Tuzo ya ufungaji Bara ngoma droo

Muktasari:

  • Aziz Ki na Fei wanachuana kuwania tuzo hiyo ambayo msimu uliopita ilibebwa kwa pamoja na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saido Ntibazonkiza wa Simba ambao kila mmoja alimaliza na mabao 17.

MBIO za kuwania tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu ngoma nzito kikanuni, licha ya nyota wa Yanga, Stephane Aziz KI na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam wakichuana katika orodha ya wafungaji wa mabao hadi sasa.

Aziz Ki na Fei wanachuana kuwania tuzo hiyo ambayo msimu uliopita ilibebwa kwa pamoja na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saido Ntibazonkiza wa Simba ambao kila mmoja alimaliza na mabao 17.

Aziz KI ndiye anayeongoza orodha kwa sasa akiwa na mabao 15, huku akifuatiwa na Fei mwenye 14, lakini kikanuni wote hawachekani kwani wanalingana kila kitui licha ya kutofautiana kwa mabao ya kufunga, pia hata michezo iliyocheza timu zao zikitofautiana, Yanga ikicheza 23 na Azam 24.


AZIZ KI, FEI DROO

Wakati ikionekana Aziz Ki ndio kinara wa upachikaji wa mabao kutokana na idadi kubwa ya mabao aliyofungwa basi unaambiwa hana utofauti na Fei Toto kwa mujibu wa kikanuni.

Ipo hivi; Aziz KI mwenye mabao 15 aliyofunga mawili kati ya hayo amefunga kwa penalti kikanuni haitahesabika katika hesabu ya mwisho, hivyo hadi sasa inahesabika ana mabao 13.

Hivyo hivyo, kwa Fei Toto aliyepachika mabao 14 kikanuni pia ana mabao 13 kwani moja kati ya hayo alifunga kwa mkwaju wa penalti.

Azizi Ki alifunga mabao mawili ya penalti dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku Fei Toto mkwaju wake aliuchonga dhidi ya Tanzania Prisons.

Swali ni je, Aziz KI leo akiikabili Coastal Union atampiku Fei Toto kwa kumuongoza kwa kuzingatia kanuni hiyo ya mabao iliyotengenezwa msimu huu kutokana na utata uliojitokeza baina ya Mayele na Saido msimu uliopita wakati Yanga ikicheza mechi 24 ili kulingana na Azam?

Katika msimu huo TFF ililazimika kuigawa tuzo kwa wawili hao, japokuwa Saido mabao yake mengi yalikuwa ya penalti kulinganisha na Mayele, lakini hakukuwa na kanuni ya kumpendelea mmoja wao.


ASISTI

Nyota hao wawili wa Yanga na Azam wakiwa sawa kwenye kanuni ya mabao waliyofunga hadi sasa, lakini Aziz KI kamuacha Fei katika asisti za mabao kwani ametoa pasi za mabao saba, ikiwa ni mbili zaidi na alizo nazo mpinzani wake waliyecheza wote Yanga msimu uliopita.

Kinara wa utoaji pasi za mwisho zilizozaa mabao ni kiungo wa Azam FC, Kipre Junior ambaye ametoa pasi za mwisho nane amemuacha moja Aziz KI ambaye anashika nafasi ya pili sambamba na beki Kauassi Yao.


KANUNI ILIVYO

Kipengele katika kanuni mpya za Ligi Kuu Bara, kutafuta Mfungaji Bora ikitokea wachezaji wamelingana mabao inaainisha hivi;

Goli Lisilo la Penalti - Pointi Mbili (2)

Goli la Penalti - Pointi Moja (1)

Ikitokea wote wana mabao yanayolingana mwishoni mwa msimu, basi penalti zitahesabiwa na kutoa pointi kama unavyoona hapo juu mwenye mabao mengi ya penalti atakosa tuzo ya Mfungaji Bora.