Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukweli ndivyo ulivyo: Kina Mkude wasije wakamlaumu mtu!

Muktasari:

Kabla ya kikosi cha wachezaji 32 na jopo lao la makocha hakijapaa, zile nongwa za mashabiki na wadau wa soka zilianza upyaa! Kisa? Kutemwa kwa Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude.

MASHUJAA wa Tanzania wamepaa. Wanaenda kupigania heshima ya nchi. Wanaenda kupeperusha Bendera ya Taifa ughaibuni. Naizungumzia, Taifa Stars ambayo imepaa juzi Jumamosi kwenda Misri kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.
Stars imekwenda kama mashujaa wa kweli wa nchi, hata kama kuna wadau wa soka wanaona eti iliagwa kinyonge pale White Sands! Nongwa za mashabiki buana! Eti, Stars kuagwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza kwao ni unyonge.
Wenyewe walikuwa na kiu kubwa ya kuona Stars ikiagwa na Rais John Magufuli au Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kama sio Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe. Unajua kwa nini? Stars inaenda kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo tangu iliposhiriki mwaka 1980. Yaani miaka karibu 39. Ni miaka mingi mno.
Mashabiki wa soka walikuwa na hamu ya kuwaona mashujaa wao hao wakiagwa kama walivyoagwana Rais wao, Uhuru Kenyatta. Uganda The Cranes waliopo Abu Dhabi, Falme za Kiarabu (UAE) waliagwa na Rais wao, Yoweri Museveni, achilia mbali timu nyingine shiriki za nchi hizo zilizoagwa na kukabidhiwa bendera na viongozi wa juu wa chini zao.
Binafsi sioni tatizo kwa Stars ilivyoagwa, kwani inawezekana Rais na hata Waziri Mkuu walitingwa na shughuli za kiserikali. Kitu muhimu ni kile ambacho waliambiwa na wao kuahidi mbele ya naibu waziri wakakifanyie kazi Misri.
Kwa mara ya kwanza Watanzania huenda wasitapetape kusaka timu za kushabiki kwa vile Stars ipo Misri. Miaka zaidi ya 30 wengi walikuwa wakibadilisha timu za nchi kila fainali hizo zilipokuja na nyingine kubwa duniani zikifanyika kwa lengo za kushabikia, kwa vile Tanzania haikuwahi kunusa. Safari hii timu yao imo, kwa nini wasipagawe? Stars walio Kundi C,  wataanza na Senegal, kisha kurudi tena uwanjani siku chache baadaye kuvaana na Kenya na kumalizia mapema Julai dhidi ya Algeria. Furaha iliyoje?
Hata hivyo, kabla ya kikosi cha wachezaji 32 na jopo lao la makocha hakijapaa, zile nongwa za mashabiki na wadau wa soka zilianza upyaa! Kisa? Kutemwa kwa Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude.
Cha kustaajabisha, sio Mkude na Ajibu tu waliotemwa. Kuna orodha ya nyota wengine watano waliokuwa wameitwa na Kocha Emmanuel Amunike katika kikosi chake cha awali cha wachezaji 39. Wamo Shomary Kapombe, Kennedy Juma, Ali Ali, Ayoub Lyanga na Kassim Hamis. Nani hajui Kennedy kaifanyia nini Singida United katika Ligi Kuu misimu miwili inayoshiriki?
Nani hajui mziki wa kina Ayoub Lyanga na Kassim Khamis katika timu zao za Coastal Union na Kagera Sugar? Ni nani asiyejua beki Ali Ali alivyoisaidia KMC kumaliza nafasi ya nne na kufuzu michuano ya kimataifa msimu ujao?
Mbona hawa hawapigiwi kelele? Mbona hakuna mijadala juu ya kutemwa kwao na mjadala uwe kwa kina Ajibu? Au ni kwa sababu hawazichezei Simba na Yanga?
Bahati nzuri, Amunike kama walivyo makocha wengine wa kigeni, huwa hawajui kuficha kitu ama kupindisha maneno. Mnigeria huyo amefichua kilichomfanya awateme nyota hao. Nidhamu na kushindwa kujituma mazoezini ni jambo lililowaponza. Huwezi kuwa na askari kwa maandalizi ya vita lakini wala hana nidhamu au kuwa siriazi na maandalizi hayo. Askari wa hivyo wa nini? Anaweza kuliponza jeshi na kulifelisha uwanja wa mapambano.
