Waafrika walivyoangusha dhoruba raundi ya kwanza England

Papiss Cisse
Muktasari:
Hapana shaka ndiyo maana baadhi ya timu huwa zinapata wakati mgumu pindi wachezaji wa Afrika wanaporudi nyumbani kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
JEURI ya Wazungu dhidi ya wachezaji wa Afrika inazidi kupungua. Robo ya mabao yaliyofungwa katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu England iliyoanza wikiendi iliyopita yalifungwa na wachezaji kutoka Afrika. Hapana shaka ndiyo maana baadhi ya timu huwa zinapata wakati mgumu pindi wachezaji wa Afrika wanaporudi nyumbani kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Yaya Toure vs West Brom
Kiungo huyo mahiri wa kimataifa wa Ivory Coast alirudi katika ubora wake ambao wengi tunaufahamu. Yaya alikuwa mhusika mkuu katika mauaji ya City dhidi ya West Brom katika ushindi wa mabao 3-0 pale kwenye dimba la Hawthorns alipofunga mabao mawili muhimu.
Bao lake la kwanza lilitokana na shuti ambalo lilimbabatiza David Silva na kutinga wavuni na la pili halikuwa na utata. Alipokea pasi murua kutoka kwa raia mwenzake wa Ivory Coast, Wilfried Bony na kupiga shuti kali ambalo lilimwacha kipa wa West Brom, Boaz Myhill, akiwa amezubaa hana la kufanya.
Riyad Mahrez vs Sunderland
Winga mahiri wa kimataifa wa Algeria ambaye Jumamosi aliwateka mashabiki waliofurika dimba la King Power. Mahrez alizaliwa Ufaransa lakini ana uraia wa Ufaransa, Algeria na Morocco.
Alikuwa chachu kubwa kwa vijana wa Kocha Claudio Ranieri, ambao walidhamiria kuanza ligi kwa kishindo. Alifunga mabao mawili na kuifanya Leicester kuongoza kwa mabao matatu hadi dakika ya 25 ya kipindi cha kwanza.
Kiungo huyu wa zamani wa Le Havre ya Ufaransa, alikuwa chachu kubwa wakati akiiokoa Leicester isishuke Ligi Kuu msimu uliopita na anaonekana ataendelea kuwa shujaa wao msimu huu.
Kouyate vs Arsenal
Kiungo wa kimataifa wa Senegal ambaye ndiye aliyeanza kuwaduwaza mashabiki wa Arsenal duniani kote pamoja na kocha wao, Arsene Wenger, wakati West Ham walipopata ushindi wa kushangaza nyumbani kwa Arsenal pale Emirates katika mechi ya kwanza tu.
Kouyate aliyezaliwa Dakar, Senegal alifunga bao la kwanza kwa kuuwahi mpira wa faulo uliopigwa na winga mpya wa West Ham, Mfaransa Dimitri Payet na kumwacha kipa Petr Cech akiwa hana la kufanya.
Shabiki mmoja wa kike wa West Ham amejichora mchoro (tattoo) katika mwili wake ambao unaonyesha matokeo ya mechi hiyo na majina ya wafungaji. Jina la Kouyate litakaa katika mwili wa dada huyo kwa maisha yake yote.
Arouna Kone vs Watford
Achilia mbali Yaya Toure, kuna staa mwingine wa Ivory Coast ambaye aliwaonyesha mashabiki wa soka la England kile ambacho wachezaji wa taifa hilo wanaweza kufanya katika Ligi Kuu England.
Arouna Kone alikuwa shujaa wakati Everton iliposawazisha bao katika dakika za majeruhi katika dimba la nyumbani la Goodison Park na kuzuia aibu kubwa kutoka kwa wageni Watford.
Bao la Kone katika dakika za majeruhi ndilo ambalo lilisaidia ubao wa matokeo usomeke 2-2. Vinginevyo ingekuwa aibu kwa Everton kuchapwa nyumbani na timu ambayo ndiyo kwanza imepanda Ligi Kuu.
