Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UOZO : Mdudu anavyolitafuna soka la Tanga

Wachezaji wa Mgambo .

Muktasari:

Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Coastal Union bado wanashiriki ligi hiyo lakini hali yao si nzuri. Timu hiyo inatafunwa na mambo madogo madogo ya chini chini ambayo kama hayatafanyiwa kazi, basi itakuwa ni vigumu timu hiyo kushindania ubingwa tena kama ilivyofanya miaka ya nyuma.

HALI  ya soka la Tanga ni tete, tena siyo kitoto. Licha ya uwepo wa timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu kutoka jijini hapa, bado hali ya soka si nzuri kwani timu hizo zimekosa ushindani na hamasa ya kutosha kama zamani.

Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Coastal Union bado wanashiriki ligi hiyo lakini hali yao si nzuri. Timu hiyo inatafunwa na mambo madogo madogo ya chini chini ambayo kama hayatafanyiwa kazi, basi itakuwa ni vigumu timu hiyo kushindania ubingwa tena kama ilivyofanya miaka ya nyuma.

African Sports ambayo iliwahi kutwaa ubingwa wa Muungano mwaka 1988, imepanda kushiriki Ligi Kuu kwa msimu huu baada ya kushuka kwa zaidi ya miaka 20. Timu hiyo inaonekana pia kukumbwa na matatizo madogo madogo ya ndani ambayo kama hayatafanyiwa kazi pia inaweza kushuka tena ama kusalia katika nafasi za mkiani mwa ligi.

Mgambo JKT ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa nne sasa, inaonekana kuwa na hali ngumu zaidi kutokana na kukosa sapoti ya kutosha kutoka kwa wamiliki wake ambao ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mgambo kama haitashuka, basi itabaki katika nafasi za mkiani mwa ligi. Mwanaspoti ambalo liliweka kambi kwa wiki nzima mkoani hapa limefanya uchunguzi wa kina ili kufahamu mambo ambayo yanazorotesha soka la Tanga na kuzifanya timu za jiji hilo kushindwa kushindania ubingwa wa Ligi Kuu licha ya uwepo wa timu tatu tofauti.

Hata hivyo, kutokana na unyeti wa habari hii, wadau wengi wanaozungumza wanaomba hifadhi ya majina yao, hivyo majina yatakayotumika katika makala haya siyo majina halisi.

Jambo unalotakiwa kufahamu ni kwamba viongozi kadhaa wa soka jijini hapa wana nongwa na tabia ya kuweka visasi, hivyo wadau hawa wameomba kupewa hifadhi ili kujiondoa katika migogoro hiyo.

Uvamizi katika uongozi

Tatizo kubwa ambalo linazikumba timu za Tanga ni kuwa na viongozi ambao si watu wa mpira. Hamis Juma ambaye ndiye mpasha habari wetu mkuu anasema Coastal Union na African Sports zote zina tatizo, hilo jambo ambalo linazifanya zishindwe kuwa washindani.

“Timu zimevamiwa na watu ambao hawajawahi kuwa katika mpira, itazame Coastal Union, makamu mwenyekiti pekee ndiye mtu wa mpira lakini hawa wengine hawafahamu lolote kuhusu mpira, hivyo kuwa tatizo.

“African Sports nayo ina tatizo kama hilo, Makamu Mwenyekiti, Abdul Bosnia ndiye mtu ambaye amekuwepo kwenye mpira hapo awali, wengine wote ni wageni, hapo inakuwa ni changamoto kubwa sana,” anasema Hamis.

Mpasha habari mwingine ambaye anapewa jina la Mohammed Juma anasema viongozi hao wamekuwa wakitazama mkwanja zaidi na wengine huenda mbali na kumpangia kocha kikosi.

“Kuna kiongozi mmoja wa hizi timu huwa anataka kufanya kila kitu mwenyewe, anaingilia hadi kazi za kocha, anataka kikosi apange yeye na kila kitu afanye yeye, hii inasababisha wachezaji wazuri wasicheze kwani yeye anapanga aliowasajili,” anasema.

Soka la vijana limeachwa

Naelezwa kuwa wakati timu ya Coastal inatamba miaka ya nyuma kulikuwa na timu tatu tofauti lakini sasa mambo yamebadilika na timu za Tanga hazina timu za vijana zinazoeleweka tena.

“Wakati Coastal Union inatamba miaka ya zamani ilikuwa na timu mbili za vijana, kulikuwa na timu inaitwa Coastal Kids na Coastal Heroes ambazo zilitoa wachezaji kwa ajili ya timu ya wakubwa.

“Mchezaji akifanya vizuri Coastal Kids anapanda kwenda Coastal Heroes hapo anakomazwa vizuri kwa ajili ya timu ya wakubwa, kulikuwa pia na timu iliyokuwa inaitwa Mwananchi ilikuwa inamilikiwa na Mahafudu ambayo ndiyo ilitoa wachezaji kwa timu hizo,” anasema Khamis Ali.

