Wabaya wa Yanga hawa hapa

Muktasari:

Droo hiyo itahusisha jumla ya klabu 16 kutoka mataifa 14 ambazo zimefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kupenya ile ya mtoano ambayo mechi zake za marudiano zilichezwa Jumanne na Jumatano wiki iliyopita.

Dar es Salaam. Yanga itafahamu rasmi timu tatu itakazopangwa nazo pamoja kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo droo yake itachezeshwa leo saa 9.00 Alasiri, jijini Cairo, Misri.

Droo hiyo itahusisha jumla ya klabu 16 kutoka mataifa 14 ambazo zimefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kupenya ile ya mtoano ambayo mechi zake za marudiano zilichezwa Jumanne na Jumatano wiki iliyopita.

Katika kundi hilo la timu 16, Yanga ina uwezekano wa kukutana na timu tatu kati ya 13 tu kwani nyingine tatu zitawekwa katika chungu kimoja sambamba na wawakilishi hao wa Tanzania wakati wa uchezeshaji wa droo hiyo.

Timu tatu pekee ambazo hazina uwezekano wa kupangwa kundi moja na Yanga katika hatua hiyo ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Gor Mahia (Kenya) pamoja na Rayon Sports (Rwanda).

Kutokana na pointi ilizonazo kulingana na mafanikio na ushiriki wake katika mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu, Yanga itawekwa katika chungu cha pili sambamba na timu hizo tatu, huku chungu cha kwanza kikiwa na klabu za AS Vita Club, Enyimba, Al-Hilal pamoja na USM Alger.

Chungu cha tatu kitakuwa na timu za Aduana Stars, Williamsville, UD Songo pamoja na Raja Casablanca wakati chungu cha nne kitakuwa na timu za RS Berkane, Djoliba, CARA Brazzaville na Al-Masry.

Baada ya droo hiyo kuchezeshwa, mechi za hatua hiyo kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), zitaanza kuchezwa kuanzia Mei 16 na zinatarajiwa kumalizika Agosti 29 na baada ya hapo timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu hatua ya Robo Fainali.

Yanga itakuwa na kibarua cha kuvunja rekodi yake isiyoridhisha ya kutowahi kufika mbali zaidi ya hatua ya makundi kwani mara zote ambazo imekuwa ikiingia kwenye hatua hiyo, imekuwa ikimaliza ikiwa imeshika mkia ambapo ilikuwa ni mwaka 1998 na 2016.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema tuko tayari kupangiwa na timu yoyote ile kwa sababu jina la timu halichezi bali ni wachezaji. Sisi kama wachezaji tunachoamini ni kwamba tukiwa fiti na tukafuata maelekezo ya benchi la ufundi, tunaweza kufanya vizuri dhidi ya timu yoyote ile tutakayopangwa nayo.

“Tumeshawahi kucheza na timu bora na kubwa zaidi ya hizo zilizopo na tuliweza kuzifunga hivyo sidhani kama tunaweza kuhofia klabu yoyote kati ya hizo zilizofuzu," alisema Cannavaro.