Wachezaji wa Bandari FC wakishangilia ushindi wa bao 1-0

Wachezaji wa Bandari FC wakishangilia ushindi wa bao 1-0
ABDULRAHMAN SHERIFF Wachezaji wa Bandari FC wakishangilia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Thika United katika mechi ya Ligi Kuu Kenya (KPL) iliyochezwa Uwanja wa Mbaraki. MWENYEKITI wa Chama cha Soka Kenya (KFA) tawi dogo la Mombasa, Ali Hassan Tito, ameipongeza Bandari FC kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Thika United katika mechi iliyochezwa Jumamosi iliyopita. Tito alisema ushindi huo unafurahiwa na wapenda soka wote mkoani Pwani na ni dalili kwamba Bandari inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao. Tunaitakia kila la kheri timu yetu ya Bandari ifanikiwe kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya Chemelil Sugar. Tunajua wanaweza kutekeleza na kukamilisha kazi yao hapo Novemba 26,” alisema Tito. Naye mwakilishi wa soka ya wanawake tawi la Pwani Kusini, Asha Pili Ramadhani, aliwataka wanasoka wa Bandari waendelee kuwa na moyo wa kujibidiisha kwa mazoezi na kucheza kwa makini wapate ushindi katika mechi ya mwisho. Nawapongeza kwa jinsi mlivyoonyesha soka zuri dhidi ya Thika United na ushindi wenu ni wa kujivunia, lakini tunachotaka ni kuhakikisha hampotezi mchezo wenu dhidi ya Chemelil, tunawatakia kila la heri, alisema alipozungumza na wachezaji hao. Mwenyekiti wa KFA tawi la Malindi, John Ngoa, pia alitoa ombi kwa mashabiki wa soka wenye uwezo kutoka Pwani waifuate timu hiyo hadi Chemelil kuishangilia ili ishinde isishuke daraja. Bandari ndiyo wamebakia kuwa wakombozi wetu watu wa Pwani, tuipe nguvu kwa kuishangilia,” alisema. Shabiki sugu wa soka mkoani Pwani, Kombo Dzarino, wa Likoni alisema umefika wakati kwa mashabiki wote wa Pwani kuondoa chuki na kuiombea Bandari ishinde mchezo wao wa mwisho. Mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wakiwemo wa Lamu, Kilifi, Kwale, Witu, Mpeketoni, Voi na Msambweni, wameanza kuwa na matumaini ya timu hiyo ya kutoshuka daraja.