Odion Ighalo vs Everton
Bao ambalo Kone alikuwa amelisawazisha katika mechi hii dhidi ya Watford nalo lilikuwa limetoka Afrika. Mtu ambaye alikuwa anakaribia kuiaibisha Everton ni mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Odion Ighalo, ambaye bao lake lilionekana kuwa lilikuwa limekaribia kukipa ushindi kikosi cha Kocha Quique Sanchez Flores.
Staa huyu mzaliwa wa Lagos mwenye umri wa miaka 26, alikuwa ameingia uwanjani akitokea benchi na kutupia bao la pili lililoufanya ubao wa matokeo usomeke 2-1 kwa Watford kuwa mbele. Inavyoonekana Ighalo anarudia makali yake ya msimu uliopita ambao kwa kiasi kikubwa mabao yake yalichangia timu hiyo inayoshabikiwa na mwanamuziki, Elton John kutinga Ligi Kuu.
Rudy Gestede vs Bournemouth
Baada ya kumpoteza mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Christian Benteke, aliyenunuliwa na Liverpool, kocha wa Aston Villa, Tim Sherwood, alihitaji mshambuliaji mwenye sifa zile zile kwa ajili ya kuziba pengo hilo.
Nyota wa kimataifa wa Benin, Rudy Gestede, alimwonyesha kuwa yeye alikuwa mtu sahihi baada ya kuifungia Aston Villa bao la ushindi ikiwa ni mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu katika timu hiyo. Gestede ambaye alinunuliwa kwa dau la Pauni 6 milioni kutoka Blackburn katika dirisha hili la uhamisho, alifanikiwa kuizamisha Bournemouth katika uwanja wao wa nyumbani kwa bao hilo moja la ushindi. Staa huyu alizaliwa Ufaransa, lakini anakipiga katika katika timu ya taifa ya Benin.
Andre Ayew vs Chelsea
Mmoja kati ya nyota wa Afrika wanaotazamiwa kuitengenezea Afrika heshima kubwa katika Ligi Kuu England hasa baada ya mastaa kama Didier Drogba kuanza kuondoka.
Haikuchukua muda mrefu kabla ya Ayew kuonyesha kile anachokusudia kufanya baada ya kufunga bao muhimu la kusawazisha katika pambano la ufunguzi dhidi ya mabingwa Chelsea katika uwanja wa nyumbani, Stamford Bridge.
Achilia mbali bao hilo, Ayew alionyesha kiwango kikubwa cha soka na kufanikiwa kuipa Swansea matokeo ya kushangaza ya sare ya 2-2 ingawa Chelsea ilitazamiwa kushinda pambano hilo.
Papiss Cisse vs Southampton
Wakati Kouyate akiikandamiza Arsenal katika dimba la Emirates, staa mwingine wa Senegal, Papiss Demba Cisse, alikuwa akiendeleza makali yake ya kawaida katika dimba la St James’ Park ambalo ni kama vile limemzoea kwa sasa.
Cisse alikuwa miongoni mwa wafungaji wa mabao mawili ya Newcastle katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya timu ngumu ya Southampton ambayo ilikuwa inaongozwa na staa wa kimataifa wa Kenya, Victor Wanyama.
Mataifa mengine
Wachezaji kutoka nchi nyingine za Ulaya walifunga mabao 14, wakati kulikuwa na wachezaji watatu tu kutoka Amerika Kusini ambao walifunga katika raundi hiyo. Bao moja kati ya hayo lilikuwa ni lile shuti la Philippe Coutinho wa Liverpool katika lango la Stoke City, wakati Oscar alifunga katika pambano dhidi ya Swansea na Mauro Zarate alikuwa mfungaji wa bao la pili la West Ham dhidi ya Arsenal. Mshambuliaji wa kimataifa wa Mexico, Miguel Layun aliifungia Watford na huyo alikuwa mchezaji pekee kutoka eneo la Amerika Kaskazini na kati kufunga bao.
Kulikuwa na mabao mawili ya kujifunga. Ni wachezaji sita tu wa Uingereza ambao walifanikiwa kuziona nyavu. Hao ni Ross Barkley, Jermaine Defoe, Jamie Vardy, Marc Albrighton, Nathan Redmond na Wilfried Zaha.