Wakali 11 wa kigeni

Jean Mugiraneza, Azam

Muktasari:

  • Hata hivyo, kuna baadhi ya nyota wa kigeni ambao wamekuwa wakilitendea haki soka la Tanzania kama ilivyowahi kufanywa na Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango, Kipre Tchetche na wengine ambao kwa sasa hawapo tena nchini.

KWA miaka ya karibuni Tanzania imegeuzwa kama chaka la wachezaji wa kigeni kuja kumalizia soka lao, huku wakisajiliwa kwa mbwembwe na kwa mamilioni ya fedha tofauti na viwango vya soka wanavyoonyesha uwanjani.

Baadhi yao ni kama wanawaibia Watanzania na klabu zao kutokana na ukweli kwamba hawana jipya katika kulisaidia soka la Tanzania kwa sababu viwango vyao huwa duni na mwishowe kuondolewa kwa aibu.

Hata hivyo, kuna baadhi ya nyota wa kigeni ambao wamekuwa wakilitendea haki soka la Tanzania kama ilivyowahi kufanywa na Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango, Kipre Tchetche na wengine ambao kwa sasa hawapo tena nchini.

Kwa sasa katika Ligi Kuu Bara inayoendelea wapo mastaa wengine wa kigeni ambao wameonyesha viwango vya hali ya juu na Mwanaspoti linakulea wakali 11 wa kigeni ambao wanafanya kazi ya ziada wanapokuwa uwanjani.  

1. Vincent Angban, Simba

Huyu ni kipa namba moja wa Simba ambaye tangu ajiunge na timu hiyo msimu uliopita akishindwa kuchukuliwa na Azam alipoenda kujaribiwa, amekosa mpinzani kwa makipa anaocheza nao Msimbazi.

Makocha wote wamekuwa wakimpa nafasi ya kucheza mechi zote za mashindano kutokana na umakini wake langoni na uzoefu unaombeba ndani ya kikosi cha Simba.

Angban ni miongoni mwa makipa wachache wa kigeni ambao wameonyesha uhai mkubwa kwenye soka la Tanzania mpaka sasa, kwani amewafunika baadhi ya wenzake  wakiwamo Youthe Rostand wa African Lyon na Owen Chaima wa Mbeya City.

Kwa umahiri wake langoni ni vigumu kumwondoa kwenye orodha ya wakali 11 wa kigeni wanaosumbua.

2. Janvier Bokungu, Simba

Pengine kukosekana kwa mabeki wenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya beki wa kulia ndani ya Simba kumemfanya Mkongomani huyu kuanza kuwakuna mashabiki wa klabu hiyo.

Mwanzoni watu walikuwa wakiamini hata mkataba wa miezi sita aliopewa ulikuwa wa bure kwa jinsi alivyokuwa akionekana mzigo uwanjani.

Hata hivyo, katika mechi chache alizopewa kucheza katika Ligi Kuu, Bokungu amethibitisha kuwa  utu uzima kweli ni dawa na anawanyoosha kwelikweli wachezaji wa timu pinzani zikicheza na Simba.

3. Mbuyu Twite

Kiraka huyu wa Yanga aliwahi kutajwa kama miongoni mwa watakaoachwa Jangwani, lakini   umuhimu wake wa kucheza zaidi ya nafasi moja, imekuwa ngumu kwa Kocha Hans Pluijm kumwacha.

Twite amekuwa msaada mkubwa ndani ya Yanga akitumiwa kufukia kila aina ya shimo linaloonekana kikosini na amekuwa akiwakuna wengi kwa soka lake la nguvu.

Licha ya kuwa umri unaomtupa mkono, kiraka huyo anaonekana bado wamo sana na anatupwa kwenye shavu la kushoto kwa vile kwake kambi ni popote pale.

4. Method Mwanjali, Simba

Wengi walimchukulia poa wakati akitua Simba, walimwita majina yote ikiwa ni pamoja na lile la kwamba ni mzee, lakini umahiri wake uwanjani umewafanya hata waliokuwa wakimtania wampigie makofi kwa sasa.

Mwanjali anayejinasibu kuwa ni Mnyakyusa na sio Mzimbabwe, alichukuliwa na Simba kama kiungo, lakini kumbe anamudu nafasi zaidi ya moja na kwa umri alionao anaitendea haki nafasi ya beki wa kati kiasi cha kutajwa kama mmoja wa mabeki visiki bora mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara.

5. Vincent Bossou, Yanga

Wakati alipotua Yanga wengi walimponda na kumwona kama ni wale wale wanaokuja nchini kuchuma fedha za bure, lakini baada ya kuanza kupewa nafasi kikosini waliomponda wamefunga midomo yao.

