Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waarabu waweka mzigo pambano la Fury, Joshua

Muktasari:

Kichapo alichokitoa kwa Wilder kimewakuna na wanataka kuona pambano lake lijalo linachezwa Saudi Arabia hasa lile la kuunganisha mikanda dhidi ya Joshua, na ndiyo maana mezani wameweka Dola 517 milioni.

LAS VEGAS, MAREKANI . KUDADADEKI! Umesikia mzigo ambao Waarabu wa Saudi Arabia wameweka mezani kwa ajili ya pambano la Tyson Fury dhidi ya Anthony Joshua au Deontay Wilder? Ni kufuru.

Ishu kamili iko hivi, familia ya kifalme ya Saudi Arabia inataka kuona pambano lijalo la Fury linafanyika nchini mwao iwe dhidi ya Joshua au Wilder na kama uwajuavyo Waarabu wanapotaka jambo lao pesa hutumika kufanikisha.

Si unakumbuka kilichotokea kwa Joshua na Andy Ruiz Jr? Dola 70 milioni tu zilitosha kupeleka pambano lao la marudiano Saudi Arabia na kuzipotezea kelele zote za walioponda kitendo hicho. Pesa iliongea. Katika pambano hilo Joshua aliingiza Dola 60 milioni milioni wakati mpinzani wake, Ruiz Jr alipiga Dola 10 milioni - pesa ambazo zilikuwa ndefu zaidi kwa kila mmoja katika historia yake ya ngumi. Si mchezo.

Inaonekana shoo ya Joshua na Ruiz Jr iliwakuna sana na sasa Saudi Arabia wanataka burudani nyingine ya ngumi, lakini safari hii akili yao yote ipo kwa Tyson Fury au The Gypsy King kama anavyojulikana na wengi.

Kichapo alichokitoa kwa Wilder kimewakuna na wanataka kuona pambano lake lijalo linachezwa Saudi Arabia hasa lile la kuunganisha mikanda dhidi ya Joshua, na ndiyo maana mezani wameweka Dola 517 milioni.

Ndiyo, Dola 517 milioni! Hatari sana

Wanajua ugumu uliopo kulipata pambano la Fury kwa wakati huu, na wanajua kama pambano hilo litakuwa dhidi ya Joshua basi ndiyo itakuwa ngumu zaidi kwa sababu Waingereza watalitaka pale kwao England. Si unajua wote wajukuu wa Malkia. Lakini kwa sababu siku zote penye uzia penyeza rupia, Saudi Arabia wameamua kupenyeza rupia za kutosha kwenye uzia ili kufanikisha harakati zao ndiyo maana Dola 517 milioni za mafuta zimewekwa mezani.

Picha lilianza siku ileile ya pambano la Fury na Wilder, kwa sababu wanafamilia wanne wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia walikuwepo katika ukumbi wa MGM Grand Arena, Las Vegas, Nevada, Marekani kushuhudia shoo ile ya kibabe.

Ile mikono mfululizo aliyokuwa anatupa Fury imewakuna na sasa wanataka kuiona wakiwa kwenye ardhi yao ya nyumbani. Watafanyaje kufanikisha hilo? Wameamua kutumia pesa maana wanajua ile ni sabuni ya roho. Mchakato wa kumpeleka Fury, Saudi Arabia unasimamiwa na Mwanamfalme Khaled ambaye amepewa majukumu na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman kupeleka matukio ya kimichezo nchini humo ili kumaliza kelele za uvunjifu wa haki za binadamu zinazolichafua taifa hilo.

Khaled anaamini Gypsy King ndiye mtu sahihi wa kusafisha taifa hilo na ndiyo maana anataka pambano lake lijalo lipigwe Saudi Arabia kwa gharama yoyote ile.Japokuwa Waarabu wanamtamani zaidi Joshua, lakini wanaweza kumpata Wilder ambaye tayari ametumia kipengele cha mkataba wake kudai pambano la marudiano dhidi ya Fury, lakini vyovyote itakavyokuwa pesa itatumika.

Lakini, wakati Waarabu wakitenga dau hilo si vibaya kutazama mapambano ya ngumi ambayo yamewahi kuangaliwa kwa gharama kubwa zaidi na mabondia kupiga pesa ndefu.

6. Tyson vs Holyfield II

Mwaka: 1997

Mzigo: Dola 100 milioni

Hili ndilo pambano ambalo Mike Tyson alimng’ata sikio Evander Holyfield. Hili lilikuwa ni pambano la marudiano lililofanyika katika ukumbi wa MGM Grand. Pambano hilo liliingiza Dola 100 milioni na lilivunjika katika raundi ya tatu baada ya Tyson kumng’ata sikio mpinzani wake. Katika pambano hilo Holyfield aliingiza Dola 35 milioni na Tyson Dola 30 milioni.

5. Tyson vs Lewis

Mwaka: 2002

Mzigo: Dola 112 milioni

Mwaka 2002, Tyson alipanda ulingoni kupambana na Lennox Lewis katika Uwanja wa Pyramid Arena, Memphis, Tennessee, Marekani. Wawili hao walikuwa wanachukiana sana na ilifika hatua Tyson akadai anataka kumuua Lewis. Siku ya pambano Tyson alichapwa kwa KO, kila bondia akaingiza Dola 17.5 milioni.

4. Mayweather vs De la Hoya

Mwaka: 2007

Mzigo: Dola 136 milioni

Pambano hili kati ya Mayweather dhidi ya The Golden Boy, Oscar de la Hoya lilikuwa kubwa sana katika miaka hiyo, likiweka rekodi kibao zilizodumu kwa miaka mingi. Mayweather alishinda kwa pointi na kuchukua mkanda wa uzito wa unyoya wa WBC. De la Hoya alipiga Dola 52 milioni na Mayweather, Dola 25 milioni

3. Mayweather vs Canelo Alvarez

Mwaka: 2013

Mzigo: Dola 150 milioni

Mayweather na Canelo Alvarez waliingia kwenye mwaka 2013 wakiwa hawana rekodi ya kupigwa. Mayweather alishinda pambano hili kwa pointi na kupiga Dola 80 milioni wakati mpinzani wake akiingiza Dola 12 milioni. Pambano hilo lilikuza jina la Alvarez ambaye baadaye alikuja kusaini mkataba mnono wa miaka mitano na kampuni ya DAZN wenye thamani ya Dola 365 milioni.

2. Mayweather vs McGregor

Mwaka: 2017

Mzigo: Dola 360 milioni

Pambano lisilo la ubingwa kati ya Floyd Mayweather Jr dhidi ya Conor McGregor, liliwaingizia wawili hao jumla ya Dola 360 milioni ambapo Mayweather Jr alipiga Dola 275 milioni na McGregor Dola 85 milioni. Kabla ya pambano mezani iliwekwa Dola 130 milioni ambapo Dola 100 milioni ilitakiwa kwenda kwa Mayweather na Dola 30 milioni kwa mpinzani wake. Pesa hizo zilipanda baada ya kupata matangazo na haki za televisheni.

1. Mayweather vs Pacquiao

Mwaka: 2015

Mzigo: Dola 410 milioni

Katika pambano hili mezani kulikuwa na Dola 400 milioni ambapo Mayweather alipiga Dola 250 milioni na Manny Pacquiao Dola 150 milioni. Mashabiki milioni 4.6 walinunua haki ya kutazama pambano hilo moja kwa moja kwenye televisheni. Mayweather alishinda kwa pointi.