UTATU TISHIO : Hawakuachi salama, usiombe ukutane nao

Muktasari:
- Mwanaspoti inakuletea orodha ya baadhi ya mastraika tishio waliotengeneza utatu ambao hata mabeki wanajua wanavaana nao hubadili mbinu zao za kuwakaba ili wasiwaaibishe wao na makipa wao. Jamaa wanajua kufunga mpaka wanaudhi unaambiwa.
RAHA ya mechi bao, asikwambie mtu. Soka safi inahusisha mambo mengi ukianza na ufundi, burudani, mbwembwe na mambo kibao, yote tisa kumi, soka safi bila mabao, ni kazi bure!
Kocha yeyote yule mwenye kiu ya mafanikio katika soka la sasa, ana ndoto ya kupata kombinesheni nzuri yenye uwezo wa kufumania nyavu wakati wote na katika nafasi yoyote ile.
Katika Ligi Kuu Bara kuna safu matata ya kufumania nyavu achana na zile pacha tishio, kuna utatu matata ambao ukikutana nao kwenye mechi na kama hujajipanga ni lazima wakuumize kwa jinsi wanavyotupia tu kambani.
Mwanaspoti inakuletea orodha ya baadhi ya mastraika tishio waliotengeneza utatu ambao hata mabeki wanajua wanavaana nao hubadili mbinu zao za kuwakaba ili wasiwaaibishe wao na makipa wao. Jamaa wanajua kufunga mpaka wanaudhi unaambiwa.
MAKAMBO, AJIBU, TAMBWE-YANGA
Mkongomani, Heritier Makambo ndiye mfalme wa safu ya ushambuliaji wa kikosi cha Yanga hadi sasa, kwani ametupia mabao tisa katika mechi 17 ambayo timu yake imecheza mpaka sasa, akishirikiana na nyota wenzake, Mrundi Amissi Tambwe na Ibrahim Ajibu ‘Kadabra’.
Hii ndio safu kali kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, kwani utatu wao umezalisha jumla ya mabao 19 ambayo ni zaidi ya nusu ya mabao yote yaliyofungwa na Yanga iliyopo kileleni ikiongoza Ligi Kuu ikiwa na alama 47. Yanga ndio timu yenye mabao mengi ikifunga 33.
Tambwe na Ajibu kila mmoja amefunga mabao matano, idadi hiyo wanaonyesha kuna uelewano mkubwa zaidi kwa nyota hao kwani sehemu kubwa ya mabao ya Yanga msimu huu yametengenezwa na Ajibu, mbali na yeye mwenyewe kutupia kimiani.
Pamoja na Tambwe kutokuwa na nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Mwinyi Zahera kutokana na mara nyingi kuingia akitokea benchi lakini ameonyesha kuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani kwani kila akiingia basi ni lazima afunge.
KAGERE, OKWI, BOCCO- SIMBA
Hii ndio safu iliyokuwa ikitajwa kuwa tishio katika Ligi Kuu Bara msimu huu, kutokana na kujaa watu wanaojua kucheka na nyavu.
Utatu huu katika mechi 13 iliyocheza timu yao ya Simba tayari wameshazalisha jumla ya mabao 16, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi kila mmoja ana mabao saba, huku John Bocco aliyemaliza nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya Okwi akiwa na mabao 14 amefunga mawili.
Wakali hao wamefunga zaidi ya nusu ya mabao ya timu yao, kwani katika mechi 13 walizocheza, Simba imetupia nyavuni mara 25 na kukusanya alama 30 ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam zilizopo juu yake katika msimamo.
Kasi yao inaweza kuwafunika wengine mara baada ya kumaliza majukumu yao ya kimataifa ambao nako wanakiwasha kinoma ambao jioni ya jana walikuwa wakimalizana na Nkana FC.
