodoma Jiji wana kazi mbele ya Simba katika mchezo utakaopigwa Mei 16, 2024 pale Jamhuri, Dodoma
ambapo Simba mechi tatu za mwisho ikicheza ugenini dhidi ya mwenyeji wake huyo, imeshinda zote.

Ukiangalia rekodi ya Dodoma Jiji ilipocheza nyumbani katika mechi tatu za hivi karibuni, imeshinda moja,
sare moja na kupoteza moja.
Mei 21, 2024, itakuwa ni zamu ya Simba kuikaribisha Geita Gold baada ya mchezo wa mzunguko wa
kwanza ugenini Simba kushinda 1-0, huku rekodi ya Simba nyumbani mbele ya Geita Gold ikiwa nzuri
kutokana na kushinda mara mbili walizokutana.

Geita Gold mechi zao za ugenini hivi karibuni, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja, bado
inajitafuta ikiwa katika timu nafasi tano za chini.
Mei 25, 2024 Simba itaikaribisha KMC, mzunguko wa kwanza matokeo yalikuwa sare ya 2-2, huku mechi
zao tatu za mwisho kukutana, Simba ikishinda mbili na sare moja.

Rekodi ya KMC katika mechi tatu za mwisho ugenini, imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja. KMC
kwa sasa nayo inapambana kumaliza nne bora.
Mwisho kabisa Mei 28, 2024, Simba itacheza nyumbani dhidi ya JKT Tanzania, mechi ya kwanza Simba
ilishinda 1-0. Rekodi walipokutana mechi tatu za mwisho Simba imeshinda mbili na kupoteza moja.

JKT Tanzania rekodi yao ya kucheza ugenini mechi tatu za mwisho imepoteza moja na kuambulia sare
mbili, haijashinda. Kwa sasa timu hiyo inapambana isishuke daraja baada ya kupanda msimu huu.

Katika mechi zao nane zilizobaki, Simba itacheza sita jijini Dar es Salaam, mbili zikiwa nje ya mkoa huo.
Zote hizo zitakuwa ndani ya siku 29 kukiwa na wastani wa kucheza mechi moja kila baada ya siku tatu.