Wachezaji wote Yanga marufuku uswahilini

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm akiteta na baadhi ya wachezaji wa klabu ya Yanga. Picha ya Maktaba
Muktasari:
Mzungu huyo amewaambia wachezaji hao kuwa hadhi ya Yanga ya sasa si ya kuishi maisha ya uswahili badala yake wanapaswa kujitahidi kujiweka kwenye levo ya tofauti kuthibitisha ubora wao na aina ya rasilimali ambazo uongozi umewekeza kwao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amemtumia staa wa Tanzania, Mbwana Samatta kuwajaza upepo wachezaji wake kufanya mambo katika mechi nne za kimataifa zilizobaki msimu huu, lakini badae akafura dhidi ya nyota hao.
Mzungu huyo amewaambia wachezaji hao kuwa hadhi ya Yanga ya sasa si ya kuishi maisha ya uswahili badala yake wanapaswa kujitahidi kujiweka kwenye levo ya tofauti kuthibitisha ubora wao na aina ya rasilimali ambazo uongozi umewekeza kwao.
Aliwaambia wachezaji hao kwamba wazingatie nidhamu ya muda na kwamba hataki kusikia wala kuona mchezaji wa klabu hiyo akifanya mambo ya hovyo mitaani na ni marufuku kupanda bodaboda.
Kiungo wa timu hiyo, Deus Kaseke anaendelea kuuguza majeraha yake yaliyotokana na ajali ya bodaboda jambo ambalo limemfedhehesha Pluijm na kupigwa na butwaa kwa kutoamini kilichotokea na haamini kama kwa hadhi ya mchezaji wa mshahara na posho za Yanga anaweza kupanda bodaboda.
“Unajua wengi ni wachelewaji, tuna usafiri mzuri wa basi lakini wengi wamekuwa wakichelewa na kuamua kuchukua usafiri huu wa pikipiki sasa mwendo wake sio mzuri nimeambiwa wengi hawajui kuendesha kwa umakini,”alishangaa Kocha huyo.
“Nimewaambia kuanzia sasa sitaki kuona mchezaji anatumia pikipiki kila mmoja anatakiwa kuwahi klabuni mapema tuondoke na basi kwa pamoja na turudi kwa pamoja tukiwa salama lakini sio kuumia kwa mazingira ya namna hii. Na mchezaji yoyote wa Yanga ni marufuku kupanda bodaboda.”
Mechi za kimataifa
“Hizi ni mechi ambazo ukijiongeza kwa kupambana kwa ukweli ukafanikiwa kuonyesha kitu tofauti huwezi kubaki Yanga ni lazima timu zitakuona, mawakala na timu mbalimbali wanatafuta wachezaji katika mechi hizi,”alisema Pluijm.
“Nimewaambia wavute picha maisha ya Samatta alifanya vizuri katika mechi hizi hatua ya kwanza akauzwa TP Mazembe lakini alipofika huko akajituma zaidi kupituia mechi hizihizi akauzwa tena Genk sasa na wao hili linaweza kuwatokea kama wakitulia.”
“Yanga sasa inacheza mechi tofauti na zile za ligi kila mchezaji akipambana timu itafanikiwa lakini pia hata wao kama wachezaji kuna kitu wataongeza katika vipaji vyao a kufikia hata kuuzwa.”
“Nataka kuona ushindani unaongezeka katika kikosi, kwangu mimi kila mchezaji ana nafasi ya kucheza unachohitaji ili uvae jezi ya kuitumikia timu ni kiwango chako hakuna lingine.”
Dante abadilika
Beki mpya wa Yanga, Vicent Andrew ‘Dante’ amesema ndani ya mwezi mmoja aliokaa na Yanga, amejifunza mambo mawili kujua kocha wake Hans Pluijm anahitaji nini kwake na wenzake wanacheza soka la aina gani.
“Kocha Pluijm amekuwa akinirekebisha jinsi ya kukaba hivyo nina hatua nyingine tofauti na nilivyokuwa Mtibwa Sugar, ambako kocha Mecky Maxime alikuwa na mbinu zake,” alisema.
Dante anafichua kwamba siku za mwanzo alikuwa anaona amekumbana na mtihani mgumu jinsi alivyokuwa anawaona mabeki wenyeji kama Kelvin Yondan, Hajji Mwinyi, Vincent Bossou na Oscar Joshua,wanavyokaba alijua ana kazi ya ziada mbele ya wakongwe hao.
“Kwa sasa najiamini kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kupata namba ndani ya kikosi cha kwanza cha Pluijm kwani nimewasoma nimeanza kuingia kwenye fomu yao,” alisema
Mbali na ushindani wa mazoezi pia alieleza kwamba Yanga, ameikuta inashiriki michuano ya kimataifa, jambo hilo limempanua akili yake kuwaza kimataifa na kuamini kwamba hakuna linaloweza kushindikana mbele ya malengo.
“Kila jambo lina hatua zake, nilipokuwa Mtibwa nilitamani kuitumikia Yanga na sasa nawaza kwamba nina uwezo wa kufika mbali zaidi, hivyo ninafanya juhudi kwa kila jambo najua hakuna jambo rahisi,” alisema