Mashabiki wanataka nini cha zaidi kwa maelezo kama hayo ya kuachwa kwa wachezaji hao? Ni nani hajui Mkude na Ajibu walivyo katika suala la nidhamu? Nimefurahi sana kuupitia ujumbe wa nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga na Taifa Stars kwa mafanikio makubwa, Amri Kiemba.
Kiungo huyo fundi anayezeeka na kipaji chake alichokiheshimu na kukitumikia kwa nidhamu ya hali ya juu, ameandika ujumbe ambao kila mwenye akili timamu ameuelewa. Ukweli ndivyo ilivyo, Mkude na Ajibu lazima wajiulize kwa nini wao tu kila mara?
Badala ya kuanza kumnyooshea kidole Amunike, ni vyema kwanza mashabiki wakaanza na nyota hao, bila ya shaka wana matatizo na lazima tuwasaidie.
Ni kweli ni wachezaji hao wana vipaji vya hali ya juu vya soka, lakini soka bila nidhamu na kujituma iwe mazoezini ama uwanjani kwenye mechi ni kitu kinachofelisha. Kina Ajibu wanafelishwa na kitu hicho, hata kama kuna watakaochukia kwa kusema hili wachukie tu!
Kocha Mwinyi Zahera amewahi kunukuliwa mara kadhaa juu ya tabia za Ajibu. Hata alipokuwa Simba, alikuwa pia akilalamikiwa kwa uvivu wa mazoezi. Inadaiwa huwa anaenda anapojisikia pia kuyafanya pale anapopenda tu. Kocha Zahera alimsaidia kwa kuamua kumpa unahodha Yanga ulioibua mjadala baada ya kumnyang’anya kitambaa, Kelvin Yondani. Zahera alifichua alifanya hivyo kwa lengo maalumu. Alikiona kipaji halisi cha soka katika miguu ya Ajibu, lakini kilififishwa na uvivu wake.
Aliamini unahodha ungemfanya abadilike na kuyapenda mazoezi na kuyafanya kwa bidii ili kupandisha kipaji hicho. Alichemka, kwani fundi huyo wa mpira alikuwa kama ana homa ya vipindi, kipindi hiki anakuwa moto, ghafla tu watu wakijiandaa kuona utamu zaidi anakuwa baridiiii!
Mkude kadhalika ishu ya nidhamu imekuwa ikielezwa kwa muda mrefu tangu alipopandishwa kikosini mwanzoni mwa miaka ya 2010 akitokea Simba B.
Kocha Joseph Omog, alijiingiza matata alipojaribu kumzindua kiungo huyo mkabaji kwa kumpiga chini kwenye kikosi chake cha kwanza na kumpa nafasi James Kotei na viungo wengine.
Kocha huyo Mcameroon alishambuliwa na mashabiki wa Simba, licha ya kutoa ufafanuzi na mwishowe akaona isiwe tabu akamrejesha kikosini, ili tu kibarua chake kiwe salama.
Hakuna ubishi Mkude anajua soka, akipiga kazi lazima utampenda ni kama Ajibu tu. Lakini anaponzwa na nidhamu yake wakati mwingine ikielezwa ni ile ya nje ya uwanja zaidi. Bahati nzuri ni kwamba ni mmoja wa nyota wenye kupendwa na mashabiki kama ilivyo kwa Ajibu, ndio maana kila likitokea la kuwatokea hasa mbele ya makocha wao iwe wa klabu zao ama wale wa timu ya taifa, hupata watetezi watokwao povu.
Hata hivyo, wakati mwingine ni kama makocha wanaonewa na kuwatia kiburi cha bure nyota hao na kushindwa kuwasaidia kuamka usingizini.
Mkude na Ajibu hawatofautiana kiumri na Mbwana Samatta ama Simon Msuva, Himid Mao, lakini mashabiki walishawahi kujiuliza kwa nini wenzao wako hapo walipo kwa sasa? Kina Msuva, Samatta na Himid wote wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi kama ilivyo kwa kina Farid Mussa, Yahya Zayd, Shaaban Idd Chilunda ambao kiumri wamewaacha kidogo kwa sababu wametambua thamani ya vipaji vyao na kuvitumikia kwa uaminifu.
Nidhamu na kupenda kupokea ushauri wa maana wa kulinda vipaji vyao vimewasaidia,  kitu ambacho hata marafiki wa karibu wa kina Mkude wanapaswa na kuwasaidia nyota hao ikizingatiwa wakati ukuta.
Mashabiki wa soka wa ukweli na wenye nia ya dhati wanaowatakia mazuri kina Mkude, ni lazima waumizwe na mambo wanayokutana nayo.
Lakini inawezekana hawana cha kuwasaidia kama wenyewe hawatajisaidia, kwani kila mchuma janga hula na wakwao. Kiemba amefafanua vizuri ni wajibu wa nyota hao kuupitia upya na kuusoma ujumbe wake, ili wauelewe kisha kuufanyia kazi na inshallah miezi kadhaa ijayo nyota hao wawe wakifurahia neema na vipaji walivyojaliwa.