Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa hili la TOC, Makonda ajishushe


Miaka ya 90 tulikuwa na matatizo makubwa kati ya uendeshaji wa mchezo wa mpira wa miguu na miongozo ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).


Matatizo mengi yalitokana na maamuzi ya wakati huo ya waziri aliyekuwa anahusika na michezo. Kulikuwa na hoja muhimu kabisa za kuonyesha uongozi wa wakati ule ulikuwa unakiuka misingi muhimu ya utaratibu wa utawala bora, lakini maamuzi mengi ya serikali yalionekana kutozingatia michakato ya kuwawajibisha viongozi waliokuwa wanaongoza soka wakati huo.

Kwa hiyo, waziri aliyekuwa anahusika na michezo wakati huo alipewa vifungu vya sheria za nchi vinavyompa mamlaka ya kufanya maamuzi makubwa bila ya kuzingatia taratibu ambazo vyama vilijiwekea ili kutatua matatizo yake.

Ndiyo maana waziri wa wakati huo aliyekuwa anahusika na michezo aliingia katika rekodi za viongozi wa serikali walioingilia masuala ya michezo mara nyingi bila ya kuibuka na ushindi. Mara zote, serikali ilibidi ikubaliane na misimamo ya Fifa kuwa shughuli za uendeshaji wa vyama au mashirikisho ya michezo hazina budi kuwa na uhuru kamili ili kuepuka masilahi mengine ya kisiasa, kijamii au kiuchumi kuathiri michezo.

Hadi leo, waziri aliyekuwa na mamlaka katika usimamizi wa michezo wa wakati huo, Juma Kapuya hajawahi kuwa na nyayo zinazotakiwa kuheshimiwa na wadau wa michezo nchini na amesahaulika kana kwamba hajawahi kushika wadhifa huo muhimu kwenye nchi ambayo mpira wa miguu ni kipenzi cha Watanzania zaidi ya asilimia 50.

Katika mazingira hayo ndiyo unasikia waziri mwingine anayehusika na michezo anaunda safu mpya ya uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), eti kwa sababu kumetokea matatizo katika mchakato wa uchaguzi! Matatizo ya mchakato wa uchaguzi ndiyo yasababishe uongozi mzima wa TOC uwekwe kando?

Kwani juhudi gani zilifanyika kujua matatizo yaliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi, vikwazo gani vilionekana na kwa nini haikuwezekana kuvitatua ili uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa?

Kwa nini tukimbilie kwenye mamlaka ya mwisho ya waziri katika kufanya maamuzi badala ya kujikita kwanza katika kutafuta suluhisho la kilichojitokeza kwa kukutanisha wadau wote na kukubaliana nini kifanyike badala ya kutumia nguvu za sheria ambazo zitaibua mgogoro mpya kati ya serikali na mashirikisho ya kimataifa ya michezo?

Nadhani uamuzi wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Makonda wa kuunda uongozi mpya wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) eti kwa sababu kumetokea matatizo katika mchakato wa uchaguzi, si sahihi kwa kuangalia katiba na miongozo ya kamati hiyo na uhusiano wake na mashirikisho ya kimataifa, hasa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Kwa mujibu wa kanuni zake, IOC haitaki kabisa kuwepo na vitendo vya serikali kuingilia uendeshaji wa kamati za olimpiki za nchi. IOC inataka kamati hizo za nchi kuwa huru ili kuepuka masilahi ya kisiasa kutamalaki katika shughuli za michezo.

Na moja ya shughuli zinazozuiwa na IOC ni uundwaji wa uongozi wa kamati za olimpiki za nchi. Kwamba iwe na mapinduzi au mabadiliko ya kawaida yanayotokana na uchaguzi, ni lazima maamuzi hayo yafanywe na mkutano mkuu na wanaoteuliwa kuunda uongozi wa muda ni lazima wawe wajumbe wa mkutano mkuu.

Lakini Waziri Paul Makonda ameunda uongozi wa muda ambao hautokani na mkutano mkuu wa TOC, jambo ambalo haliwezi kuwa na mashiko katika hoja za utawala bora. Kama kuna wagombea ambao hawaridhiki na mwenendo wa mchakato, haiwezekani kuunda uongozi wa muda ndio ukawa suluhisho la tatizo hilo.

Nadhani ilibidi wizara husika itafute jinsi ya kushughulikia tatizo hilo kwa kuliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kukutana na pande zinazosigana kujua tatizo liko wapi na kutafuta jinsi la kulisuluhisha.

Naamini hilo lingefanyika, suluhisho lingepatikana hata kabla ya kuamua kutumia mamlaka ya mwisho ya waziri ambayo kwa kawaida huibua migogoro isiyo ya lazima na mashirikisho ya kimataifa.

Pamoja na ukweli uchaguzi ni kitu muhimu sana katika uhai wa chama au shirikisho, bado suala hilo lineza kuwa dogo sana  kama busara itatumika kulishughulikia. Haiwezekani tuhuma za baadhi ya wagombea zikalazimisha uongozi mzima wa TOC ukaondolewa na kuundwa uongozi mwingine usiotokana na mfumo wa uongozi wa TOC.

Wengi waliochaguliwa hawatokani na viongozi wa vyama vya kitaifa vya michezo, hasa ukiangalia mwenyekiti wa kamati hiyo ya muda, Ismail Aden Rage, ambaye kwa sasa haongozi chama chochote cha michezo cha kitaifa. Iwapo hali hii itaendelea, maana yake waziri anaweza kujifanyia chochote kile bila ya kujali misingi na utamaduni wa uendeshaji michezo nchini.

Ni kwa jinsi hiyo, ninashauri Waziri Makonda ajisahihishe na kurekebisha maamuzi yake ili yaendane na misingi ya utawala bora katika uongozi wa michezo. Kama ni kutafuta tatizo la rushwa katika uchaguzi wa TOC, basi ni muhimu akaiagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) ishughulikie tatizo hilo na kutoa ripoti ili suluhisho lipatikane.

Kitendo cha waziri kuunda uingozi mpya wa TOC eti kwa sababu kuna tagtizo katika uchaguzi, hakiwezi kutuletea suluhisho sahihi la matatizo ya uongozi katika vyama vya michezo.

Waziri Makonda hana budi kuweka ufahari chini na kukubali kuangalia kwa makini tatizo la uchaguzi wa viongozi wa TOC kabla ya kukimbilia sheria inayompa mamlaka ya mwisho katika shughuli za michezo, hasa mamlaka hayo yanapokuwa yanaweza kusababisha migogoro na vyama vya kimataifa vya michezo.