AMBOKILE, SELEMAN, MAPUNDA-MBEYA CITY
Mbeya City ya msimu huu imekuwa tishio katika kufumania nyavu ikishika nafasi ya nne kati ya timu zinazojua kutupia kambani, ikifunga mabao 20, japo imekuwa na ukuta dhaifu ulioruhusu idadi kama hiyo ya mabao.
Hata hivyo utatu wao unaoongozwa na Eliud Ambokile aliyewakimbiza kwa muda mrefu wafungaji wenzake akiongoza orodha kabla ya kunaswa na Makambo na Said Dilunga na Ruvu Shooting ni tishio.
Ambokile anashirikiana na Idd Seleman ‘Nado’ na mkongwe Peter Mapunda ambao jumla yao wamezalisha mabao 15, Nado akifunga manne na Mapunda mawili katika mechi 17 ilioyocheza timu yao iliyokusanya alama 23 na kushika nafasi ya saba.
KUTINYU, NGOMA, ZAYD- AZAM
Tofauti ya msimu uliopita, Azam ya Hans Pluijm imeonekana kuwa moto ikiwa haina mfungaji mmoja lakini wana utatu wao matata ukiongozwa na Wazimbabwe, Tafadzwa Kutinyu na Donald Ngoma wakipigwa chapuo na Yahya Zayd.
Ukiangalia idadi ya mechi walizocheza Azam (16), timu hii imefunga mabao 26 ikiizidi Simba, lakini watatu hao wanachuana wenyewe na nyota wao wengine kikosini.
Zayd na Kutinyu kila mmoja amefunga mabao matano huku Ngoma aliyerejea uwanjani kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu akitumia kambani mabao manne na kufanya utatu huo kuzalisha jumla ya mabao 14 mpaka sasa katika Ligi yenye jumla ya michezo 380.
DILUNGA, VIALLI, SAID-RUVU SHOOTING
Ni kweli Ruvu Shooting hawapo katika nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu Bara, lakini hiyo haijaifanyab timu hii kuwa tishio kwa wapinzani wao kutokana na kuwa na utatu mkali wa kutupia ukiongozwa na Said Dilunga ambaye msimu huu amekuwa moto mkali.
Safu hii imefunga jumla ya mabao 13, kwani Dilunga anayekabana na kina Makambo na Ambokile kwenye kilele cha orodha ya wafungaji akiwa na mabao yake 9, huku Mcha Khamis ‘Vialli’ na Mussa Said kila mmoja ametupia nyavuni mara mbili.
Ruvu licha ya kushika nafasi ya 15 katika msimamo lakini ni kati ya timu mbili zinazoshika nafasi ya sita kwa kufunga mabao mengi ikiwa na 17 kama Stand United, lakini utatu wao matata umechangia sehemu kubwa ya mabao hayo ni mabao manne tu yamechangiwa na wengine.
KHAMIS, ATHANAS, MUJWAHUKI-MBAO
Utatu mwingine ambao ni tishio katika Ligi Kuu Bara ni huu wa Mbao FC iliyokuwa chini ya Kocha Amri Said ‘Jaap Stam’, anayetajwa kuwindwa na Msimbazi ili kwenda kumsaidia Mbelegiji, Patrick Aussems.
Said Khamis, mwenye mabao sita, Pastory Athanas mwenye mabao mawili na Evaligestus Mujwahukimwenye mabao matatu ni noma sana. Ukikutana nao hawakuachi kwani hata Simba wanaijua baada ya kuizima CCM Kirumba na kuwatibulia mapema msimu huu.
Mastraika hao wametupia kambani jumla ya mabao 11 katika mechi 17 walizocheza, ikiwa na maana mabao karibu yote ya Mbao iliyofunga 12 yamefungwa na nyota hao watatu pekee na kuiacha timu yao katika nafasi ya nne.
KMC NAO WAMO
KMC nayo ni moja ya timu yenye utatu matata mkali kwani Emmanuel Mvuyekure, James Msuva na Omar Issa Ramadhani wameibeba timu yao inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu.