Prime
Utabiri wa Okwi na maajabu ya miguu ya Okello
KATIKA mechi sita za mwisho za Yanga za Ligi Kuu Bara, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Allan Okello raia wa Uganda amekuwa na kiwango cha juu kilichowaibua makocha na mastaa kumzungumzia.
Okello aliyezaliwa Julai 4, 2000 akiwa na umri wa miaka 25, alijiunga na Yanga msimu huu akitokea Vipers ya Uganda, katika mechi sita za mwisho amehusika na mabao 11 akifunga manne na kutoa asisti saba, kitu ambacho kimewavutia wengi na kuona klabu hiyo haikukosea kumvuta Jwangani.
Mechi ambazo Okello alifunga na kutoa asisti ni dhidi ya Coastal Union (mabao 2, asisti 1), KMC (bao 1), Simba, Mbeya City (asisti 2), Pamba Jiji (asisti 3) na Tanzania Prisons (bao 1, asisti 1). Kabla ya hapo alifunga bao moja dhidi ya Singida Black Stars (Machi 5).
Kwa ujumla tangu Okello ajiunge na Yanga Januari 2026, amecheza mechi 15 za Ligi Kuu Bara akihusika na mabao 12, akifunga matano na asisti saba.
Kutokana na kiwango chake, aliyekuwa nyota wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda alimtaka nyota huyo kujituma na kuzidisha nidhamu akiamini ana muda mwingi wa kufanya vitu vikubwa.
“Ana mwanzo mzuri, ajitahidi kuwa na muendelezo na kuzingatia vitu gani vinatakiwa katika mpira wa miguu, atafanya makubwa zaidi, kwani umri wake bado unamruhusu,” amesema Okwi ambaye pia aliitumikia Yanga msimu wa 2013–2014.
Staa mwingine ambaye ni raia wa Uganda, Khalid Aucho anayeitumikia Singida BS msimu huu akitokea Yanga, amesema: “Okello ana kipaji kikubwa, aendelee kujituma zaidi ya hapo, naamini atafanya mambo makubwa.”
Okello ambaye saini yake ilikuwa inawaniwa na Simba lakini Yanga iliipiga bao, huduma yake iliwahi kutakiwa na Mamelod Sundowns kipindi kocha akiwa Pitso Mosimane.
Mosimane amesema: “Nilikuwa namfuatilia Okello, nilimtaka kweli lakini alikuwa bado ni mdogo sana, angehitaji muda mwingi zaidi, sikutaka nimchukue halafu asicheze.”
Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moalin, amesema: “Kuhusu Okello ana talenti kubwa, jukumu letu kama benchi la ufundi kupata kilicho bora kwa kila mchezaji, siyo Okello pekee.”
Kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Paul Put hayupo nyuma kumfuatilia anachofanya nyota huyo, alikuwa na haya ya kusema: “Nafurahishwa na kiwango chake, akitumika kama namba 10 akicheza kwa uhuru atafanya vitu vikubwa zaidi.”
Okello akiwa na timu ya taifa ya Uganda, katika mechi 10 za mwisho ametoa asisti nne na kufunga mabao mawili, jambo ambalo kocha huyo amesema siyo kiwango kibaya.