Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umri mdogo, mpira mwingi

Muktasari:

Kwenye soka la Bongo kwa sasa kuna wachezaji kadhaa wenye umri mdogo ambao wanashika hatamu taratibu. Wana miaka michache lakini wamepewa majukumu makubwa na mpira wanaupiga mwingi kinoma. Makala haya yanawazungumzia kwa kina.

KILA zama zina mbuyu wake. Kila ufalme una zama zake. Wahenga walikuwa sahihi zaidi kutoa misemo hiyo ambayo katika soka inaonekana kuwa na maana kubwa. Ni eneo ambalo ufalme unabadilika kila wakati.
Ligi Kuu Bara imepita katika ufalme wa mastaa kibao. Kwa sasa kuna wachezaji ambao wanakula pensheni baada ya kutamba na kumaliza ufalme wao. Mmoja wao ni Fred Mbuna ambaye anacheza Majimaji ya Songea. Huyu jamaa alikuwa mfalme pale Yanga lakini zama zake zilishapita. Siku anaondoka Yanga alifanyiwa bonge la sherehe na watu walikula pilau.
Kwenye soka la Bongo kwa sasa kuna wachezaji kadhaa wenye umri mdogo ambao wanashika hatamu taratibu. Wana miaka michache lakini wamepewa majukumu makubwa na mpira wanaupiga mwingi kinoma. Makala haya yanawazungumzia kwa kina.

Aishi Manula, Azam
Miaka yake ni michache hajatimiza hata miaka 24 lakini anafanya kazi ya maana pale Azam. Anafanya kazi ya maana katika timu ya taifa pia. Tangu amepandishwa kucheza Ligi Kuu miaka mitatu iliyopita tayari ameshinda mataji matatu na Azam ambapo yote alionyesha uwezo mkubwa. Ameshinda taji la Ligi Kuu Bara, Kagame na Ngao ya Hisani. Kote huko alifanya kazi kubwa. Katika Kagame aliiwezesha timu hiyo kutinga nusu fainali baada ya kupangua penalti ya Haji Mwinyi kwenye hatua ya robo fainali. Kwenye Ngao ya Hisani alipangua penalti ya Hassan Kessy na kuipa timu yake ushindi. Ni dhahiri kuwa katika magokipa waliopo nchini kwa sasa, Manula ni bora zaidi.

Mohammed Hussein, Simba
Kuna watu wanapenda kumuita kiberenge. Wengine wanamuita mtu wa kazi, kwani ni mara chache sana kuona kicheko chake. Zimbwe anaingia mwaka wa tatu sasa tangu alipopata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba. Bado ni mdogo na hajatimiza miaka 23 lakini kazi yake inaonekana. Ana uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambulizi kupitia upande wake wa kushoto. Kuna nyakati ambapo inafurahisha kumtazama uwanjani. Kikubwa kwa sasa ni kwamba anaweza pia kusaidia kwenye kutoa pasi za mabao kutokana na mipira yake makini ya krosi na faulo. Kwa umri alionao na kazi anayofanya ni dhahiri kuwa anasogelea ufalme.

Hassan Kessy, Yanga
Hassan Kessy na mapozi yake kama alivyo. Kessy na umbo lake dogo kama alivyo. Kessy na kiburi chake kama alivyo lakini kwenye soka anafanya kazi ya maana. Nyota huyu hajafikisha miaka 23 lakini anafanya kazi ya maana pale Yanga. Ana uwezo mkubwa wa kukaba, kupanda kusadia mashambulizi na kupiga krosi. Kessy ana uwezo mkubwa pia wa kukokota mpira na kupiga chenga jambo ambao linamfanya kuwa beki ambaye amekamilika zaidi. Itawachukua Simba muda mrefu kupata mbadala wake baada ya kufanya uzembe na kumuacha atue Yanga.

Ibrahim Ajibu, Simba
Ibrahim Ajibu na uvivu wake wa mazoezi. Ibrahim Ajibu na mwili wake mdogo kama anavyoonekana lakini anaupiga mpira mwingi kinoma. Ajibu ndiyo kwanza ana miaka miwili tu Ligi Kuu lakini anafanya kitu ambacho hakifanywi na wachezaji wengi. Ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga, kukokota mpira na kufunga. Mara nyingi akiwa uwanjani huwa anafahamu anafanya kitu gani. Hata hivyo, pamoja na uwezo wake huo, makocha mbalimbali wamekuwa wakidai kuwa bado hajatumia kipaji chake vizuri. Wanaamini kuwa Ajibu ana uwezo mara mbili zaidi ya ule anaocheza kwa sasa.

Rafael Alfa, Mbeya City
Kijana mmoja hivi mstaarabu anacheza pale Mbeya City. Anaitwa Raphael Alfa ama wengine wanapenda kumuita Raphael Daudi. Anacheza kama kiungo wa juu japo pia anamudu kucheza kama kiungo mkabaji. Chipukizi huyu ana uwezo mkubwa pia wa kupiga mipira ya adhabu na kufunga. Tangu amepandishwa kikosi cha kwanza mwaka jana ameonyesha kwa nini timu hiyo ilikuwa inamsubiri kwa muda mrefu. Kwa sasa Mbeya City haina shida tena katika eneo la kiungo.

Farid Mussa, Tennerife
Unataka kusikia kitu gani kuhusu Farid Mussa? Bado hajatimiza miaka 22 lakini anafanya kazi kubwa uwanjani. Alikuwa chachu ya Azam kushinda kombe la Kagame mwaka jana. Farid ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira na kupiga chenga. Anajua pia kufunga. Kwasasa anaupiga mpira mwingi kwelikweli. Azam tayari imekubali kumuuza kwenda Tennerife ya Hispania.

Waziri Junior, Toto Africans
Yawezekana hazungumzwi sana lakini Waziri Junior ni miongoni mwa vijana wadogo wanaopiga mpira mwingi. Anacheza pale Toto Africans kwa msimu wa pili sasa lakini tayari ameonyesha kuwa ana safari nzuri mbele. Msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji wachache ambao walifunga mabao matatu katika mchezo mmoja (hatrick). Msimu huu tayari ameanza kwa kuifungia Toto bao la ushindi dhidi ya Mwadui. Hakika anaonyesha kitu.

Shiza Kichuya, Simba
Kwenye winga ya kulia ya Simba kuna jamaa mmoja mfupi anatumia mguu wa kushoto. Anaitwa Shiza Kichuya. Jamaa anaupiga mpira mwingi kwelikweli. Ana kasi, kontroo ya maana na uwezo wa kufunga pia. Kichuya bado hajafikisha miaka 22 lakini uwezo wake hauna mashaka. Msimu uliopita alikuwa kinara wa mabao katika klabu ya Mtibwa Sugar licha ya kucheza pembeni kama winga. Pengine chipukizi huyu anaweza kuwa mchezaji hodari zaidi baadaye.