WALETE! Vikosi vya ushindi Simba, Yanga CAF hivi hapa!

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Lakini Benchikha anapata ahueni ya urejeo wa Sadio Kanoute ambaye alikosa mechi iliyopita dhidi ya Jwaneng Galaxy kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kuwa na kadi tatu za njano.

WACHEZAJI 20 kwa kila upande, wanashikilia kwa kiasi kikubwa hatma za Simba na Yanga katika mechi za kwanza za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Ijumaa na Jumamosi dhidi ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns.

Nyota hao 20 ndio kwa kiasi kikubwa watakuwa na jukumu la kubeba mipango na mbinu za ushindi za makocha Abdelhak Benchikha wa Simba na Miguel Gamondi wa Yanga katika mechi hizo muhimu ambazo timu zao zinapaswa kuibuka na ushindi ili zijiweke katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Kati ya hao ishirini, 11 ndio wataanza kikosini, huku tisa wakibakia kama silaha za ziada kwa timu hizo na makocha hao katika mechi hizi ambazo zote zitachezwa kuanzia saa 3:00 usiku zikiwa zimeshikilia hatma ya vigogo hivyo katika kuandika rekodi ya kucheza nusu fainali kwa mara ya kwanza pamoja.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

SIMBA

Dhidi ya Al Ahly, Ijumaa eneo ambao linaweza kumpasua kichwa kocha Benchikha ni lile la mshambuliaji wa kati ambalo Pa Omar Jobe na Freddy Michael wameonekana kuwa na kiwango kisichoridhisha ndani ya timu hiyo tangu waliposajiliwa katika dirisha dogo.

Urejeo wa Willy Onana unampa fursa nzuri Benchikha katika upande wa machaguo kwa upande wa ushambuliaji kutokana na uwezo wa nyota huyo wa Cameroon kucheza kama mshambuliaji wa kati na pia kushambulia kutokea pembeni akiwa na mabao mawili tayari katika michuano hii ya CAF hadi sasa.

Lakini Benchikha anapata ahueni ya urejeo wa Sadio Kanoute ambaye alikosa mechi iliyopita dhidi ya Jwaneng Galaxy kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kuwa na kadi tatu za njano.

Kanoute anaweza kutengeneza balansi nzuri ya kuzuia na kushambulia hivyo uwepo wake sambamba na viungo wengine wawili wa ukabaji, Fabrice Ngoma na Babacar Sarr unaweza kuifanya Simba ikawa na uimara mkubwa katikati mwa uwanja. Kanoute ndiye aliyeitungua Al Ahly nje ndani katika mechi za African Football League zilizoisha kwa sare nyumbani na ugenini. Kwa Mkapa iliisha kwa sare ya 2-2 na ugenini ikawa 1-1.

Mbali na Kanoute, pia mechi hii inaweza kuwapa fursa nzuri Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza kushambulia kutokea pembeni na mmojawapo kati ya Kibu Denis au Willy Onana kuanza kama mshambuliaji wa kati. Saido amehusika kwenye mabao manne ya Simba katika mechi hizo za CAF, akifunga mawili na kuasisti mara mbili, wakati Chama amefunga bao moja na kuasisti mara moja, lakini anaijulia sana Al Ahly aliyoanza kukutana nayo tangu mwaka 2016.

Kwa jinsi upepo ulivyo kama Simba itaamua kuanza na kikosi hiki huenda ikatoboa kiulaini ikianzia nyumbani na hata kumalizia ugenini;

Kikosi chenyewe:

Simba inaweza kuanza na Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Enock Inonga, Che Malone Fondoh, Babacar Sarr, Saido Ntibazonkiza, Fabrice Ngoma, Willy Onana, Sadio Kanoute na Clatous Chama.

Kwenye benchi, wachezaji tisa ambao wanaweza kuwa mpango mbadala wa Benchikha ni Ally Salim kwa nafasi ya kipa, mabeki ni Hussein Kazi, Israel Mwenda na Kennedy Juma, viungo ni Mzamiru Yassin na wachezaji wa mbele ni Ladack Chasambi, Jobe, Michael, Luis Miquissone na Kibu Denis.

YANGA

Katika mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Jumamosi Yanga huenda isiwe na mabadiliko makubwa katika kikosi chake cha kwanza kutokana na ubora mkubwa wa wale ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

Kurejea kwa Khalid Aucho kunaihakikishia Yanga usalama katika eneo la kiungo cha ulinzi ambalo amekuwa akicheza sambamba na Mudathir Yahya ambaye hata hivyo huwa na uhuru mkubwa wa kusogea juu kusaidia mashambulizi.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Uhitaji wa kuwa na mshambuliaji ambaye anaweza kucheza mgongoni mwa mabeki wa kati wa timu pinzani ili awe silaha ya kunufaika na udhaifu wa mabeki wa kati wa Mamelodi ambao huwa wana udhaifu wa kutonyumbulika kwa haraka, unamlazimisha Gamondi kumuanzisha ama Kennedy Musonda au Clement Mzize katika nafasi ya mshambuliaji wa kati na sio Joseph Guede.

Kasi na ujanja wa Augustine Okrah unaonekana unaweza kuwa msaada mkubwa kwa Yanga katika kuwadhibiti mabeki wa pembeni wa Mamelodi ili kutoa nafasi kwa beki wa pembeni wa Yanga kusogea juu na kupiga krosi kama ilivyo kwa upande wa Stephane Aziz Ki.

Huenda kusiwe na mabadiliko makubwa katika eneo la ulinzi ambapo Djigui Diara, Yao Attohoula, Nickson Kibabage, Dickson Job na Ibrahm Bacca wanaweza kuanza.

Kikosi chenyewe:

Yanga inaweza kuanza na Diara, Yao Attohoula, Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Augustine Okrah, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Silaha tisa za ziada za Gamondi katika benchi zinaonekana zitakuwa ni Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Gift Fred, Zawadi Mauya, Farid Musa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Clement Mzize, Joseph Guede na Bakari Mwamnyeto.

WASIKIE WADAU

Winga wa zamani wa Simba, Uhuru Selemani anasema kuwa ushindi wa Simba na Yanga nyumbani utachangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji.

“Kama wachezaji wasipocheza kwa kujitolea na kufuata vyema kile wanachoelekezwa, makocha watakuwa wanafanya kazi bure hata kama ni wazuri. Wachezaji wa Simba na Yanga wanapaswa kufahamu kwamba hii ni nafasi nzuri kwao kujiweka katika ramani ya soka Afrika kwa kuzitoa Mamelodi na Al Ahly,” anasema Uhuru.

Beki wa zamani wa Yanga, Kenneth Mkapa anasema Yanga na Simba zina wachezaji wazuri wa kuamua mechi.

“Hakuna kinachoshindikana kama wachezaji watajituma. Hizo timu mbili wanazocheza nazo zinafungika, lakini ni lazima wachezaji wetu wajitume kwa dakika zote 180 ambazo watakabiliana nazo,” anasema Mkapa.

Mechi zilivyo;

Ijumaa, Machi 29, 2024

Simba v Al Ahly

Saa 3:00 usiku

Kwa Mkapa


Marudiano

Aprili 05, 2024

Al Ahly v Simba

Saa 3:00 usiku

Cairo, Misri


Jumamosi, Machi 30, 2024

Yanga v Mamelodi

Saa 3:00 usiku

Kwa Mkapa


Marudio

Aprili 05, 2024

Mamelodi v Yanga

Saa 3:00 usiku

Pretoria, Sauzi