WAJE TU WATAISOMA

Muktasari:
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 wakati Yanga ipo katika nafasi ya pili na pointi 43 baada ya kucheza mechi 18.
RAIS John Pombe Magufuli tayari amelipia kifurushi chake cha Azam TV na leo Jumamosi saa 10:00 jioni atakuwepo Ikulu jijini Dar es Salaam akishuhudia mchezo wa kwanza wa watani wa jadi Simba na Yanga tangu alipoingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana na kutumbua majipu kadhaa serikalini mpaka sasa.
Wakati Magufuli akiutazama mchezo huo pale Magogoni, shabiki nguli wa Yanga ambaye ni Rais wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, atautazama mchezo huo akiwa kwake Msoga mkoani Pwani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 wakati Yanga ipo katika nafasi ya pili na pointi 43 baada ya kucheza mechi 18.
Kocha wa Simba Jackson Mayanja ametamba kuwa kikosi chake hakiwezi kuzuilika kirahisi hii leo hasa baada ya kushinda mechi zote saba tangu alipopewa kazi ya kuifundisha timu hiyo mwezi uliopita.
“Utakuwa ni mchezo muhimu kwetu, tumefanya kazi kubwa hadi kufika hapa tulipo, wachezaji wanapambana na lazima tupambane zaidi, Yanga ni timu kubwa lakini ni sawa na timu nyingine za ligi, hatuoni sababu ya kuiogopa” alisema Mayanja maarufu kwa jina la Mia Mia.
Kocha Mdachi wa Yanga, Hans Van Pluijm anasema: “Tulikwama kidogo na Simba wametukuta, ni lazima sasa tupambane ili kushinda, mchezo dhidi yao utakuwa ni mchezo muhimu zaidi kwetu hasa katika mbio za ubingwa.”
FOMU YA KILA TIMU
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na fomu nzuri zaidi baada ya kushinda mechi zake saba za ligi ilizocheza kwa mwaka huu wa 2016 wakati Yanga imeshinda mechi tatu tu kati ya tano ilizocheza kwa mwaka huu.
Simba ilianza mwaka huu kwa kuifunga Ndanda bao 1-0 katika sherehe za mwaka mpya kabla ya baadaye kuzifunga Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, African Sports, Mgambo JKT, Kagera Sugar na Stand United. Yanga imezishinda JKT Ruvu, Ndanda na Majimaji huku ikitoka sare na Prisons na kupoteza mchezo dhidi ya Coastal Union.
JEURI YA KAMBI
Yanga imetumia usafiri wa anga kufika visiwani Pemba ikitokea Mauritius ilikokwenda kucheza mchezo wa awali wa klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cercle De Joachim na kuweka kambi ya wiki moja visiwani humo kujiandaa na mchezo huo wakati Simba ilisafiri kwa basi kutoka Shinyanga hadi Morogoro ilipoweka kambi.
Ikiwa visiwani Pemba Yanga ilifanya mazoezi makali katika siku za mwanzo kabla ya kupunguza dozi hiyo siku mbili za mwisho. Kazi kubwa aliyokuwa anaifanya Pluijm ni kupandisha morali ya timu na kuimarisha safu yake ya ulinzi itakayocheza bila uwepo wa beki kisiki Kelvin Yondani.
Makomandoo wa Yanga waliimarisha ulinzi katika kambi yao na kuhakikisha hakuna mtu asiyehusika anaingia huku pia wachezaji pamoja na viongozi wakizuiwa wasizungumze chochote kuelekea mchezo huo. Simba ilikuwa ndani ya eneo la chuo hivyo haikuhitaji ulinzi mkubwa sana lakini pia ulinzi wa kiinteligensia ulikuwa wa juu.
VITA YA WACHEZAJI
Ndani ya uwanja kutakuwa na vita ya mchezaji mmoja mmoja huku upinzani mkubwa ukitarajiwa kuwa kati ya Donald Ngoma (Yanga) na Juuko Murshid (Simba) na Nadir Haroub ‘Cannavaro’(Yanga) dhidi ya Hamis Kiiza(Simba).
Mabeki watakuwa na kazi ngumu ya kuwadhibiti washambuliaji hao wenye usumbufu mkubwa ambapo wachambuzi wengi wanatabiri kwa safu ya mabeki itakayozembea ndio itaamua matokeo ya mchezo huo.
Kutakuwa na mpambano pia kati ya kiungo Deus Kaseke (Yanga) dhidi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba) na Hija Ugando (Simba) dhidi ya Mwinyi Haji (Yanga) katika pande mbili za uwanja.
