Usajili umewatoa nishai kweli

Jonas Mkude
Muktasari:
Usajili mpya uliofanyika kuimarisha timu zao unataka kuwatoa nishai. Heshima zao ndani ya timu wanazocheza huenda zikashuka kwa kiasi kikubwa. Msimu huu mpya unaweza kuwa wa changamoto zaidi kwao.
KUNA baadhi ya mastaa wa timu za Ligi Kuu sasa matumbo yao yanawaka moto. Hawaamini kabisa kinachotokea katika maisha yao ya soka.
Usajili mpya uliofanyika kuimarisha timu zao unataka kuwatoa nishai. Heshima zao ndani ya timu wanazocheza huenda zikashuka kwa kiasi kikubwa. Msimu huu mpya unaweza kuwa wa changamoto zaidi kwao.
Makala haya yanakuletea orodha ya mastaa ambao usajili mpya wa wachezaji uliofanyika katika timu zao unawatoa jasho. Wanahaha kwelikweli kupigania nafasi zao.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Yanga
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ haamini kinachoenda kumtokea kwa sasa klabuni hapo. Alikuwa amejenga makazi katika kikosi cha kwanza cha Yanga kwa miaka kadhaa, lakini makazi hayo yanaonekana kutaka kubomoka.
Usajili wa beki, Vincent Bossou kutoka Togo unaanza kumhenyesha Cannavaro pale Yanga. Nafasi yake katika kikosi cha Yanga inayumba vilivyo kwa sasa. Ni jambo gumu kuamini kama Cannavaro atapata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Kocha Hans Pluijm kwa sasa.
Elius Maguli, Simba
Simba ilifanya usajili wa nyota wake wa zamani Mussa Hassan ‘Mgosi’ kisha ikatulia. Wiki chache baadaye ikamleta Hamis Kiiza ‘Diego’ kutoka Uganda kisha ikatulia tena. Wiki chache baadaye ikampandisha chipukizi Boniface Maganga kisha ikatulia. Siku chache baadaye ikawaleta Kevin Ndayisenga kutoka Burundi na Danny Lyanga aliyeicheza FC Lupopo ya DR Congo.
Hapa hali ikawa mbaya kwa straika Elius Maguli. Usajili huu ukamfanya aachwe katika kikosi cha wachezaji 22 waliocheza siku ya Simba Day. Usajili huu umemfanya kocha mkuu wa timu hiyo Dylan Kerr kupendekeza straika huyo atolewe kwa mkopo. Hakika usajili huu umemtoa nishai.
Saimon Msuva, Yanga
Mshambuliaji Saimon Msuva ni mfungaji bora na mchezaji bora wa msimu uliopita, lakini usajili uliofanyika Yanga umemtoa nishai. Msuva licha ya kuwa nyota muhimu katika kikosi cha Yanga msimu uliopita bado hana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha msimu huu.
Usajili wa Geofrey Mwashiuya umeonekana kuiyumbisha kidogo nafasi ya Msuva. Uwezo binafsi wa kinda huyo unamtetemesha Msuva na inabidi apambane vilivyo kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Jonas Mkude, Simba
Haonekani kutishika sana ila ni ukweli usiopingika kwamba usajili wa kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi unamweka tumbo joto. Majabvi anaonekana kuimarika siku hadi siku na huenda akiwa fiti kwa asilimia 100 akatikisa Simba.
Mkude anaweza asikubali kwa kinywa chake, lakini usajili wa Majabvi unamweka tumbo joto kupata nafasi katika kikosi cha kwanza hasa kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda sasa akiuguza majeraha.
Oscar Joshua, Yanga
Beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua ‘OJ’ naye ameonja joto ya jiwe la usajili mpya. Tayari ameanza kusugua benchi Yanga na nafasi yake imekwenda kwa Mwinyi Haji Mngwali, aliyesajiliwa kutokea KMKM ya Zanzibar. Oscar kwa sasa ana changamoto kubwa ya kudhihirisha ubora wake mbele ya Mwinyi na akishindwa benchi litamhusu zaidi.
Didier Kavumbagu, Azam
Straika wa Azam, Didier Kavumbagu naye usajili uliofanywa na timu yake huenda ukamtoa nishai. Kavumbagu licha ya kuwa mfungaji bora wa Azam msimu uliopita, kwa sasa anakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhihirisha ubora wake mbele ya kocha mpya Stewart Hall.
Usajili wa Allan Wanga na kurejea kwa makali ya John Bocco vinamtoa nishai Kavumbagu pale Azam. Ujio wa kinda, Farid Mussa nao unaibua changamoto kubwa zaidi.
Kipre Bolou, Azam
Kiungo wa Azam, Kipre Bolou naye anatarajiwa kuonja joto ya jiwe ya usajili mpya. Ujio wa Jean Mugiraneza ‘Migi’ unaonekana kuibua changamoto mpya Azam. Bolou kwa sasa bado hajawa fiti kwa asilimia 100 baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha, hivyo kujiweka katika hali ya wasiwasi wa kutetea nafasi yake.
Ubora wa Migi ni changamoto kwake. Anatakiwa kurejea katika ubora wake wa awali kama kweli anahitaji kuendelea kucheza katika kikosi cha kwanza. Hall atalazimika kuwatumia viungo hao wawili kwa pamoja pia kama anahitaji huduma zao.
Andrey Coutinho, Yanga
Mbrazili wa Yanga, Andrey Coutinho naye ana wakati mgumu Yanga. Usajili wa Deus Kaseke unaonekana kumtoa nishai. Nafasi ya Coutinho katika kikosi cha kwanza cha Yanga haitabiriki tena. Kaseke anapewa nafasi kubwa zaidi kwa sasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchangamsha mchezo.
Bahati nzuri ni kwamba baadhi ya viongozi wanampigania aendelee kupewa nafasi ya mwisho na Kocha Pluijm, hata hivyo bado kazi anayo msimu huu.