Prime
Waamuzi: Yanga wameonewa

Muktasari:
- Timu hiyo ilivaana na Mamelodi katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Luftus Versfeld jijini Pretoria na kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90 kama ilivyokuwa mchezo wa kwanza uliochezwa Kwa Mkapa wiki iliyopita na kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti wenyeji wakashinda 3-2 na kufuzu nusu fainali.
KIKOSI cha Yanga kilirejea Dar es Salaam usiku wa jana kutoka Sauzi kilipokwenda kucheza mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku gumzo likiwa ni bao la kiungo Stephane Aziz KI lililokatawaliwa na VAR, lililowaibua baadhi ya waamuzi nchini waliodai imeonewa.
Timu hiyo ilivaana na Mamelodi katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Luftus Versfeld jijini Pretoria na kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90 kama ilivyokuwa mchezo wa kwanza uliochezwa Kwa Mkapa wiki iliyopita na kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti wenyeji wakashinda 3-2 na kufuzu nusu fainali.
Hata hivyo, gumzo kubwa ni kukataliwa kwa bao la dakika 59 lililofungwa na Aziz KI aliyefumua shuti kali akipokea pasi ya Kennedy Musonda na mpira kugonga besela kabla ya kuangukia ndani, kisha kurejea uwanjani ambapo mwamuzi Dahane Beida kutoka Mauritania kupitia VAR alilikataa.
Tayari mabosi wa Yanga waliorejea jana saa 2 usiku, wameaiandikia barua CAF kulalamikia kitendo cha waamuzi wa mchezo huo kulikataa bao hilo ambalo wanaamini lingewavusha kwenda nusu fainali bila mechi kufika hadi katika mikwaju ya penalti, huku baadhi ya waamuzi nchini wakisema lilikuwa halali japo matokeo hayawezi kubadilishwa.
Baadhi ya waamuzi hao wa zamani wamesema Yanga ilinyimwa bao halali kutokana na mpira kuvuka mstari wa lango, huku wengine wakieleza sababu kubwa iliyoinyima ushindi ni kukosekana teknolojia ambayo ingeweza kuibeba kwenda nusu fainali badala ya Mamelodi..
Erick Onoka ambaye pia ni mwamuzi mstaafu kutoka jijini Arusha alisema kilichotokea kwa upande wake anaamini hakikuwa sawa kwa sababu Yanga ilistahili kupata bao hilo kutokana na mpira uliopigwa kuonekana wazi kupita mstari wa kati ya goli.
“Wengi wanahoji kwanini mwamuzi hakwenda kuangalia VAR mwenyewe tukio lile, lakini ninachofahamu endapo kutakuwa na utata ndipo wale wasaidizi kwenye vyumba wanaweza kumuita akajiridhishe. Kwangu Yanga imenyimwa bao halali kabisa,” alisema Onoka, huku mwamuzi mkongwe Israel Mujuni Nkongo akiliambia Mwanaspoti, mwenye uamuzi wa mwisho katika mchezo ni mwamuzi hivyo hakuna sababu ya kutafuta mchawi.
“Huenda walikosea au walipatia kwa jinsi walivyoona wao ila mashabiki wanapaswa kutambua uamuzi wa mwisho ukishatolewa basi unabaki kama ulivyo, katika uamuzi kuna watakaoumia na watakaofurahia hivyo tuheshimu yaliyotokea,” alisema Nkongo.
Mwamuzi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema ameshangazwa na uamuzi uliofanyika kwani ni dhuluma ya wazi iliyoikosesha Yanga nafasi ya wazi ya kusonga nusu fainali ya mashindano hayo.
“Kilichofanyika ni kama dhuluma. Yanga ilistahili kupewa bao kwani lilikuwa halali hata katika marejeo ya televisheni, ila ndio basi tena, wenyeji wamenufaika na uamuzi huo,” alisema mwamuzi huyo.
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Dahane Beida kutoka Mauritania anakumbukwa kwani aliwahi kuchezesha mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita wakati Yanga iliposhinda bao 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Bao hilo lilitokana na penalti iliyokwamishwa wavuni na beki Djuma Shaban ambaye kwa sasa hayupo.
Mechi hiyo iliyopigwa jijini Algeria Juni 3, mwaka jana haikuweza kuipa Yanga taji hilo la Afrika kutokana na faida ya bao la ugenini kwani ilishindwa kutamba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kufungwa mabao 2-1, Mei 28 mwaka jana.
ISHU YA RUFAA
Mapema jana Yanga Yanga iliwasilisha malalamiko yake kwa barua iliyomwandikia katibu mkuu wa CAF, ikitaka hatua zichukuliwe dhidi ya waamuzi wa mchezo huo kwa kulikataa bao halali la Aziz KI.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Yanga inadai tukio la kukataliwa kwa bao hilo ni upangaji wa matokeo na imependeza mambo kadhaa yafanyike ikiwamo kuchukuliwa hatua kwa waamuzi wa mchezo huo.