HAPO KATI SASA
YANGA: Msimu huu Yanga ina mabadiliko makubwa kwenye kiungo baada ya kurejea kwa Mzimbabwe Thaban Kamusoko ambaye ataungana na Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela na Mnyarwanda Mbuyu Twite ingawa mawinga, Mniger Issoufou Boubacar Garba na Deus Kaseke wana uwezo pia wa kucheza nafasi hiyo.
Yanga ina uwezekano wa kuwatumia wachezaji wanne katikati mfumo wa 4-4-2 ambapo viungo watakuwa watatu ambao ni Niyonzima pembeni kushoto, kati Kamusoko na Mbuyu Twite wakati pembeni kulia atacheza, Simon Msuva ama Deus Kaseke. Telela hatacheza mchezo huo kwa kuwa ana kadi tatu za njano wakati Makapu atakuwa pembeni akisoma mchezo.
SIMBA: Mzimbabwe Justice Majabvi, Jonas Mkude, Abdi Banda, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na Awadh Juma ingawa washambuliaji, Ibrahim Ajib na Hija Ugando pia wana uwezo huo.
Kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda ambaye kwa kawaida anapenda soka la kushambulia ili kuvuna mabao mengi ya kufunga, lakini mchezo huu kama ilivyo historia ya Simba atajaza viungo wengi na kuua winga moja kwa kuwatumia Majabvi kama kiungo mkabaji, atasaidiana na Mkude na Kazimoto.
Viungo wa Simba wanatajia kuwapa tabu kubwa wale wa Yanga katika mchezo huo kama ilivyokuwa pia kwenye mchezo wa mwisho. Yanga itategemea zaidi kupitisha mashambulizi yake pembeni.
NI SIMBA TENA?
Simba inaamini kuwa imekuwa na matokeo mazuri dhidi ya Yanga katika miaka ya hivi karibuni lakini hali ni tofauti kwani rekodi zinaonyesha kuwa Yanga imepata matokeo mazuri zaidi katika miaka mitano iliyopita.
Katika kipindi hicho Yanga imeshinda michezo minne, Simba miwili na michezo mingine minne ikimalizika kwa sare. Hii ni kwa michezo ya Ligi Kuu tu.
Ushindi mkubwa wa Simba ni ule wa bao 5-0 mwaka 2012 wakati Yanga ikiwa katika migogoro ya ndani huku Yanga ikipata ushindi mkubwa wa mabao 2-0 mara mbili tofauti katika kipindi hicho. Mchezo wa kushangaza zaidi ni ule wa sare ya mabao 3-3 Oktoba 2013 ambapo Yanga ilitangulia kufunga mabao hayo kabla ya kurejeshewa na Simba.
SIMBA KUSHANGILIA MIA MIA
Mashabiki wa Simba maeneo ya Buguruni na Ilala jana walikuwa wakipita na vuvuzela zao kwenye magari huku wakizipuliza na kuimba “Mia..mia” wakimaanisha kwamba wao kila kitu ni asilimia mia kuanzia kocha mpaka wachezaji.
Staili ambayo huenda wakaitumia kwa nguvu leo ndani ya Uwanja wa Taifa. Yanga wameonekana kujiamini pia kutokana na aina ya kikosi walichonacho ingawa wanaposikia neno Mayanja wanashtuka kisirisiri.
Mashabiki wa Yanga wamekuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kukosekana kwa Kelvin Yondani katika safu ya ulinzi huku Cannavaro akitarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza tangu mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana.
YANGA WOTE KUKAA SIMBA
Kanuni namba 14 ya Ligi Kuu inayozungumzia Taratibu za Mchezo kifungu cha (39) kinasema; Benchi la wachezaji wa akiba na viongozi zitapangwa kwa kuzingatia timu ya nyumbani kuwa upande wa kushoto na timu ngeni upande wa kulia mwa mwamuzi wa akiba (4th Official). Vyumba vya kubadilishia (changing room) na sehemu ya kufanyia mazoezi mepesi (warming up) vitakuwa upande uleule wa mabenchi kwa timu husika.
Katika mchezo wa leo Yanga ndiyo mwenyeji hivyo wachezaji wake watalazimika kukaa upande wa kushoto ambapo kwa jukwaani mara nyingi hukaa mashabiki wa Simba huku wachezaji wa Simba wakiketi upande wa kulia ambao jukwaani mara nyingi huwepo mashabiki wa Yanga.
