Walahi Yanga msirudi!

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao lao la kuongoza dhidi ya Medeama ya Ghana katika mchezo wao wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Timu hizo leo Jumanne zinarudiana nchini Ghana. PICHA | SAID KHAMIS.
Muktasari:
- Yanga ikipoteza au kutoka sare kwenye mchezo huo ndiyo biashara imekwisha kwani watarudi kukamilisha ratiba tu. Sikia kwanza walichosema wachezaji.
KAMA Yanga inataka heshima Afrika kuendelea kusalia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho isirudi kwenye ardhi ya Dar es Salaam bila ushindi dhidi ya Medeama leo Jumanne.
Yaani kwa maneno mengine kabla jogoo hajaingia ndani baadae saa 1 jioni wanapaswa wawe wameshakinukisha, kwavile mechi inaanza saa 12 na tayari muda huo wakati jogoo linaambaa na ukuta watakuwa mapumziko. Yanga ikipoteza au kutoka sare kwenye mchezo huo ndiyo biashara imekwisha kwani watarudi kukamilisha ratiba tu. Sikia kwanza walichosema wachezaji.
NGOMA
Straika Donald Ngoma amesema; “Wakati mwingine ni kutokuwa na bahati, lakini nataka kufanya uamuzi wa umakini katika kila nafasi nitakayopata kwenye mchezo huu, timu nzima ipo katika hali nzuri ya ushindi. “Tunaposhindwa kufunga ndipo tunapoumiza timu na sitaki hilo litokee kwenye mechi hii, nitahakikisha hata kama sitafunga basi nitasababisha bao letu la ushindi.”
NIYONZIMA
Kiungo mshambuliaji, Haruna Niyonzima: “Tukiingia kinyonge tu tumekwisha, kila mmoja nadhani anatakiwa kufuta kumbukumbu mbaya ya vipigo viwili tulivyopata, kila uwanja unaweza kuutumia vizuri.
“Muhimu katika hili ni kuhakikisha kuwa akili zinatulia na kila atakayefanikiwa kuanza ajue kuwa anawakilisha jeshi kubwa la Yanga na timu inataka kusonga mbele licha ya kucheza ugenini.”
“Hapa sasa hatuangalii ukubwa wa mashindano, tunaangalia ukubwa wa mchezo kwanza, wakifanikiwa katika hilo hakuna tatizo,” aliongeza mchezaji huyo.
MSUVA
Winga Saimon Msuva amesema hakuna namna zaidi ya kufungua mapafu hadi mwisho katika mchezo wao wa leo. “Huku hakuna namna, ni kufunguka hadi mwisho, nikipata nafasi nadhani hata kocha atashangaa maana nataka kufanya kitu mara mbili zaidi ya nilivyozoeleka. Tunatakiwa kushinda kiukweli na kila mtu yupo makini na hilo, hili nadhani litasababishwa na kila mmoja wetu kama atajiongeza zaidi uwanjani, nadhani tunaweza kupata matokeo,” alisema Msuva.
CANNAVARO
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’; “Yanga imeshacheza mechi nyingi za ugenini na mazingira mara nyingi yanakuwa na changamoto kubwa, lakini bado hilo si tatizo kwetu.
“Tulishacheza katika mazingira magumu mno nchini Angola na tukafuzu kwa hatua hii, nadhani ni kujipanga na kuangalia tunataka nini kwa ajili ya kusonga mbele.”
“Ndiyo maana nikasema kuna kazi kubwa katika hili, tukishinda tutakuwa na nafasi nzuri ya kutuliza akili katika mechi mbili za mwisho kwani zina pointi sita na tunaweza kufikisha pointi 10 kwa kuanza na ushindi.”
KINACHOTAKIWA
Yanga inahitaji ushindi tu katika mchezo huo kama inataka kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu huku ikiombea Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe awachakaze MO Bejaia pale Jijini Lubumbashi.
Katika mechi hiyo ya Kundi A, Mazembe inaongoza kwa pointi saba, Bejaia katika nafasi ya pili kwa pointi tano wakati Medeama ikiwa ya tatu kwa pointi mbili, ikiizidi Yanga pointi moja. Mechi itapigwa kwenye Uwanja wa Sekondi na mwamuzi akiwa Mmorocco Redouane Jiyed.
MAZINGIRA
Hali ya hewa ya Mji wa Takoradi haitofautiani sana na baadhi ya maeneo ya Tanzania kwani mji huu upo pwani na kuna vipindi vingi vya mvua na baridi kiasi.
Lakini tangu Yanga iwasili hakukuwa na mvua licha ya wenyeji kudai kuwa kulikuwa na mvua kwa siku kadhaa nyuma kabla ya ujio wa mabingwa hao wa Tanzania.
Hali ya hewa imewaridhisha pia makocha wa Yanga, Hans Pluijm, Juma Mwambusi na Juma Pondamali wakidai kuwa haiwezi kuwachosha wala kuwapa tabu wachezaji wao.
Kocha wa Yanga, Pluijm alitamka baada ya mazoezi ya jana kwamba: “Lengo ni ushindi bila kuangalia tunacheza katika mazingira gani, tunajua kuwa tukishindwa hapa hali ni mbaya zaidi, lakini tunahitaji kupata matokeo hapa. Vijana wapo katika hali nzuri na tunaamini kuwa kila kitu kitakuwa sawa.”
KIKOSI
Mchezo huo utachezeshwa saa 9 alasiri kwa saa za Ghana (saa 12 jioni kwa Tanzania). Kwa mujibu wa mazoezi ya hapa kipa Deo Munishi ‘Dida’, atakayelindwa na Juma Abdul na Oscar Joshua wataanza.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ atacheza na Kelvin Yondani. Viungo watasimama Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Saimon Msuva wakati Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Donald Ngoma watakabidhiwa jukumu la kufunga.
Mshambuliaji Malimi Busungu ameonekana kuwa katika kiwango chake kwa kuongoza katika ufungaji kwenye mazoezi ya Yanga mjini hapa.