Ukweli ndivyo ulivyo! Kina Ajibu kuna mahali wanakwama!

Muktasari:
Bao la Stars iliyotangulia lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Shadrack Nsajigwa dakika mbili kabla ya pambano kumalizika. Wengi waliamini Stars ilikuwa ikienda Nusu Fainali kwani msimu huo timu zilizofuzu fainali zilikuwa nane tu, tofauti na fainali nyingine zilizofuata baadaye zilizoshirikisha timu 16 kama ilivyo sasa.
SIJAJUA nyota wa sasa wanaokipiga kwenye soka wamekwamia wapi? Wamekumbwa na mdudu gani? Pia hata sijui aliyewaroga! Unajua kwa nini? Wiki chache zijazo panapo majaaliwa, kama Virusi vya Corona, havitazingua kule Cameroon. Zitafanyika Fainali za Sita za Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, yaani Chan 2020.
Hakuna asiyejua kama Tanzania nao kwa mara nyingine itakuwepo kwenye fainali hizo. Imepangwa Kundi D na timu za Zambia, Namibia na Guinea.
Kwa wale wasiosahau, Tanzania ilienda mara ya kwanza kwenye fainali hizo mwaka 2009 zilizokuwa za kwanza kabisa tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo. Ilienda Ivory Coast ikiwa chini ya Kocha Mbrazili, Marcio Maximo. Kwenye mechi za mwaka huo, Tanzania ilipangwa kundi moja na Zambia, Ivory Coast na Senegal.
Lilikuwa kundi gumu kwelikweli na ndio maana haikushangaza kuona Taifa Stars ikimaliza nafasi ya tatu katika kundi lao, ikikusanya alama tatu tu na mabao mawili. Ndio mabao mawili tu.
Moja waliwafunga wenyeji kwenye pambano lao la ushindi. Mrisho Ngassa, huyu huyu Anko wa Yanga, ndiye alifunga bao hilo katika mchezo wao wa pili. Stars ilianza kwa kipigo kutoka kwa Senegal, kisha kumalizia kwa sare ya 1-1 dhidi ya Chipolopolo.
Bao la Stars iliyotangulia lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Shadrack Nsajigwa dakika mbili kabla ya pambano kumalizika. Wengi waliamini Stars ilikuwa ikienda Nusu Fainali kwani msimu huo timu zilizofuzu fainali zilikuwa nane tu, tofauti na fainali nyingine zilizofuata baadaye zilizoshirikisha timu 16 kama ilivyo sasa.
Lengo langu sio kuzungumzia mechi hizo za miaka 10 iliyopita. Hapana! Ila mnakumbuka kikosi kilichoenda Ivory Coast. Maximo alienda na majembe yake 23 ambao timu zao kipindi hicho zikiwa kwenye mabano kisha ndipo tuitarudi kwenye mada ya leo.
Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (JKT Ruvu), Deo Munishi ‘Dida’ (Simba), Shaaban Dihile (JKT Ruvu), Farouk Ramadhan (Miembeni), Shadrack Nsajigwa (Yanga), Salum Sued (Mtibwa Sugar), Nadir Haroub ‘Cannavaro (Yanga), Kelvin Yondani (Simba), Juma Jabu (Simba), Amir Maftah (Yanga) na Nurdin Bakar (Yanga).
Wengine ni; Henry Joseph (Simba), Geofrey Bonny (Yanga), Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Haruna Moshi ‘Boban’ (Simba), Nizar Khalfan (Moro United), Athumani Idd ‘Chuji’ (Yanga), Abdi Kassim ‘Babi’ (Yanga), Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Jerson Tegete (Yanga), Mrisho Ngassa (Yanga) na Kigi Makasi (Yanga).
Ukichungulia kikosi hicho utabaini kuna majina yaliyoenda Cha 2009 bado wamo wakiendelea kukimbizana na vijana katika Ligi Kuu Bara na hata Daraja la Kwanza (FDL), tena wakiwafunika kabisa mayanki ambao wamekuwa na kama homa ya vipindi juu ya viwango vyao.
Ngassa bado yumo. Yondani, Nyoni, Kazimoto, Dida, Nditi, Chuji, Boban, Makassy, Tegete, Nizar na Henry nao wanaendelea kukimbiza, hata kama sio kwa kiwango chao cha zamani. Hapo ndipo ninapojiuliza, hiki kizazi cha kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Juma Mahadhi na wenzao kibao, wana uwezo wa kudumu uwanjani kwa miaka mingi kama hiyo walivyofanya kina Chuji?
Ukimwangalia Nditi ambaye ni mmoja ya nyota waliocheza katika Ligi Kuu kwa muda mrefu ni fundi zaidi kuliko hata Jonas Mkude? Inashangaza! Ukiangalia Kiggy Makassy anavyoteleza uwanjani, unaweza kudhani ni dogo wa juzi juzi. Mwangalie Nyoni na Yondani walivyo lulu ndani ya klabu zao na Taifa Stars.
Imekuwaje wao wamemudu muda mrefu, wakati madogo wanaocheza soka kwa sasa hawatii matumaini.
Kuna mahali wanakosea na lazima wabadilike! Lazima wajifunze kitu toka kwa wakongwe wanaoendelea kusumbua kwenye Ligi Kuu Bara.
Inashangaza kidogo, eti Hussein Javu ana mabao mengi kuliko Ajibu? Javu ana manne. Inachekesha eti, Tegete, Ngassa na Makassy wana mabao mengi kuliko Mohammed Ibrahim ama Salum Kihimbwa!
Kama ni vipaji, vijana wa sasa wanavyo na pia wamerahisishiwa mambo kutokana na teknolojia ya kuwatazama kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kama sio Neymar wanavyofanya yao uwanjani. Kwanini nyota wa sasa hawaendi na dunia ilivyo.
Kwa nini hawadumu kwenye viwango vyao kama ilivyokuwa kwa waliowatangulia. Yondani, hata kama ana umri mkubwa na kuonekana kushuka, bado ni mtamu kuliko Kennedy Wilson. Nyoni ni bora kuliko Yusuf Mlipili. Hili ni tatizo. Inawezekana watu wakasema labda nyota wa sasa wana mambo mengi, lakini wanaweza kuwashinda kina Boban na Chuji?
Mbona wanaendelea kuaminiwa na baadhi ya timu na kukinukisha uwanjani? Inashangaza kidogo kuona kila msimu ndani ya Ligi Kuu wanaibuka wachezaji wanaotamba msimu mmoja kabla ya kupotea msimu mwingine, lakini kina Makassy, Nyoni, John Bocco wakiendelea kupeta na kuitwa Stars.
Kwa hakika kama kina Ndemla na wenzake, wasipoamka au kuamshwa na washkaji zao wa karibu, wasitarajie wawe na maajabu miaka mitano ijayo. Pia kama vijana walioitwa Stars kwa fainali za CHAN 2020 wasipoamka na kujitoa, wajue mapema watarudi na aibu kuliko ile ya kina Dida na wenzake kule Ivory Coast. Wala Msibishe!