Vijana yalipiza kisasi kwa Pazi, JKT hoi NBL

Dar es Salaam. Wakati timu ya Vijana ‘City Bulls’ ikifanikiwa kulipaza kisasi kwa Pazi, mambo yamezidi kuwaendea kombo mabingwa watetezi wa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL), JKT, baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo.

Vijana ambayo ilifungwa pointi 54-48 na Pazi katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), ilibadili kibao katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Don Bosco, Upanga, Dar es Salaam na kushinda kwa pointi 82-63, huku JKT ikichapwa na Kurasini Heat kwa 65-62.

Kocha wa Vijana, Ashraf Haroun alisema pamoja na ushindi walioupata kulinganisha na ule wa Pazi dhidi yao, bado timu hizo zilionyeshana ushindani mkubwa.

Haroun alisema walijiandaa vizuri kuikabili Pazi ambayo kwa sasa imeanza kurejesha makali katika mchezo wa kikapu.

Alisema waliusoma mchezo wa kwanza waliofungwa na Pazi na kubaini eneo walilokosea, kisha wakaweka mkakati wa kuzikabili mbinu za wapinzani wao.

“Tulianza kuwabana wachezaji wao nyota na kuhakikisha kuwa hawapati mwanya wa kucheza na hata kama watapata nafasi basi kwa upande wao, mbinu hiyo iliwasumbua wapinzani wetu na kujikuta wakipoteza mipira mingi,” alisema Haroun.

“Kwa upande wetu, tuliamua kucheza kwa umakini na kutumia kila nafasi tuliyoipata kwa faida na kufanikiwa kuibuka na ushindi mnono, nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi huu mkubwa ambapo sasa tunahitaji kushinda mechi moja ili kuingia hatua ya robo fainali.”

Kwa ushindi huo, Vijana inaongoza kwa kuwa na pointi nne ikiwa imeshinda mechi mbili na kufuatiwa na Ukonga Kings, Pazi na Dodoma Panthers.

Katika mchezo mwingine, Kurasini Heat iliendeleza ubabe dhidi ya JKT baada ya kuichapa kwa pointi 65-62 katika mchezo mkali.

Huo ni ushindi wa nne kwa timu ya Kurasini Heat ambao ni mabingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mchezo huo.

Kocha wa Kurasini Heat, Shendu Mwagalla alisema ushindi huo ni faraja kwao kwani wameweka nia ya kutwaa ubingwa wa Taifa.

Hatima ya JKT kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo itategemea na taratibu za waandaaji katika kundi hilo lenye timu tatu, huku Kurasini Heat na Oilers zikiwa zimefuzu hatua hiyo.

“Tunataka kuweka historia katika mchezo wa kikapu kwa kutwaa ubingwa wa Taifa (NBL). Nawapongeza wachezaji wangu kwa kupambana muda wote na kufanikiwa kushinda mechi ambayo ilikuwa na kila aina ya ushindani,” alisema Mwagalla.

Kocha wa JKT, Chriss Webber alisema kuwa walipoteza mechi hiyo kiufundi, lakini bado timu yao ni ngumu na yenye kuleta ushindani inapokuwa inacheza.

“Hatima yetu kama tutaingia robo fainali kutegemeana na matokeo ya timu nyingine, sisi tuna magoli sita ya faida, tusubiri waandaaji watafanyaje ili kupata timu nane katika makundi matatu ya mashindano,” alisema Webba.

Katika mechi nyingine Ukonga Kings iliifunga Dodoma Panthers pointi 68-63 na kwa upande wa wanawake, JKT Stars iliicharaza Jeshi Stars kwa pointi 82-41.