VIDEO: Siri nyuma ya penzi la Galis, Masogange

Muktasari:

  • Hata hivyo, kwenye shughuli nzima ya msiba wa staa huyo, kuna mtu mmoja alikuwa mstari wa mbele na hata wakati wa kuaga mwili wa Masogange pale Leaders alipoteza fahamu na kusaidiwa na wasanii wenzake. 

NI siku 23 sasa zimekatika tangu tasnia ya burudani nchini ilipompoteza video Queen, Agnes Gerald ‘Masogange’ aliyefariki wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mama Ngoma, Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwenye shughuli nzima ya msiba wa staa huyo, kuna mtu mmoja alikuwa mstari wa mbele na hata wakati wa kuaga mwili wa Masogange pale Leaders alipoteza fahamu na kusaidiwa na wasanii wenzake.

Huyu ni msanii nyota wa Bongo Movie, Rammy Galis, na baada ya tukio hilo mengi yalizungumzwa huku baadhi wakienda mbali zaidi kwa kudai kuwa, staa huyo alikuwa akijaribu kutengeneza kiki. Hata hivyo, Galis ambaye alikuwa mpenzi na mtu wa karibu wa Masogange, aliweka bayana kuwa hakuzimia bali aliishiwa nguvu na kila kitu kilichokuwa kinaendelea alikisikia vizuri.

Lakini, hiyo ya kudaiwa kutengeneza kiki sio ishu kabisa na kama vipi achana nayo, Galis amechonga na Mwanaspoti na kufichua mambo kibao aliyoyafanya akiwa na Masogange wakati wa uhai wake.

Kwanza ifahamike kwamba, Galia na Masogange walikuwa wapenzi wa kupika na kupakua na kwamba, msiba huo ulikuwa kama mkuki ndani ya moyo wake japo walikuwa wameachana kwa wakati huo. Huyu hapa Galis anafunguka kila kitu.

Walikutana wapi na Masogange

Anafichua kuwa kwa mara ya kwanza walikutana na Msogange mwaka 2015 wakiwa Uwanja wa Ndege wa Abuja, Nigeria alipokwenda kwa shughuli zake za filamu.

Wakiwa uwanjani hapo walizungumza mengi na kubadilisha mawasiliano ambapo, kukutana kwao huko ndiko kulikofungua mahusiano na kujikuta wamezama kwenye mapenzi. Kutokana na uhusiano wao kuwa motomoto walitafuta nyumba pamoja, ambapo mpaka Masogange anafikwa na umauti alikuwa akiendelea kuishi kwenye nyumba hiyo.

“Mimi ndio nilitafuta ile nyumba na kulipia kodi ili kutufanya kuwa huru kabisa kwenye mapenzi yetu, lakini baadaye tuliposhindwa nikamuacha pale kila mmoja akaendelea na maisha yake.”

Masogange ana heshima bana

Galia anafichua kuwa, jamii haikuwa ikimwelewa Masogange, lakini ni msichana mwenye heshima na aliyekuwa akijitambua. Anasema kuwa Masogange alikuwa anafahamu mwanaume anataka nini na alikuwa mahiri wa kulinda mwanaume asichepuke.

“Yaani mlivyokuwa mnamuona Masogange nje sivyo alivyokuwa ndani, ni mtu aliyekuwa anajua nini mwanaume anataka, pia alikuwa ana heshima ya aina yake. “Alinibadilisha mambo mengi sana ikiwemo kunilinda na kuniweka mbali na makundi ya marafiki wasio na tabia njema,” Galis anasema.

Galis anakiri kuwa Masogange hakuwa mwanamke anayezoeleka kutokana na mvuto wake na alikuwa akiwavutia wanaume wengi, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwake.

Miezi sita bila mpenzi

Mpaka Masogange anafariki alikuwa na urafiki wa kawaida tu na Galis kwani, walishatemana muda mrefu hivyo, kujikuta kwenye wakati mgumu wa kuanzisha uhusiano mpya.

Anafichua kuwa baada ya kuachana na Masogange hakuwa kwenye hali ya kawaida na kwamba, ilimchukua miezi sita kuanzisha uhusiano mpya.

“Sikuona mrembo ambaye anaweza kuziba nafasi yake kwa haraka, lakini ndio hivyo kama mwanaume hawezi kukaa bila mtu.

“Tulikuwa karibu sana na tukafanya vitu vingi pamoja na kuanza kuandaa filamu ‘Hukumu ya Kifo’. Lengo la kuandaa filamu hiyo ilikuwa ni kuweka kumbukumbu hata kwa watoto wetu kwamba, tulipendana na kufanya kitu kwa ajili ya ukumbusho,” anasema. Hata hivyo anasema anasikitika filamu hiyo ikiwa inakaribia kutoka Masogange hataweza kuishuhudia ukizingatia ndio kazi yake ya kwanza kwenye upande wa filamu.

“Yaani hii filamu ndiyo ilikuwa imtambulishe Masogange anafaa kwenye video queen au kwenye filamu, lakini nasikitika hatoweza kuishuhudia wala kusikia maoni ya watu juu yake.”

Anasema pamoja na kwamba Msogange alikuwa mtu maarufu, binafsi hakupenda kuwa na mahusiano na mtu maarufu kwani, inakufanya uwe midomoni mwa watu mara kwa mara.

Vipi kuhusu ‘mtoto wao’

Galis anasema anatarajia kuizindua hiyo baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Dar es Salaam na Mbeya ambako alizaliwa Masogange na sehemu ya mapato yatakayopatikana atapewa mtoto wake.

Ili kuepuka kuleta maneno baadaye, Galis anasema atakaa na pande mbili za familia inayomlea mtoto wa Masogange na kuangalia namna gani ya lifanikisha hilo.