Umafia wa Gamondi kwa Simba ni huu

Muktasari:

  • Mara ya mwisho Simba kupoteza ndani na nje dhidi ya Yanga ilikuwa mwaka 2014 ambapo historia hiyo imekuja kujirudia msimu huu tena Wekundu wa Msimbazi wakipoteza kwa jumla ya mabao 7-2 baada ya katika raundi ya awali kupasuka mabao 5-1 kisha hiki kipya cha mabao 2-1.

KAMA kuna kitu kinawaumiza Simba basi ni kitendo cha kikosi chao kupoteza mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara ndani ya msimu mmoja tena dhidi ya Yanga, jambo ambalo rekodi zinaonyesha halikutokea kwa miaka 10 iliyopita lakini shida hiyo imesababishwa na hawa akiwemo Miguel Gamondi.

Mara ya mwisho Simba kupoteza ndani na nje dhidi ya Yanga ilikuwa mwaka 2014 ambapo historia hiyo imekuja kujirudia msimu huu tena Wekundu wa Msimbazi wakipoteza kwa jumla ya mabao 7-2 baada ya katika raundi ya awali kupasuka mabao 5-1 kisha hiki kipya cha mabao 2-1.

Simba ilimfukuza kocha Mbrazili Roberto Oliveira 'Robertinho' baada ya kupigwa mabao 5-1 na kumleta mpya Abdelhak Benchikha ambaye naye hakunusurika akipasuka 2-1 wiki iliyopita.

Kuna mambo kadhaa ambayo Mwanaspoti imeyaona katika ubabe wa Gamondi dhidi ya makocha wote wawili wa mwisho Simba.

Mbinu hizi
Kitu cha kwanza ambacho Gamondi amefanikiwa kuwaumiza wapinzani wake hao wawili ni mbinu ya kikosi chake kuwa na kasi ya kukaba kuanzia juu yaani eneo la wapinzani la ulinzi inapoanzisha mashambulizi.

Simba haikujiandaa sawa sawa kukabiliana na ubora huo ambapo ikajikuta inafanya makosa ambayo kwenye mchezo uliopita wa Aprili 20 ndio ulisababisha bao la kwanza baada ya Stephanie Aziz KI na Joseph Guede kumbana vizuri beki wa Msimbazi, Hussein Kazi na kujikuta anapiga pasi mbovu iliyonaswa na KI, ambaye aliingia ndani ya boksi kwa kasi na Kazi kumchezea faulo iliyozaa penalti ya bao.

Yanga ya Gamondi pia inasifika kwa kuwa na kasi inaponasa mpira kwenda kwenye lango la wapinzani huku wachezaji wake wakijipanga sawasawa kwa kuongezeka idadi katika eneo la mpinzani kwa haraka wakati inasukuma mashambulizi jambo ambalo limekuwa likiinufaisha kupata mabao kwenye mechi hizo mbili.


Simba hawana kasi
Simba ya Benchikha ingeweza kuzuia aibu ambayo imeipata kwa Yanga lakini nayo ikakutana na wakati mgumu inapounasa mpira kutoka kwa Yanga kwa kasi ndogo ya kuelekea lango la wapinzani wao ikijikuta inakuwa na wachezaji watano mpaka sita huku timu ya Wananchi ikiwa na wachezaji saba hadi wanane. Kibu Denis ndiye mtu pekee anayeonekana kuwa na kasi ya kutosha Simba ikifanya mashambulizi.


Yanga wana pumzi
Kocha wa mazoezi ya viungo Taibi Lagrouni ndiye mtu anayeonekana kuwaadhibu Benchikha na mtangulizi wake kutokana na kufanikiwa kuwajaza pumzi sawasawa wachezaji wa Yanga kwa kujua kusaka mpira inapopoteza.

Yanga imeendelea na ubora wa msimu huu kwa kuhakikisha hakuna mpizani anayeweza kupiga pasi kumi kwenye eneo lao ambapo Simba licha ya kupiga pasi 235 zilizowafikia walengwa kwenye mchezo dhidi ya watani wao, lakini ni pasi 57 pekee walizipiga kwenye nusu ya wapinzani wao.

Simba ilikuwa ikipiga pasi tano mpaka nane kwenye eneo la Yanga lakini baadaye ikajikuta inaupoteza mpira kutokana na nguvu ya wachezaji wa Yanga kusaka mpira kwa haraka.


WASIKIE MAKOCHA
Tuanze na kocha George Lwandamina ambaye aliuangalia mchezo huo akiwa kwao Zambia ambaye alisema Simba kupata ushindi kwenye mchezo huo ilikuwa inategemea na usiriazi wa wachezaji wa Yanga baada ya timu yake hiyo ya zamani kuonyesha kuwa imara kwa mbinu kuliko wekundu hao.

Lwandamina alisema wachezaji wa Yanga kama wangekuwa na utulivu wangeweza kutengeneza ushindi mkubwa kutokana na kuwazidi kasi wenzao wa Simba kwani kila walipofika jirani na lango la wapinzani wao walikuwa hatari zaidi.

"Nadhani Yanga hawakutaka kushinda zaidi au kuwa na njaa ya ushindi mkubwa hii nayo ilikuwa mechi yao, Simba walianza kwa kasi lakini baadaye wakashuka na kuanza kucheza taratibu sana kufuata kasi ya Yanga, wangeweza kupoteza vibaya zaidi kama wasingekuwa watulivu," alisema Lwandamina.

"Yanga kikosi chao kimetengenezwa kwa pumzi ya kutosha na wana kasi sana ya kutafuta mpira na hata kupandisha mashambulizi kuelekea lango la wapinzani, hiki kinazihukumu timu nyingi hapo Tanzania."

Naye kocha wa zamani wa Simba, Goran Kopunovic alisema Simba inakabiliwa na wachezaji wengi waliokosa kasi endapo kama makocha wao walifanya kazi nzuri ya kuimarisha pumzi za wachezaji wao.

"Simba ilikuwa taratibu sana wakati haina mpira na hata ikiwa na mpira hata bao ambalo walifunga ni akili tu ya mtu aliyepiga pasi lakini bado Yanga ingeweza kulizuia kama wangekuwa makini kidogo tu," alisema Kopunovic ambaye amewahi kuifunga Yanga kwa bao 1-0.

"Sijajua ni shida ya wachezaji au makocha hawakuimarisha vizuri pumzi za wachezaji, ulikuwa unaona kabisa tofauti ya kasi ya Yanga na wao, Yanga ilikuwa ikipeleka mashambulizi unaona kasi yao na hata ikipoteza mpira inapambana sana kuutafuta kwa haraka.

"Nidhamu hii pia Yanga iliwasaidia sana ilipocheza dhidi ya Mamelodi Sundowns, ilikuwa inaonekana kwamba Yanga inawalazimisha Mamelodi kucheza kwenye eneo lao na sio eneo la Yanga, kuna kazi ya kufanyika pale Simba."