Ulimwengu aliamsha dude Sudan

Muktasari:

Iko hivi. Kuna jamaa mmoja Mbrazil anaitwa Giovanni Marne alikuwa akitumikia adhabu, sasa amerudi na pale Al Hilal Omdurman ndiye mtu pekee anayeitishia namba ya Ulimwengu.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Mtanzania Thomas Ulimwengu itambidi akaze kweli kujihakikishia namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha AL Hilal ya Sudan.

Iko hivi. Kuna jamaa mmoja Mbrazil anaitwa Giovanni Marne alikuwa akitumikia adhabu, sasa amerudi na pale Al Hilal Omdurman ndiye mtu pekee anayeitishia namba ya Ulimwengu.

Ulimwengu aliyejiunga na Al Hilal, Mei 22 mwaka huu, hadi sasa  amepachika mabao matatu katika michezo miwili aliyocheza ya Ligi Kuu Sudan na kurejea kwa Giovanni wakati Ulimwengu akiwa ameuwasha moto wake ni wazi sasa itabidi akaze ili kuzuia kupokwa namba kwenye kikosi hicho ambacho kinapewa nafasi  kubwa ya kutwaa ubingwa wa Sudan.

Mara baada ya kujiunga na timu hiyo, Ulimwengu aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kuwaacha midomo wazi  wazawa wanne na Wanigeria wawili ambao wamekuwa wakisugua benchi.

Nyota hao ni Al Sadig Adam, Mudather El Tahir, Walaa Eldin na  Mohamed Eldai ambao ni raia wa Sudan pamoja na Shobowale Azeez na Haruna Zambuk Garba, raia wa Nigeria.

MBIO ZA UBINGWA

Al Hilal wanaongoza kundi A kwa upande wa Sudan na hivyo kuwa moja ya timu zitakazofuzu hatua ya mchujo kuwania ubingwa pamoja na timu za nne nyingine za Sudan.

Zilizotoka kundi A,  ni Al Hilal Omdurman, Hilal Obayed, Al Khartoum na Al-Ahly Merowe huku kwa upande wa Kundi B  ni Al Merreikh, Al Ahly Shendi, Merreikh El-Fasher na Hay Al Arab.