Pia inadai mwamuzi wa kati kwa makusudi hakutaka kwenda kuangalia VAR ili kujiridhisha kama bao hilo lilikuwa halali au la, hivyo kwa ujumla hakukuwa na usawa katika mchezo huo.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Aden Rage, mwenyekiti wa zamani wa Simba aliyewahi kuwa katibu mkuu wa TFF (enzi za FAT) alisema licha ya Yanga kuliandikia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kulalamikia bao hilo, uamuzi wa mchezo huo hautabadilishwa zaidi ya mwamuzi wa mchezo kuadhibiwa.
Rage alisema hata kama Yanga itakata rufaa CAF bado matokeo yatabaki yalivyo ila ikitokea wakajiridhisha waamuzi wa mchezo huo walifanya makosa kitakachofanyika ni kuwaadhibu kutokana na kanuni na sheria walizojiwekea.
“Mwenye uamuzi wa mwisho ni refa, hivyo hata akikataa bao la halali msimamo wake utaendelea kubaki kama ilivyo na baada tu ya hapo wahusika watakaa chini na kuangalia kilichotokea na kutolea uamuzi, lakini sio kubadili matokeo ya uwanjani,” alisema Rage
Kiongozi huyo mkongwe wa soka nchini alifafanua utata uliojitokeza kwa bao hilo la Aziz KI ni kutokana na kutoonekana vizuri mpira wakati ukiwa ndani kwa sababu kwa pembe moja inaonyesha ni kweli uliingia, ila kwa kuangalia kamera za upande wa goli ni ngumu kujua uliingia au la.
YANGA NA SIMBA
Licha ya gumzo hilo kwa upande wa Yanga, lakini wadau mbalimbali nchini wametoa maoni yao juu ya kilichozikwamisha Simba na Yanga kufuzu robo fainali katika michuano hiyo ya msimu huu na kuzipa mbinu za kufanya kwa ajili ya michuano ijayo ili kuendelea kuleta ushindani zaidi.
Kama ilivyokuwa kwa Yanga iliyotolewa na Mamelodi ugenini, Simba nayo ikicheza jijini Cairo, Misri ilikumbana na kipigo kingine kutoka kwa watetezi wa taji Al Ahly iliyoifumua kwa mabao 2-0 na kufuzu nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 baada ya wiki iliyopita kushinda pia bao 1-0 Kwa Mkapa.
Hiyo ilikuwa robo fainali ya tano kwa Simba katika misimu sita ikikwamia robo fainali na tayari nayo usiku wa jana ilirejea nchini kujiandaa na mechi za 16 Bora ya Kombe la Shirikisho ikitarajiwa kucheza na Mashujaa Kigoma keshokutwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, wakati Yanga itakuwa Jamhuri Dodoma kuumana na Dodoma Jiji kabla ya kuigeukia Ligi Kuu kusaka tiketi nyingine za CAF.
Akizungumza kilichofanywa na timu hiyo, Rage alizipongeza timu zote kwa hatua kubwa ilizofikia huku akieleza sababu kubwa ilizozikwamisha ni kukosa washambuliaji wazuri wenye njaa na uchu wa kufikia mafanikio yaliyowekwa na viongozi.
“Yanga ingekuwa na mshambuliaji wao wa zamani, Fiston Mayele kwa sasa tungezungumza mengine kwa sababu inakosa aina ya mtu kama yeye. Timu yao bado ni nzuri sana na wakiboresha tu eneo hilo naamini wanaweza kuleta taji la Afrika,” alisema Ragen aliyewahi kucheza kama beki wa kushoto.
Rage aliongeza kwa upande wa Simba kumekuwa na upungufu mwingi katika eneo la ushambuliaji kwani kitendo cha kuondoka kwa Moses Phiri na Jean Baleke kwa wakati mmoja kimeleta shida kwa sababu walioingia dirisha dogo la usajili wanahitaji kuzoeana zaidi.
Kwa upande wa kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Habibu Kondo alisema timu hizo zimeonyesha ushindani, ingawa bado kuna upungufu mwingi kwenye eneo la ushambuliaji kwani licha ya viungo wao kutengeneza nafasi nyingi lakini hawajazitumia kufunga mabao.
Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi imeandika rekodi mpya baada ya kutinga hatua hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika 1997.
Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.
Timu hii ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi D kwa msimu huu ikiwa na pointi nane sawa na CR Belouizdad ya Algeria ila Yanga ilinufaika tu na faida ya jinsi zilivyokutana zikiwa nyuma ya mabingwa mara 11 wa michuano hiyo, Al Ahly iliyomaliza na pointi 12.
Simba iliyotinga hatua ya robo fainali ya CAF kwa mara ya tano katika kipindi cha miaka sita, ilimaliza nafasi ya pili na pointi tisa sawa na Wydad Casablanca ya Morocco huku Jwaneng Galaxy ya Botswana ikiburuza mkiani na pointi zake nne. Kinara wa kundi hilo alikuwa ni ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambayo ilikuwa na pointi 11 baada ya michezo yake sita. Tangu Simba ilipocheza nusu fainali enzi za Klabu Bingwa 1974, haijawahi kuifikia tena hatua hiyo, kwani mara tano tofauti imeishia robo fainali, ikiwemo ya 1994 kabla ya mfumo kubadilishwa na 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024.