“African Sports na Coastal Union za sasa hazina timu za vijana, zimekusanya tu waliopo kwa kuwa ni kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lakini hakuna wachezaji hapo,” anaongeza

Mwanaspoti liliwashuhudia wachezaji wa timu ya vijana ya Coastal Union wakirandaranda nje ya Uwanja wa Mkwakwani kutaka kuingia uwanjani ili kucheza mechi ya utangulizi dhidi ya timu ya vijana ya African Sports wakati Simba ilipokwenda kucheza na Sports wikiendi iliyopita.

Vijana hao walishindwa kuingia uwanjani kutokana na kukosa kadi za utambulisho ambazo hutolewa na TFF jambo ambalo linaashiria kuwa viongozi wa timu hiyo ambao wote walisafiri kwenda Dar es Salaam kwenye mechi yao dhidi ya Yanga hawako makini.

Ukata

Wenyeji wangu wananiambia kuwa timu za African Sports na Coastal zina ukata mkubwa wa fedha ambao kwa namna moja ama nyingine umechagizwa na uzembe wa viongozi.

Mmoja wa wapasha habari hao ananiambia kuwa African Sports imepiga chini udhamini wa Sh150 milioni kutoka katika kampuni ya kutengeneza Chilli Source ya jijini hapa kwa madai kuwa kampuni hiyo itaweka nembo nyekundu katika jezi yao wakati wao hawafungamani na rangi hiyo.

“Wamepata udhamini hapa kutoka kiwanda cha Chilli lakini hawataki kuupitisha kwa kuwa ina rangi nyekundu, wamewataka wadhamini wabadili rangi ili wawatangaze jambo ambalo haliwezekani, ona sasa hawana udhamini wowote wa maana,” anasema.

Mpasha habari mwingine Miraji Athuman anasema Coastal wamejiweka wenyewe katika mazingira magumu ya kupata udhamini kutokana na masilahi binafsi katika uongozi na kwanza walipoteza udhamini wa kampuni kadhaa kabla ya kupata huo wa Kampuni ya Unga.

“Watu wengi wa kampuni za hapa Tanga wanaogopa kuzidhamini timu hizi kutokana na viongozi kutokuwa makini, we tazama timu hizi mbili zimefanya mikutano yao bila kuwa na ajenda ya mapato na matumizi, hapo wadhamini wataanzia wapi kutoa udhamini wao,” anasema.

“Ni lazima timu itoe taarifa ya namna ilivyotumia fedha ilizopata, hapo kunakuwa na uwazi, hivyo hata watu wenye nia ya kuzidhamini inapata moyo wa kufanya hivyo lakini hayo hapa Tanga ni mageni, klabu hazina uwazi huo.”

Migogoro isiyoisha

Timu za Tanga zinakumbwa na migogoro mingi ya ndani kwa ndani ambayo bila shaka inachangia kwa namna moja ama nyingi kurudisha nyuma soka la mkoa huo.

Mmoja wa wapasha habari anasema timu za African Sports na Coastal zote zina migogoro mbalimbali ambayo inasababisha timu hizo kutokuwa vizuri.

Miongoni mwa migogoro mikubwa ya klabu hizo iliyowahi kukaririwa ni pamoja na kufubazwa kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto mwaka jana bila sababu za msingi kabla ya baadaye TFF kuingilia kati na kutatua tatizo hilo. Migogoro mingine iliyozitikisa timu hizo ni pamoja na vurugu za uchaguzi wa klabu hizo mbili ambao uligubikwa na figisu figisu nyingi na kusababisha hata baadhi ya wanachama kuzisusia timu hizo.

“Uchaguzi wa African Sports haukuwa huru na wa haki, wanachama wengi walinyimwa haki yao, timu ilifanya uchaguzi na wanachama wachache na wengi walinyimwa kadi kwa hofu ya kutowachagua watu ambao walikuwa wamegawana madaraka.

“Nafasi nyingi zilikwenda bila pingamizi, watu walipata ushindi kabla hata ya siku ya kura, hapo soka haliwezi kuendelea kabisa,” anasema mpasha habari huyo.

Utata wa udhamini

Coastal Union iliwahi kudhaminiwa na Kampuni ya Saruji jijini hapa ambayo ilikuwa ikifanya malipo moja kwa moja kwa wachezaji, lakini yaliyokuja kugundulika baadaye yalikuwa ni ya uozo.

Mmoja wa wapasha habari hao anasema viongozi wa Coastal walipeleka akaunti feki ambazo hazikuwa za wachezaji ili waweze kupata mwanya wa kupiga mkwanja jambo ambalo lilikuja kufumuka baadaye.

“Ule udhamini wa Kampuni ya Saruji ulikuwa unafanyika kwa masharti na miongoni mwa masharti ilikuwa ni kufanya malipo ya mishahara ya wachezaji moja kwa moja, jambo ambalo viongozi waliona linazuia mianya yao ya kupiga mkwanja.

“Baadaye ilitokea Coastal inacheza na Simba na wachezaji wakagoma kwa madai kuwa hawajalipwa, Kampuni ya Saruji ilipofuatilia ilibaini kuwa fedha zilikuwa haziendi moja kwa moja kwa wachezaji hivyo ikaamua kujitoa,” anasema.