Hali hii mara nyingi huzua hofu pindi wachezaji wanapokwenda kupasha misuli ili waingie uwanjani ambapo wachezaji wa Yanga watalazimika kupasha misuli mbele ya mashabiki wa Simba vivyo hivyo kwa upande wa pili.
HAWATABIRIKI HAWA
Manahodha wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara wamekaa pembeni na kuwaachia vigogo Simba na Yanga wauane wenyewe.
Nahodha Tanzania Prisons ambaye pia ni beki wa kushoto, Laurian Mpalule ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Hawa jamaa bwana huwa hawatabiriki kabisa unaweza kushangaa timu inayofanya vizuri ndiyo ndiyo inayofungwa. Mfano, utakapoangalia mechi za ligi hivi karibuni, unaweza kuwapa Simba kwa sababu wao wamefanya vizuri katika mechi zao za karibuni ambazo zitawafanya wawe na wanajiamini zaidi na kuifanya mechi kuwa rahisi kwao. Hawana tatizo kwenye ulinzi wala ushambuliaji wakati Yanga nao ni hivyo, wao pamoja na kutokuwa na matokeo mazuri kwenye ligi sasa, wamefanya vizuri mechi yao ya kimataifa ugenini na safu zao zote ziko vizuri.”
Kwa upande wa nahodha wa JKT Ruvu, Michael Aidan naye ni beki wa kulia amesema: “Kwa ukweli kuutabili mchezo wa Simba na Yanga huwa hutabiliki kabisa na ndiyo kinachonifanya nisite. Unaweza kungalia ubora wa kila kikosi kuangalia ulinzi hadi ushambuliaji kinachofanya vizuri ndiyo kinachoharibu. Ninachoweza kusema, timu itakayocheza vizuri ndiyo itakayoshinda.”
Kocha wa zamani wa Prisons Joseph Kanakamfumu anasema: “Simba imekuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kwa muda huku ikiwa na uwezo mzuri wa kutengeneza nafasi za kufunga kila mara kupitia kona zote za uwanja. Simba kwa sasa wanaweza kufunga kwa njia ya krosi kutoka pembeni, huku krosi hizo zikipigwa hata na viungo wa kati, lakini pia Simba imekuwa ikipata mabao mengi kupitia mipira ya kupenyeza katikati ya uwanja. Hii itawasumbua Yanga.
“Yanga kumekuwa na matumizi madogo ya viungo wenye ubunifu, hii inatokana na falsafa ya kocha Hans Pluijm kupenda kujaza washambuliaji wengi mbele na hivyo kusahau uwepo wa viungo bora ndani ya kikosi. Ni katika hilo ndipo tunapoona Yanga ikiwategemea viungo wawili tu walio bora kwa sasa Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima huku Salum Telela akiwa si chaguo la mwalimu kila mara.”
VIINGILIO
Kiingilio cha chini ni Sh7,000. Kiingilio cha juu cha mchezo huo ni Sh30,000 kwa VIP A, Sh20,000, VIP B & C Sh10,000 kwa viti vya rangi ya machungwa.
Tiketi za mchezo huo zinauzwa katika vituo vya TFF (Karume), Buguruni Oilcom, Ubungo Oilcom, Kidongo Chekundu (Mnazi Mmoja), Posta (Agip), Uwanja wa Taifa, Makumbusho Stand, Kivukoni Ferry.
MWAMUZI
Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi wote wenye beji za Fifa, mwamuzi wa katikati Jonesia Rukyaa (Kagera), akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha), mwamuzi wa akiba Elly Sasii (Dar) huku Kamisaa wa mchezo huo akiwa Khalid Bitebo (Mwanza).
MECHI NYINGINE
Za leo Mbeya City v Azam (Mbeya), Stand United v JKT Ruvu (Shinyanga), Toto v Kagera Sugar (Mwanza), Mgambo v Prisons (Tanga) na Majimaji v Mtibwa (Songea).
Kesho Jumapili ni Mwadui v Coastal Union (Shinyanga) na Ndanda v African Sports (Mtwara).
Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajib na Haji Ugando.
Akiba: Peter Manyika, Emiry Nimuboma, Novatus Lufunga, Said Ndemla, Awadh Juma, Danny Lyanga na Brian Majwega.
Yanga: Ally Mustafa, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Vicent Bossou, Mbuyu Twite, Pato Ngonyani, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima.
Akiba:Deo Munishi, Oscar Joshua, Said Juma, Malimi Busungu, Paul Nonga, Matheo Anthony na Issofou Boubacar