VAR: Utata bao la Phiri kwa Dodoma Jiji

GWIJI wa Arsenal, Thierry Henry amesema matumizi ya teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (VAR) yanaua hamasa ya asili ya soka duniani.

Henry ambaye alishinda Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa na Timu ya Taifa ya Ufaransa alisema hana tatizo na teknolojia hiyo, lakini amemchanganya zaidi na kasi ya marejeo ya matukio ya uwanjani kulinganisha na michezo mingine.

Henry mwenye rekodi ya ufungaji Arsenal, alisema anaamini VAR inasabisha malalamiko mengi mbali na kuibua hoja za kimaamuzi zinazofanywa na waamuzi wakati wa mechi.

“Katika soka, bado tupo nyuma, tuna mambo mengi ya kujifunza.

Ninachokiona katika mpira wa miguu wa Marekani, raga, kriketi, tenisi na michezo mingine ni tofauti na kinachoendelea katika soka,” alisema Henry.

Henry, Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Ubeligiji alisema maamuzi ya VAR yana ukakasi kwani hayatoki haraka.

“Ni wazi kuwa maamuzi ya VAR ni ya mtu au watu ambao wapo kwenye chumba maalumu uwanjani au sehemu nyingine wakiangalia mechi. Siyo VAR inayotoa majibu yenyewe, kwa hiyo bado kuna tatizo,” alisema.

Alifafanua kitendo cha VAR kusimamisha sherehe ya kushangilia bao kusubiri uamuzi wa mtu au watu wengine waliopo kwenye chumba maalumu kutoa maamuzi ya tukio husika.

“Tunachotaka kuona ni mechi kuendelea na hamasa ya mashabiki iendelee, siyo kukatizwa na maamuzi ya waamuzi waliopo kwenye chumba maalumu.

Wakati nacheza mpira wa ushindani, nilikuwa nafunga goli na kushangilia kwa kuruka juu, lakini kwa sasa ni vigumu kwani unahitaji kushangilia mara baada ya maamuzi ya VAR na hakuna mwendelezo wa furaha.

Unaweza kushangilia na baadaye VAR ikatakaa bao uliolofunga, hamasa imepotea kabisa,” alisema.


SIMBA VS DODOMA JIJI FC

Jumapili jioni, mashabiki wa soka walishuhudia timu ya Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, mchezo ambao ulichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ukiacha bao la kujifunga la Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na bao la tatu la Habib Kyombo, bao la pili la Simba lililofungwa na Moses Phiri limezua hoja nyingi miongoni mwa wadau wa soka huku wengine wakisema ni bao halali na wengine wakisema si halali.


ILIVYOKUWA

Wakati Phiri anapiga shuti, Bocco alikuwa katika eneo la kuotea na mbali ya kuzidi, aliuruka mpira uliopigwa na Phiri kumfanya Kipa wa Dodoma Jiji FC, Aaron Kalambo kushindwa kuona mpira huo kutinga wavuni.


TUANGALIE SHERIA

Sheria ya kuotea namba 11 ya mpira wa miguu inahusika katika tukio hili.

Sheria hiyo inavipengele vingi sana ambavyo mpaka sasa tafsiri yake imekuwa na utata mkubwa na kuendelea kuwa miongoni mwa sheria ambazo maamuzi yake hayana utatuzi maalumu.

Kwa kifupi, kitendo cha kuotea kwa mchezaji si kosa, ila kuna vipengele kadhaa ambavyo vinamfanya aadhibiwe kwa kuwa ni kosa la kunufaika na mchezo. Moja ya kitendo ambacho kitamfanya asiadhibiwe ni kutojihusisha na mpira au mchezo moja kwa moja.

Katika tukio la Bocco linafanana na tukio la Ligi Kuu ya England msimu uliopita ambapo mchezaji wa Arsenal, Eddie Nketiah ambaye alimziba kipa wa Manchester United, David de Gea.

Hata hivyo, mwamuzi alitumia kigezo cha umbali aliokuwepo kati ya Nketiah na De Gea na kubaini kuwa kipa huyo haukuathiri uwezo wa kuona wa kipa wa Manchester United na kulikubali kuwa bao halali. Bado hapo alifanya kosa.

Tukio hili pia linafanana na like la bao la Simba dhidi ya RS Berkane lillofungwa na Pape Ousmane Sakho ambapo wakati anapiga shuti, Meddie Kagere ambaye alikuwa mbele ya kipa wa RS Berkane, aliuruka mpira na kuzua utata pamoja na kuwa na makosa ya kibinadamu ya mwamuzi.

Inaonekana wazi kabisa sheria namba 11 ya kuotea bado ni tatizo kwa waamuzi na hata baada ya kuanza kutumika kwa VAR. Wengi wanasema kuwa VAR haijatatua tatizo hilo na hii wengi wanasema inatokana zaidi na ‘maoni’ ya mwamuzi ambao pia ni ‘binadamu’. Ni wazi kuwa Bocco alikuwa amezidi pamoja na mwamuzi kuwapa bao Simba kwasababu kipa aliuona mpira, ndio maana akajaribu kuuzuia na Bocco hakuathiri uwezo wa kipa huyo kushindwa kuuona mpira.