Waarabu wamganda Kamusoko Dar

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm ana mchezaji wa timu, Thaaban Kamusoko.
Muktasari:
YANGA na mashabiki wao walikuwa wakiamini kuwa, wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri wamesharejea kwao ili kujipanga kwa mechi yao ya marudiano, lakini kumbe wapi, jamaa wameamua kukomaa hapa hapa.
YANGA na mashabiki wao walikuwa wakiamini kuwa, wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri wamesharejea kwao ili kujipanga kwa mechi yao ya marudiano, lakini kumbe wapi, jamaa wameamua kukomaa hapa hapa.
Mabosi wa Ahly wameganda jijini Dar es Salaam ili kuifuatilia Yanga na hasa kiungo wao fundi, Thabani Kamusoko na straika Donald Ngoma na juzi Jumatano katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara waliwashuhudia kwenye Uwanja wa Taifa na kuwarekodi video kisha kuituma kwao kuifanyia kazi.
Waarabu ni kama wameingiwa mchecheto na kiwango cha Yanga, hivyo kuamua kuifuatilia kwa makini mechi yao dhidi ya Mwadui inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye ni mwanachama wa Simba.
Yanga iliifunga Mwadui 2-1, lakini timu hiyo ilikuwa na makosa kadhaa ya kiufundi ikiwemo safu ya ulinzi kukosa umakini na kiungo cha timu hiyo chini ya Ras Kamusoko anayeonekana kuzidi kupwaya. Ni kama vile Ahly haijakubali kiwango cha Kamusoko na kudhani aliwazuga ndio maana wamebaki kumsoma zaidi.
Pia walitaka kujiridhisha na kiwango cha straika Ngoma aliyewasumbua, sambamba na nyota wengine wa Yanga ambao waliwapeleka mchakamchaka katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Jumamosi iliyopita na kuisha kwa sare ya 1-1.
Ahly tayari wamechukua kipande cha picha za video za mechi hiyo ya kiporo cha ligi ili kuisoma zaidi Yanga kabla ya mechi ya marudiano ya Jumatano ijayo.
Yanga katika mechi na Mwadui ilifanya mabadiliko ya wachezaji watano katika kikosi kilichocheza dhidi ya Ahly kwa kuwaanzisha kipa Deo Munishi ‘Dida’ mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Haruna Niyonzima na winga Simon Msuva aliyeingia kipindi cha pili kwenye mechi ya dhidi ya Ahly.
Mabadiliko hayo ambayo yalishuhudia kipa Ally Mustapha ‘Barthez’, mabeki Kelvin Yondani na kiungo Salum Telela na winga Issofou Boubakar wakianzia nje huenda yakawagharimu Waarabu hao kwani Yanga ilikuwa na utofauti mkubwa wa kiuchezaji japo pia ilionyesha mapungufu kadhaa makubwa.
Ni kama vile Yanga imewazuga Waarabu hao kwani walioumana nao katika mechi ya awali si waliowaona katika mchezo huo wa juzi ambao vijana wa Julio waliwakimbiza wapinzani wao kabla ya Niyonzima kuwanyamazisha mwishoni.
Akili nyingi
Kitendo cha Waarabu hao kufuatilia mechi za ligi kuu za Yanga kinaonyesha namna wanavyoipa uzito mkubwa mechi ya marudiano kwa kuhakikisha wanakuwa na taarifa sahihi za wapinzani wao, lakini Yanga nayo imetanguliza mtu mmoja tu nchini Misri kuandaa mazingira ya hoteli za kufikia na si ya ufundi.
Tofauti hiyo ya maandalizi huenda ikaongeza ugumu wa mchezo huo kwa Yanga baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani, licha ya kocha wa timu hiyo, Hans Van Pluijm kusisitiza ngoma bado mbichi.
“Mchezo bado upo wazi, tunaweza kwenda kushinda kwao, kama wamepata sare hapa kwanini sisi tushindwe kupata matokeo kwao, kikubwa ni kuhakikisha tunafunga mabao,” alisema Pluijm.
Hata hivyo rekodi zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1982 Yanga haijawahi kupata ushindi wa aina yoyote kwenye ardhi ya Waarabu zaidi ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Ismailia ya Misri mwaka 1992 baada ya awali kuchezea kichapo cha 2-0 nyumbani.