Mgambo nayo

Timu ya Mgambo JKT haiingii katika mkumbo wa African Sports na Coastal Union, lakini timu hiyo ina matatizo mengi pengine kuliko hata timu hizo mbili.

Kwanza Mgambo haina bajeti ya maana kwa ajili ya wachezaji pamoja na maandalizi ya timu jambo ambalo linaifanya timu hiyo kuendelea kushiriki Ligi Kuu kwa mazoea.

Wakati Mgambo inajiandaa kucheza na Simba ilikuwa ikifanya mazoezi katika uwanja ambao ni mchakavu na usipokuwa makini unaweza kufikiri ni shamba lililotelekezwa na siyo uwanja kwani hata kukimbia ni tatizo katika uwanja huo.

Mbali na hilo, wachezaji wa Mgambo walibeba maji yao ya kunywa katika ndoo na kuwa na kikombe kimoja ambacho kilitumiwa kunywea maji na wachezaji wote. Hiyo pekee ni kuonyesha namna wachezaji walivyo katika hatari ya kuambukizana magonjwa hatarishi bila wenyewe kujali.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alitetea matumizi hayo ya maji ya ndoo na kudai kuwa maji ya Jiji la Tanga ni safi na salama na ndiyo sababu hawaoni haja ya kutumia maji ya kununua.

“Maji ya hapa ni safi na salama, tunakunywa hayo hayo nyumbani kwetu, hivyo hatuoni haja ya kununua maji, tumekuwa tukifanya hivyo kwa miaka yote,” anasema Shime.

Katibu wa FA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Soka jijini Tanga (TRFA), Beatrice Mgaya anakiri kuwepo kwa matatizo mbalimbali yanayolikumba soka la Tanga na chama chao kimekuwa kikifanya jitihada za kuyatatua lakini bado mengine yanabaki kuwa changamoto.

“Yapo matatizo kadhaa hapa, tunajaribu kuyatatua kwa kukutana na viongozi wa klabu husika na kufanya nao vikao na semina, kuna ambayo tumeyatatua na mengine bado.

“Kikubwa sisi hatukati tamaa, tunajitahidi kupambana nayo mpaka yatakapopata ufumbuzi ili soka letu la Tanga liweze kwenda mbele,” anasema Mgaya.

Mwenyekiti wa Sports

Mwenyekiti wa African Sports, Hassan Sheikh anakiri kuwa uchafu uliofanywa na Coastal Union katika kuchezea mikataba ya wadhamini inawafanya wapate ugumu wa kupata udhamini na kampuni mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwafuata zimekuwa zikieleza kukerwa na vitendo vya nyuma.

“Siyo kwamba nawaponda viongozi wa Coastal, ila wametupa wakati mgumu kila tunapokwenda kutafuta wadhamini, tukienda wanasema viongozi wa soka Tanga hatusomeki na hawawezi kufanya kazi na sisi.

“Mfano tulikwenda katika kiwanda cha saruji na wakasema hawataweza kufanya kazi na watu wa soka tena kwa kuwa Coastal ilishindwa kuheshimu mkataba wao, tunapata wakati mgumu sana,” anasema.

“Mfano mwingine ni Binslum, tumemfuata zaidi ya mara 10 na anasema kwa kile walichomfanyia Coastal Union hawezi kufanya kazi na timu za Tanga tena, tuna magumashi sana.

“Wakati mwingine viongozi tunapigana tena majungu kwa hawa wadhamini, unakwenda kuomba udhamini wakati unatoka unakuta kiongozi wa timu nyingine anaingia na akifika huko anakuponda tena ili usipate udhamini,” anasema.

Coastal wajitetea

Licha ya uongozi wa juu wa klabu ya Coastal Union kukwepa kutoa kauli baada ya Mwanaspoti kumsaka Mwenyekiti, Dk Ahmed Twaha bila mafanikio na Katibu Mkuu, Kassim El Siagi kugoma kusema na badala yake kumsakizia Msemaji wa timu, Oscar Assenga, klabu hiyo ikijitetea.

Assenga anasema klabu yake haijawahi kuwa na matatizo ya kuheshimu mikataba ya wadhamini na kuzitaka klabu nyingine ikiwemo wapinzani wao wa jadi, Sports kwenda kusaka wadhamini bila kuisemea Coastal bali wasake kwa ajili yao wenyewe.

“Niseme jambo moja, Coastal inafahamu mikataba, kama timu nyingine za Tanga zinaenda kusaka wadhamini, basi isimamie misingi yao na siyo kuiangalia Coastal walifanya nini,” alisema.

Hata hivyo, Assenga hakutaka kuzungumzia kwa undani suala la udhamini wa BinSlum na kuihimiza Sports kujitetea kivyao katika kusaka wadhamini.

“Siwezi kuyasemea hayo ya Sports, ila niwe muwazi kuwa Coastal inajitambua na inafahamu kitu gani inafanya, Sports wao wasimamie misingi yao wasituchanganye na sisi kwani sisi tuko kivyetu na wao wako kivyao, wasituingize kabisa katika mambo yao,” alisema Assenga.