Beki huyo mzoefu wa kimataifa kutoka Togo amekuwa akifanya kazi kubwa ndani ya Yanga kiasi kwamba kila shabiki anamshangilia, anajua kutekeleza majukumu yake uwanjani na ni kiongozi mzuri kwa wenzake.

Kwa sasa ni mhimili mkuu wa Yanga akisaidiana na wazawa, Andrew Vincent na Kelvin Yondani.

6. Jean Mugiraneza, Azam

Kiungo huyu ‘ngongoti’ alikuja nchini katika klabu ya Azam kwa kazi moja tu ya kukaba tu. Lakini alikutana na changamoto ya namba kwa sababu katika nafasi hiyo kuna Kipre Balou na Himid Mao ambao nao walikuwa katika kiwango cha juu.

Mugiraneza hakusita kuonyesha kipaji chake mpaka kuwalazimisha makocha kuwachezesha viungo wakabaji wawili na yeye kuwa mmojawapo wa viungo hao katika mechi za Azam.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa Azam ndiyo timu yenye viungo wengi mafundi na wenye majina makubwa kama Sure Boy, Mudadhir Yahya, Frank Domayo mbali na Himid na Kipre Balou.

7. Hood Mayanja

Si mara ya kwanza kwa straika huyo kuichezea klabu hii kwa sababu alishakuja nchini kipindi timu hii ilivyopanda daraja lakini iliposhuka aliondoka na kwenda kwao Uganda lakini Lyon ilivyopanda tena amerejea na anafanya vizuri.

Mayanja ameonekana kuwa muhimili mkubwa katika timu hiyo kwani ndiye mchezaji pekee wa Lyon mwenye mabao mengi kwa timu hiyo na alianza kufungua akaunti ya mabao kwa kuifunga Azam bao la kona katika ufunguzi wa ligi kabla ya Shiza Kichuya kuja kulipa katika mechi ya watani.

8. Kamusoko, YANGA

Wenyewe wanapenda kumwita Rasta, aliposajiliwa kutoka FC Platinums wengi hawakumwamini sana mbele ya Haruna Niyonzima ama Mbuyu Twite ambao walikuwa katika viwango vizuri na kuelewana sana.

Kamusoko akabidi ajiongeze kwa kucheza nafasi zote za kiungo na ndipo akapata nafasi katika kikosi cha Yanga mpaka hivi sasa anaonyesha umahiri wa hali ya juu katika nafasi hiyo na kuaminika vilivyo kwa mashabiki na hata benchi la ufundi.

Kwa sasa Kamusoko ni gumzo kwelikweli kwa soka lake la kampa kampa tena, huku pia akiwa ni mahiri kwa kufumua mashuti makali kiufundi ambayo msimu uliopita ilimfanya afunge mabao matano katika Ligi Kuu Bara.

9. Amissi Tambwe, Yanga

Huyu jamaa ni hatari kwasababu popote yeye ni kambi.

Alipokuwa Simba alichukua Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora ametua Yanga kazi ni ile ile. Yaani yeye na kufunga mabao ni kama mgambo na kirungu.

Mrundi huyu ni mmoja kati ya wachezaji wenye akili ya kucheka na nyavu, kiasi kwamba katika misimu yake minne amefunga mabao 58 ikiwa ni rekodi kwani hakuna nyota wa kigeni aliyeweza kufikia rekodi hiyo mpaka sasa.

10. Donald Ngoma, Yanga

Kama Laudit Mavugo angekuwa vyema tungeweza kumweka katika nafasi hii, lakini rekodi na namna ya uwajibikaji uwanjani unampa ujiko Donald Ngoma kuingia katika orodha hii.

Mzimbabwe huyu alianza polepole sana na baadhi ya watu walihisi Yanga imeingia mkenge lakini amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga katika mechi za ndani na za kimataifa msimu uliopita ni mkali na anayetesa sana mabeki kwa uwezo wake wa kumiliki mpira na kufunga.

Ingawa kasi yake msimu huu imepungua kutokana na uchovu wa kucheza mechi za mfululizo kuanzia msimu uliopita, lakini huwezi kumweka kando Mzimbabwe huyu aliyesajiliwa toka FC Platinum ya Zimbabwe.

11. Thomas, Azam

Winga machachari kutoka Ivory Coast, kwa mwonekano wake unaweza ukasema ni sharobaro mmoja hivi kaja kuzurura mjini, lakini anapokuwa uwanjani mabeki huomba po kwa jinsi anavyosumbua.

Thomas katika mechi zake amekuwa na msaada mkubwa kwa Azam japo hajafunga mabao ya kutosha, ila ni wazi klabu hiyo imelamba dume kwa usajili wa mchezaji huyo.