Vijeba wazua jambo AFCON U17
Muktasari:
- Kocha wa Morocco, Pedro Goncalves licha ya kutonyooshea kidole moja kwa moja suala la umri, alitoa kauli inayoonyesha wasiwasi wa uwepo wa wachezaji wenye umri mkubwa.
LICHA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumia vipimo vya MRI, ili kuthibitisha umri wa wachezaji kwenye Fainali za Afrika (AFCON U17), wasiwasi wa kutumika kwa wachezaji waliozidi umri kwenye mashindano hayo umeibuka.
Pamoja na kipimo hicho cha MRI kuwapitisha, maumbile ya baadhi ya wachezaji yameonekana kuleta hisia kuwa wana umri mkubwa kuzidi ule halisi wa chini ya miaka 17.
Hilo limepelekea baadhi ya makocha wa timu zinazoshiriki mashindano hayo kuonyesha wasiwasi kuwa huenda kipimo hicho sio suluhisho sahihi la kudhibiti upandikizaji wa vijeba mashindanoni.
“Kiukweli hili jambo linatia shaka na inafika wakati mtu unaweza kujiuliza kwamba ni kweli mchezaji husika ana umri wa miaka 17 au la kwa sababu muonekeno na umbile lake havisadifu kuwa ni mdogo na kama unavyofahamu sio rahisi kwa mchezaji mdogo kumudu ushindani wa mtu mkubwa,” Kocha wa Serengeti, Oscar Mirambo alisema na kuongeza;
“Unapata shaka na vipimo, lakini kuna wakati unakuwa hauna jinsi. Kama inafikia hatua wachezaji wawili mapacha ambao wamezaliwa wakati mmoja, kipimo kinaonyesha kuwa mmoja ana umri mkubwa na mwingine ana umri mdogo, inaleta wasiwasi.”
Kocha wa Morocco, Pedro Goncalves licha ya kutonyooshea kidole moja kwa moja suala la umri, alitoa kauli inayoonyesha wasiwasi wa uwepo wa wachezaji wenye umri mkubwa.
“Mashindano haya ni mazuri kwa sababu yana kundi kubwa la wachezaji waliopevuka kulinganisha na mashindano mengine ya vijana wa umri kama huu,” alisema Goncalves.
Naye kocha wa Cameroon, Thomas Libih alisema kuwa kipimo cha MRI kimekuwa kikitoa majibu ya kushangaza jambo ambalo linatia shaka.
“Ni jambo linaloleta ukakasi kidogo lakini hatuna namna ya kupingana nalo kwa sababu ndiyo utaratibu uko hivyo. Kuna wakati vipimo viliwahi kuonyesha wachezaji wawili ambao ni mtu na mdogo wake, yule kaka mtu hana tatizo lakini yule mdogo mtu akafeli na vikaonyesha kuwa ni mkubwa,” alisema Libih.
Kabla ya kuanza kwa fainali za Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 zinazofanyika hapa nchini, wachezaji sita wa timu tofauti walienguliwa kwenye vikosi vyao kutokana na kuonekana wana umri mkubwa zaidi ya miaka 17.
Wachezaji hao sita ni watatu kutoka Cameroon, wawili kutoka Tanzania na mmoja kutoka Guinea ambaye hata hivyo alifariki dunia kwa ajali muda mfupi baada ya kutua nchini mwao akitokea Tanzania.