Mbeya City yashtuka, kumkalia kikao Mayanga

Muktasari:

  • City iliyoshuka daraja msimu wa 2022/23, imemaliza Championship nafasi ya sita kwa pointi 37, huku ikiongozwa na Salum Mayanga ambapo matarajio yao yalikuwa ni kurejea Ligi Kuu msimu ujao.

Baada ya kumalizika kwa Championship, uongozi wa Mbeya City umekiri kutofikia malengo ukiahidi kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao, huku ishu ya benchi la ufundi ikisubiri kikao cha bodi.

City iliyoshuka daraja msimu wa 2022/23, imemaliza Championship nafasi ya sita kwa pointi 37, huku ikiongozwa na Salum Mayanga ambapo matarajio yao yalikuwa ni kurejea Ligi Kuu msimu ujao.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema hawakufikia malengo yao kutokana na mabadiliko ya uongozi na maandalizi ambayo hayakuwa bora kulingana na matarajio.

Alisema jambo jingine ni kutoelewa zaidi mwenendo wa Championship, hivyo msimu ujao watajiandaa zaidi.

“Suala la kocha mkuu Mayanga linasubiri kikao cha bodi kwakuwa ameshawasilisha ripoti akipendekeza mambo gani yaboreshwe, sisi uongozi tutajipanga mapema msimu ujao,”  alisema Ally.

Kigogo huyo alisema kati ya mambo watakayofanya mapema ni usajili kulingana na mahitaji ya timu, kambi, bajeti na ushirikishwaji wa mashabiki.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Mbeya, (Mrefa), Sadick Jumbe alisema baada ya kufanikisha kuipandisha Ligi Kuu Bara Ken Gold, msimu ujao nguvu zote ni kwa Mbeya City.